Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Wanafunzi 70 Mbagala kutibiwa Muhimbili kutokana na mabomu

KARIBU wanafunzi 70 kati ya 1,000 waliobainika kuwa na matatizo mbalimbali yaliyotokana na milipuko ya mabomu iliyotokea Aprili 29 kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Mbagala Kuu, watatibiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwananchi imeelezwa.

Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa watu walioathirika na milipuko hiyo, karibu wanafunzi 900 walibainika kuwa na matatizo na kutibiwa na timu ya madaktari iliyopelekwa eneo hilo baada ya kuripotiwa kuwa watoto wengi walipata matatizo ya kutoona, kutosikia vizuri na maumivu ya kichwa.

Milipuko hiyo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 26 na kujeruhi watu kadhaa huku ikiharibu nyumba za wakazi wengi wa maeneo yanayozunguka kambi hiyo.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zinasema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliopewa rufaa hiyo ni wale waliobainika kuwa na matatizo ya kutosikia na kutoona vizuri.

“Wanafunzi sita wamepelekwa Muhimbili kutokana na kugundulika kuwa hawasikii vizuri kutoka na kuathirika na milipuko ya mabomu hayo na madaktari wamesema watoto wengine 20 hawataweza kuona vizuri hadi wapate matibabu zaidi na kupewa miwani,” alisema mwalimu mmoja wa Mbagala Kuu ambaye alikataa kutajwa gazetini.

Katika Shule ya Msingi Maendeleo habari zinasema kuwa wanafunzi 30 wamebainika kuwa na matatizo ya macho huku 14 wakiwa na matatizo ya kutosikia vizuri.

Kwa mujibu wa walimu hao, baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la masikio kuvuma wakati wote, kuwa na nta nzito na macho kuwasha walitibiwa shuleni hapo na kuendelea vizuri.

Baadhi ya walimu wa shule hizo waliliambia gazeti hili jana kwa nyakati tofauti kuwa tangu kutokea milipuko hiyo Aprili 29 mwaka huu, baadhi ya wanafunzi bado hawajafika shule.

Wamesema kuwa miongoni mwa wanafunzi hao ni pamoja na Majaliwa Petro (10) Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Maendeleo ambaye tangu kutokea milipuko hiyo hajafika shule.

Hata hivyo, dada wa Petro, Siwema Petro (13) anayesoma Maendeleo alisema mdogo wake ameathirika kisaikolojia na kuwa wakati wote anataka kukimbia na mara kadhaa anaongea mwenyewe.

“Wakati milipuko inatokea Majaliwa alikuwa shuleni, lakini tunasikia katika harakati za kujiokoa aliona mtu aliyekatwa shingo na bomu, sisi tunadhani ndicho kilichomuathiri zaidi,” alisema Siwema.

Milipuko hiyo pia imefanya miguu ya mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Mbagala Kuu, Quntinea Livingston, 7, kupooza na hivyo kusaidiwa kwa kubebwa.

Margareth Gilbert, 28, mama mzazi wa Livingston alisema mwanaye aliangukiwa na ukuta akiwa katika harakati za kukimbia baada ya kusikia milipuko ya mabomu.

Katika hatua nyingine, meya wa manispaa ya Temeke, Jerome Bwanausi amesema Mbagala sasa iko shwari na anasikitishwa na baadhi ya watu kutoa kauli za uongo na kuwatisha wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya hiyo, Bwanausi alisema taarifa zinazosambaa Mbagala kwamba mabomu yatalipuka wakati wowote ni za uongo.

“Msemaji mkuu wa suala zima la mabomu ni mkuu wa mkoa na mpaka sasa hajatoa taarifa yoyote ya ulipuaji mwingine wa mabomu kwa hiyo eneo hilo ni shwari,” alisema.

Naye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi jana alilazimika kuiongezea muda kamati inayofanya tathimini ya mali na majengo yaliyoteketezwa kwa mabomu hadi Juni 3 mwaka huu.

Lukuvi aliliambia gazeti hili jana kuwa amelazimika kuiongezea kamati hiyo muda baada ya mwenyekiti wake kuomba muda zaidi kwa ajili ya kukamilisha kazi.

