Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Fuso laua watu watano Moro

WANUNUZI watano wa mahindi  wamekufa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya tairi la gari walilokuwa wakisafiria, kupasuka na kusababisha gari hilo kupinduka,  katika eneo la Magubike katika Barabara ya Dodoma- Morogoro.Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Adolphina Chialo, aliwataja waliokufa katika ajali hiyo juzi usiku kuwa ni Mwarami Abdallah, mkazi wa Mzense jijini Dar es Salaam, Selemani Ngula (30), Kasimu Mwitago (30).

Kwa mujibu wa kamanda huyo, maiti mwingine ametambuliwa kwa jina moja la Kiejo (30) wakati mwingine hajatambuliwa. Chialo pia aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni, Timoth Paul,  Elisafi Mkumbwa na Hamisi Selemani, wote wakazi wa Kibaigwa  na kwamba majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Alisema gari hilo lilikuwa linatokea katika Kijiji cha Kibaigwa, wilayani Kilosa kwenda jijini Dar es Salaam na kwamba chanzo cha ajali ni mwendo mkali.Alisema watu hao walikuwa wanasafiri kwa kutumia gari aina ya Mistubish Fuso iliyokuwa ikiendeshwa na Jackson Bezaleli Senyegwa (27) mkazi wa Kibaigwa ambaye alitoroka mara baada ya ajali hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi katika wodi namba moja,mmoja wa majeruhi Hamisi Selemani, alisema gari hilo lilikuwa limebeba gunia 100 za mahindi, jambo lililosababisha  moja ya matairi kuelemewa na kupasuka.

Alisema abiria wote waliokuwa nyuma ya gari hilo walifariki papo hapo baada ajali na kwamba walifunikwa na mahindi.Kamanda huyo alisema miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, na kuomba wananchi kujitokeza ili kutambua miili ambayo haujatambuliwa.
[ Read More ]

Vijana wa Zanzibar kupata mafunzo ya kujiajiri kutoka India





VIJANA wanaomaliza vyuo vikuu vya Zanzibar wataanza kunufaika na utaratibu wa kupatiwa mafunzo maalumu ya biashara pamoja ufundi yatakayowawezesha kufungua miradi kujiajiri na kuwaajiri vijana wengine na kukuza hali zao za maisha.

Utaratibu huo unatarajiwa kutekelezwa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika kati ya ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar unaoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (IT&C) ya Andhara Pradesh yaliyofanyika Hoteli ya Grand Kakatiya mjini Hyderabad.

Mbali na hatua hiyo Serikali ya Andhra Pradesh imemwomba Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi kuandaa utaratibu utakaowezesha Zanzibar kunufaika na makubaliano yaliyofikiwa katika ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais kukuza mashirikiano katika nyanja za kiuchumi, biashara, kilimo na elimu kwa faida ya nchi mbili hizo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Serikali ya Andhra Pradesh, Pannola Lakshmaiah alisema utaratibu huo unapaswa kuandaliwa mikakati ya ya utekelezaji mapema ili Serikali mbili hizo hasa Zanzibar iweze kunufaika mapema na kuchangia harakati zake za kuinua hali yake ya kiuchumi.

Alisema Jimbo la Andhra Pradesh limepata heshima kubwa duniani kote kwa Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (IT), ambapo pia katika eneo hilo kunapatikana mji maalum wa Teknolojia ya Mawasiliano (Hyderabad Technology City) unaotoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa eneo hilo na India kwa ujumla.

“Jambo muhimu tutiliane saini makubaliano ya mashirikiano leo hii jioni (jana) na kitakachofuata Balozi aandae utaratibu wa utekelezaji kwa vile hakuna muda wa kusubiri, teknolojia ya habari na mawasiliano hivi sasa ni ajira ni uchumi ni kila kitu”, alisema Waziri wa IT& C.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdallah Shaaban alisema bado Zanzibar iko nyuma katika elimu ya IT&C, licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukulia kuinua elimu hiyo, ukiwamo mpango mahsusi ulioanzishwa na Serikali ya Zanzibar uitwao E -government.

