Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Askari wadaiwa kuua mpita njia Dar

ASKARI wa jeshi la polisi jijini Dar es Salaam amedaiwa kumpiga risasi Hassani Likanoga (24), mwanafunzi mtarajiwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati alipokuwa wakipiga risasi gari moja lililodhaniwa kuwa ni la majambazi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Julai 10 mwaka huu majira ya saa nane mchana katika eneo la Tandika jijini Dar es Salaam wakati polisi walipokuwa wakifukuza gari hilo aina ya Toyota RAV 4.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Mwananchi kuwa, eneo la mtaa wa Mbwela uliopo Tandika uligeuka na kuwa Darfur kwa muda wakati mirindimo ya risasi ilipokuwa ikirushwa kutoka kwenye gari la polisi kuelekea kwenye gari lililokuwa mbele lililodaiwa kuwa ni la majambazi.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Shabani Ramadhani aliliambia Mwananchi "Nikiwa kibarazani nimekaa niliyaona magari matatu yakifukuzana, gari moja ndogo aina ya Toyota RAV 4 likiwa limetangulia na limefunga vioo vyote na nyuma yake kulikuwa na magari mawili, moja likiwa ni la polisi na jingine lilikuwa Suzuki ambalo baadaye niligundua kuwa lilikuwa likitumiwa na polisi."

Alisema risasi hizo zilianza kurushwa muda mfupi baada ya magari hayo kuacha barabara ya lami inayoelekea Tandika na Mwembe Yanga na kuelekea barabara ya Vumbi inayokatisha mtaa wa Mbwela.

Alisema risasi hizo ambazo zilianza kurushwa mfululizo zililifanya eneo hilo kuwa katika hali ya hatari kwani zingine zilirushwa juu, nyingine chini na nyingine zililenga usawa wa gari walilokuwa wakilifukuza.

"Risasi hizo ambazo muda wote zilipigwa ovyo nyingine zilipigwa juu na nyingine chini huku nyingine zikilenga gari walilokuwa wakilifukuzia zikitokea kwenye gari la polisi ambalo nyuma yake kulikuwa na askari wawili tu,"alisema Ramadhani.

Alisema muda mfupi baadaye aliona mtu akianguka chini baada ya kupigwa risasi iliyotoka kwenye gari la polisi na ulipotoweka msafara huo walikwenda kumwangalia na kukuta marehemu akiwa amejeruhiwa sehemu ya shingoni huku damu ikimtoka kwa wingi.

Alisema baada ya tukio hilo lilijitokeza kundi kubwa la wasamaria wema akiwamo yeye na kwenda kutoa msaada kwa kijana huyo kwa lengo la kumpeleka hospitalini.

"Ingawa tulikuwa hatumjui, lakini kwa tukio lile tuliloliona sote tulijua wazi kuwa hakuwa jambazi, hivyo umati mkubwa watu ulilazimika kukimbnilia hapo na kuanza kutoa msaada wa kila namna ikiwa ni pamoja na kufanya juhudi za kumkimbiza hospitalini," alisema Ramadhani.

Kwa upande wake George Kiondo alifafanua kuwa kazi ya kumtafutia usafiri kijana huyo iligeuka kuwa ngumu baada ya magari yaliyokuwa yakipita katika eno hilo kukataa na kukimbia.

"Tulisimamisha gari la kwanza likakimbia, tukasimamisha la pili likakimbia ndipo tulipoamua kwa umoja wetu kutanda barabarani na kuzuia magari yote yaliyokuwa yanapita hapo kisha tukafanikiwa kumnyang'anya ufunguo dereva mmoja na kumlazimisha kumpakia kijana huyo kwa ajili ya kwenda hosptalini," alisema Kiondo.

Kiondo alibainisha adha nyingine waliyokutana nayo kuwa walipokuwa wakijitayarisha kumpakia kijana huyo gari lililodaiwa lilikuwa likitumiwa na Polisi aina ya Suzuki lilifika katika eneo hilo na kushuka askari mmoja kisha kuanza kufyatua risasi hewani huku akiwataka watu wote kutawanyika.

Kiondo alisema tulisikia sauti ikisema "Tawanyikeni sitaki kuona mtu katika eneo hilo ondokeni haraka" akimnukuu askari huyo anayedaiwa alikuwa akifyatua risasi hewani.

Alisema kizaazaa hicho kiliwalazimu umati mkubwa wa watu waliokuwa wakijaribu kutoa msaada kwa kijana huyo kukimbia hivyo kubaki idadi ndogo ya watu waliosimama na kumsisitiza askari huyo kuwa eneo hilo halikuwa na ujambazi bali wao wanashughulikia suala la kumpeleka kijana aliyekuwa amejeruhiwa kwa risasi hospitalini.

Alisema baada ya polisi huyo kuelezwa hivyo alirudi kwenye gari na kuondoka na ndipo wao walipompakia kijana huyo kwenye gari na kumpeleka kituo cha polisi cha Chang'ombe ambako walipewa PF3 na kumpeleka kijana huyo katika hosptali ya Temeke kwa ajili ya matibabu.

Mwananchi alipomtafuta Kamishna msaidizi wa Polisi na kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam Sulemani Kova alisema,"Kwa kuwa tukio hilo limetokea Temeke wasiliana na Kamanda wa huku atakupa maelekezo yote"

Kamanda wa mkoa wa Temeke Liberatus Sabas alipopigiwa simu mara ya kwanza alijibu akisema alikuwa kwenye gari hivyo kumtaka Mwanandishi kumtafuta baadaye.

[ Read More ]