“Nilitegemea kupokea taarifa ya kamati hiyo kesho (leo), lakini mwenyekiti wa kamati Cleophace Rweye alifika ofisini kwangu na kuomba muda zaidi wa kufanya kazi hiyo,” alisema Lukuvi.

“Moja ya mambo aliyodai hajayakamilishwa ni uandaaji wa taarifa na kufikisha taarifa yao kwa mtathimini mkuu wa serikali.”

Alisema ili waathirika hao waondokane na shida ya kuishi kwenye mahema hayo, serikali inahitaji kuwalipa fidia zao mapema, hivyo taarifa ya kamati hiyo ndiyo itakayokuwa mwongozo wa malipo.

Baadhi ya wakazi wa Mbagala Kuu jana waliendelea kuilalamikia kamati hiyo kuwa haikufanya tathimini kwenye nyumba zote zilizokumbwa na maafa hayo.

Wakizungumza na Mwananchi katika ofisi za kata hiyo wakazi hao walisema nyumba zao hazijafanyiwa tathimini tangu zoezi hilo lilipoanza.

Swaum Husein, 32, mkazi wa kitongoji cha Mwanamtoti alisema: “Sijafanyiwa tathimini yoyote katika nyumba yangu mpaka leo hii tunatangaziwa kuwa kazi hiyo imefikia ukomo wake.”

Lusian Matius mkazi wa mwanamtoti alisema: “Unavyotuona hapa tumelazimika kumchukuwa mjumbe wetu aje atueleze kwa nini mpaka leo hii nyumba zetu hazijafanyiwa tathimini.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mjumbe wa shina namba moja, Mohamed Likata, 48, alikiri kuwa wakazi hao hawajafanyiwa tathimini na kwamba lina nyumba 34 zinazohitaji.

[ Read More ]

CWT, HakiElimu wasaka chimbuko la kuvuja mitihani

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na asasi ya HakiElimu, wamezindua shindano la kufahamu chimbuko la kuvuja kwa mitihani ili kukusanya maoni yatakayosaidia kupata ufumbuzi wa tatizo hilo nchini. Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Idara ya Upatikanaji wa Habari wa HakiElimu, Robert Mihayo alisema lengo la shindano hilo ni kupata mawazo na maoni ya wananchi kujua sababu za kuvuja kwa mitihani nchini na kupata ufumbuzi na kuhimiza wananchi kuboresha elimu.

Alisema taifa linahitaji elimu iliyo bora ambayo siyo tu kufaulu mitihani, bali pamoja na kumjengea uwezo mwanafunzi wa kutumia elimu aliyoipata kutatua changamoto anazokumbana nazo katika maisha ya kila siku ambapo mfumo wa elimu nchini sasa umejikita zaidi katika kufaulu.

“Katika shindano hilo litakalowashirikisha Watanzania wote bila kujali umri wala uwezo wa kitaaluma yaani kuanzia wanafunzi hadi maprofesa, linawataka washiriki kutumia kurasa mbili au michoro kuelezea chanzo cha uvujaji wa mitihani, athari zake na nini kifanyike kutatua tatizo hilo,” alisema. Alisema mwisho wa shindano hilo ni Agosti 15, mwaka huu na washindi wawili wa kwanza watapata Sh 500,000 kila mmoja, washindi 10 wanaofuata watapata Sh 200,000 kila mmoja na washindi hao na wengine 50 watakaofuata watapatiwa redio moja kila mmoja zinazotumia umeme wa jua.

Alisema mawazo ya washiriki yatachambuliwa na kutengeneza kitabu kitakachosambazwa nchini ili maoni hayo yawafikie wananchi wengi na kupelekwa serikalini ili watendaji wayafanyie kazi kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Akizindua shindano hilo, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema ingawa serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwamo za kuwafukuza kazi wakuu wa shule zilizohusika, kuwafutia matokeo ya mitihani wanafunzi waliobainika kuiba, lakini uvujaji na wizi umeendelea kutokea mwaka hadi mwaka.