Waziri Shaaban alisema kuna haja Serikali ya Andhra Pradesh ambapo inafanana kiutawala na Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano kushirikiana kuandaa utaratibu wa masomo kwa vijana wa Zanzibar.

Alisema kazi hiyo inaweza kufanikishwa chini ya utaratibu wa kupeleka wataalamu Zanzibar kutoa mafunzo hayo au vijana wa Zanzibar kwenda India kujifunza na baadaye kurudi nyumbani kutumia ujuzi huo kwa maslahi yao na nchi.    

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed  Mazrui alisema Zanzibar kuna vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu na kukaa muda mrefu bila ya kupata ajira na utaratibu huo utawasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa ajira na kuwapa mafunzo ya kazi maalumu za amali zitakazosaidia kuimarisha maendeleo.

Waziri Mazrui alisema maeneo mengine ambayo Zanzibar inaweza kunufaika katika mashirikiano na Andhra Pradesh ni usindikaji wa bidhaa kama vile za matunda, viungo pamoja na mazao ya baharini.

Waziri Mazrui alisema Zanzibar imejaaliwa kuna rasilimali za viungo kama vile karafuu zao ambao linasafirishwa kwa wingi kwenda India na kama kutakuwa na utaratibu wa kufanyiwa ‘branding’ na baadaye kusafirishwa litaweza kupata soko kubwa zaidi ya sasa katika soko la dunia.
[ Read More ]

Bomu Lililofichwa Kwenye Kilemba Lamuua Rais Mstaafu wa Afghanistan





Aliyekuwa rais wa Afghanistan Burhanuddin Rabbani ameuliwa baada ya mtu aliyelificha bomu kwenye kilemba chake kulilipua bomu hilo wakati wakisalimiana.
Rais Burhanuddin Rabbani ambaye pia alikuwa ndiye mkuu wa baraza kuu la kutafuta amani nchini Afghanistan, alifariki dunia baada ya mtu aliyekuwa akimuamini kumgeuka na kujilipua kwa bomu alilolificha kwenye kilemba chake.

Wasaidizi wanne wa Rabbani nao walifariki dunia baada ya bomu hilo kulipuka wakati Rabanni aliposimama kumsalimia kwa kumkumbatia mwakilishi wa Talibani baada ya kumalizika kwa mazungumzo marefu baina yao ya kutafuta suluhisho la amani nchini Afghanistan.

Fazel Karim Aymaq ambaye ni mjumbe wa baraza la amani la Afghanistan alisema kuwa watu wawili wanaoaminika sana walifika nyumbani kwa Rabbani mjini Kabul ili kuleta ujumbe wa amani toka kwa Talibani.

"Mmoja wao alisalimiana na Rabbani kwa kuweka kichwa chake kwenye mabega ya Rabbani na kulilipua bomu alilokuwa amelificha kwenye kilemba chake", alisema Aymaq.

Taarifa zaidi zilisema kuwa mjumbe huyo wa Talibani alikuwa akijulikana kama Mohammad Masoom na alikuwa akifahamiana vizuri sana na Rabbani akiaminika kuwa anatafuta suluhisho la amani.

Masoom aliluwa akienda mara kwa mara nyumbani kwa Rabbani na aliwahi kumkaribisha Rabbani nyumbani kwake na alimpa ulinzi wa kutosha hali iliyomjengea uaminifu wa kutosha kwa rais huyo wa zamani.

Masoom aliteuliwa na Talibani kuwa mwakilishi wa Talibani katika mazungumzo ya kutafuta suluhisho la amani kati ya Talibani na serikali ya Afghanistan.

Kuuliwa kwa Rabbani ni pigo kubwa sana kwa rais wa Afghanistan, Hamid Karzai ambaye aliamua kukatisha ziara yake nchini Marekani na kurudi Afghanistan.

Mamia ya watu waliandamana leo kwenye mitaa ya mjini Kage.bul kulaani kuuliwa kwa rais huyo mstaafu aliyekuwa akiheshimika kwa jitihada zake za kuleta amani kwenye nchi hiyo ambayo imeharibiwa kwa vita.

"Alitaka amani nchini Afghanistan na alijitolea maisha yake kupigania njia ya kuleta amani", alisema mmoja wa waandamanaji hao.

source nifahamis
[ Read More ]