[ Read More ]

Barcelona mabingwa wa ulaya 2009, yaichapa Man United 2-0


MABAO ya Samuel Eto'o,dakika ya 10 ya kipindi cha kwanza na Lionel Messi, dakika ya 70 yameipa ubingwa wa tatu wa Ulaya Barcelona na kuivua ubingwa huo Manchester United.

Mpira wa kwanza wa Barca, uliomaliza utawala wa dakika 10 za kwanza za mchezo huo lilifungua mlango kwa mabingwa hao wa Hispania kuonyesha dhamira ya ushindi.

Eto'o, alibashiriwa mapema na mkongwe Rui Costa wa Ureno kuwa ndiye angeweza kuipatia timu yake bao la dakika za nyongeza na kuwaduwaza Man United.

Mshambuliaji huyo wa Cameroon aliweza kutimiza ubashiri huo, kwa kuipa Barca bao muhimu ambalo hatimaye lilireejeshea jeuri timu yake na kuanza kutawala sehemu kubwa ya mchezo kipindi cha kwanza.

Mchezo ulianza kwa timu hizo kuonyesha makali, ingawa ilikuwa Man United ambayo ilikuwa na uchu kwa kulishambulia lango la Barca na kupata mikwaju kadhaa ya adhabu ndogo ambayo 'mtaalam' wake, Cristiano Ronaldo alishindwa kuitumia.

Katika mchezo huo, mwamuzi Massimo Busacca, ambaye kabla ya mchezo alikwenda Vatican, makao ya Kanisa Katoliki, kuomba baraka kwa Papa Benedict XVI akimwonyesha kadi ya njano Gerrard Pique kwa kumchezea vibaya Ronaldo.

Nao Ronaldo na Paul Scholes walionyeshwa kadi za njano kwa mchezo mbaya dhidi ya wapinzani wao.

Mabadiliko ya kipindi cha pili ya kocha Alex Ferguson kuwatoa Ji- Sung Park na Anderson na kuwaingiza Carlos Tevez na Scholes hayakusaidia.

Vikosi:

Barcelona - Victor Valdes, Carles Puyol, Gerrard Pique, YayaToure, Sylvinho, Xavi Hernandez , Sergio Busquets, Andres Iniesta, Lionel Messi, Samuel Eto'o, Thierry Henry.

Manchester United: Edwin Van der Sar, John O'Shea, Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Patrice Evra; Anderson, Michael Carrick, Ryan Giggs, Ji- Sung Park, Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney.

[ Read More ]

Kikwete ashutumiwa vikali kwa kuendekeza ziara za nchi za nje




WAKATI Rais Jakaya Kikwete akirejea nchini kutoka Marekani kwa ziara ya siku takriban nane, jarida maarufu la uchambuzi wa kiuchumi, The Economist limehoji safari za mkuu huyo wa nchi, likisema kuwa anatumia muda mwingi katika kutangaza jina la nchi nje badala ya kutatua matatizo ya ndani.

Kikwete, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kabla ya kuingia Ikulu, ameshakwenda Marekani zaidi ya mara sita tangu ashike serikali ya awamu ya nne, ikiwa ni baadhi ya safari zake nje ya nchi alizofanya katika kipindi cha miaka mitatu na nusu hadi sasa.

Safari hizo zimewafanya watu mbalimbali, wakiwemo wanasiasa na wachumi kuhoji sababu za safari hizo, ambazo wakati fulani aliwahi kuzitetea kuwa zina tija katika kuitangaza nchi na kuvutia wawekezaji.

Katika habari ya uchambuzi wa toleo la Mei 7, gazeti la The Economist limeeleza jinsi Tanzania inavyohaha kusaka misaada nje ili kukabiliana na kuyumba kwa uchumi duniani wakati bajeti yake inafadhiliwa kwa asilimia 40.

"Ni kiasi gani kinatosha," inahoji habari hiyo ya uchambuzi yenye kichwa cha habari kisemacho, "Tanzania: Waiting for That Great Leap Forward (Tanzania: Ikisubiri Kupiga Hatua Kubwa Mbele)."

Habari hiyo inasema: "Nchi tayari inapata asilimia 40 ya bajeti yake ya serikali kutokana na misaada, lakini inataka fedha zaidi ili iweze kukabiliana na kuporomoka kwa uchumi. Ni kiasi gani kinatosha?"

Baadaye gazeti hilo linaloheshimika kwa uchambuzi wa mambo ya kiuchumi duniani, linamkariri Rais Kikwete akizungumza katika moja ya hotuba zake kwa kusema: "Tunajaribu kupunguza utegemezi wetu, lakini tunashukuru kwa kila tunachokipata."

Bajeti ya mwaka huu ya serikali ilikuwa Sh7.22 trilioni huku asilimia 33.6 ikiwa ni fedha kutoka kwa wahisani na mwaka ujao wa fedha bajeti ya serikali inatazamiwa kuwa Sh8.14 trilioni, huku kiasi cha fedha kutoka kwa wahisani kikitegemewa kupanda kutoka asilimia 33.6 hadi asilimia 34.3.

Mwaka jana, wahisani hawakutoa karibu dola 2.4 bilioni za Marekani walizoahidi na hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika mwaka mpya wa fedha kutokana na nchi wahisani kulazimika kutoa fedha kuokoa taasisi zao za kifedha zilizoathiriwa na mtikisiko wa kifedha duniani ulioyumbisha uchumi wa dunia.

Katika uchambuzi wake, linasema Tanzania, ikiwa na idadi ya watu milioni 44, ina utulivu kulinganisha na nchi jirani ya Kenya, yenye watu milioni 40.

"Inachokosa kiuwezo ndicho kinasaidia kuwa na utulivu na utambulisho wa utaifa. (Nchi) haiwezi kusambaratika wakati wa uchaguzi au wakati wowote ule," linaandika gazeti hilo.

Linasema chama kilichopigania uhuru, CCM, ambacho zamani kilijulikana kama Tanu, bado kinahangaishwa na vyama hohehahe vya upinzani.

"Bwana Kikwete ni mtu wa CCM; kazi aliyoibukia ni ya kiongozi wa vijana aliyehusika na kutangaza siasa kwenye jeshi. Ni wazi kuwa atarejea madarakani kwa ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu ujao. Bado anashawishi wawekezaji kwa kutumia kipaji chake kama mtu wa (idara ya) masoko," linaandika The Economist.

"Lakini bado wale walioanzisha maduka nchini kila mara wanakerwa. Wengi wanalalamika kuwa Tanzania ni goigoi au hata kueleza kuwa ni sehemu mbaya kufanya biashara na haina shukrani kwa misaada (inayopata) au uwekezaji.

"Hata wanaoitetea wanakiri kuwa imegubikwa na urasimu na haina wafanyakazi walio na stadi. Karibu kila mtu anasema Kikwete anatumia muda mwingi mno kutangaza nchi nje na si kutatua matatizo ya nyumbani kwa kiasi cha kutosha. Mwaka jana alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika."

Hata hivyo, gazeti hilo la Marekani linasifu kipaji cha Kikwete katika kushawishi; na imani kubwa aliyonayo kwa maendeleo, likisema kuwa ana imani kuwa misaada itaifanya Tanzania iendelee kuwa juu kiuchumi kwa muda mrefu na hatimaye kupiga hatua kubwa kwenda mbele.

"Maghorofa mapya yanayong'aa, yaliyo hata kwenye miji midogo, sambamba na barabara na miradi mipya ya maji inadhihirisha imani hiyo (ya Kikwete). Hali ya siasa ni imara. Wapinga Muungano kwenye visiwa vya Zanzibar wametulia kwa sasa," linaeleza gazeti hilo.

Gazeti hilo pia linaeleza hali ya uharaka iliyopo sasa kwenye serikali ya Rais Kikwete, likitoa mfano wa waziri anayehusika na nishati kuwa anataka kituo kipya cha umeme katika muda mfupi ili kukabiliana na kuanguka kwa huduma ya nishati hiyo, huku JK akiita viongozi wa mashirika yanayomilikiwa na serikali kama Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya Reli akitaka ufanisi.

Bila kufafanua zaidi, pia limeandika kuwa, Rais Kikwete anawashughulikia watu wanaoitwa "Wabenzi", likidai kuwa ni wale wanaoendesha magari ya kifahari kama ya Mercedes Benz.

Lakini linadai kuwa, Tanzania kwa kiasi fulani, imeshindwa kwenda na wakati au haikupata mafanikio.

"Ziara ya rais wa China ya hivi karibuni imeshindwa kutoa uwekezaji mwingi," linaeleza gazeti hilo. "Serikali ya China inadhani Kenya, na si Tanzania, ndio njia ya kupitia kwenda kwenye utajiri wa madini wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

"Reli mbili za Tanzania (reli ya kati na Tazara) ni mikweche. Bandari ya Dar es Salaam ilishindwa kupoka biashara kutoka Bandari ya Mombasa wakati Kenya ikiwa kwenye vurugu mwaka mmoja uliopita.

"Hakuna mtu anayeonekana kujua ni lini bandari hiyo kubwa itafikia malengo yake ya kupunguza mrundikano wa mizigo bandarini ifikapo mwaka 2030."


[ Read More ]

Huu ndio mguu bandia


Mtaalamu wa tibamaungo wa Kituo cha Tiba cha Kijeshi cha Walter Reedy jijini Washington, DC, Marekani, Annette Bergenon, akimwonyesha Rais Jakaya Kikwete jinsi mguu bandia unavyofanya kazi, wakati Rais alipotembelea kituo hicho hivi karibuni.Wanaoshuhudia kushoto, ni Dk. Mohamed Janabi wa Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbili (MUCHS) na Waziri wa Kazi, Vijana,Wanawake na Watoto wa Zanzibar, Asha Juma, ambao walikuwa katika msafara wa Rais Marekani.
[ Read More ]

JK kuongoza mkutano wa kujadili kilimo

Rais Jakaya Kikwete wiki ijayo ataongoza mkutano wa kujadili kilimo kuwa nguzo kuu ya uchumi wa Tanzania. Mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), pia utahudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri, wakuu wa mikoa, wajumbe wa baraza hilo, wawekezaji wa ndani, wadau wa maendeleo, wasambazaji wa mazao na wasindikaji. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dunstan Mrutu alisema mkutano huo utajulikana kwa jina la 'Kilimo Kwanza ' ukiwa na nia ya kufanya tathmini kwa nini sekta ya kilimo imeshindwa kukua na kupunguza umasikini.

Mrutu alisema mkutano huo utafanyika Juni 2 hadi 3 mwaka huu Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo. Alisema lengo la ‘Kilimo Kwanza’ ni kuwezesha Mapinduzi ya Kijani kwa kuwa na kilimo cha teknolojia ya kisasa hasa katika kilimo na ufugaji, kutumia mbegu bora na za kisasa, uzalishaji kwa chupa, dawa za kilimo, mbolea na kukuza kilimo cha umwagiliaji. “Mkutano huu utakaowashirikisha wakuu wa nchi na mikoa, utasaidia kuangalia matatizo mbalimbali yanayosababisha kilimo kushindwa kukua na jinsi ya kufanya ili kukuza sekta hiyo,” alisema Mrutu.

Alisema mkutano huo utasaidia kubadilisha kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na kibiashara kwa kuwashirikisha wakulima wadogo na wakulima wakubwa kuachana na jembe la mkono na kutumia zana za kisasa na kuacha kuuza mazao yasiyosindikwa. Alisema baada ya mkutano huo, uamuzi utakaofikiwa utasimamiwa na wakuu wa mikoa washiriki wa mkutano huo ili kuhakikisha kilimo kinakua na kuinua uchumi na kuacha kutegemea vitu kutoka nje.
[ Read More ]

Wabunge waondolewa ulaji

Wabunge wameanza kunyang’anywa sehemu ya ulaji kutokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa waraka unaowaelekeza wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye bodi za mashirika na taasisi za fedha kuondolewa mara moja. Hatua hiyo inatokana na ushauri uliotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushauri wabunge wasiwe wajumbe wa mashirika yoyote ya umma, ili kuondoa mgongano wa maslahi. Kaimu Msajili wa Hazina, Godfrey Sella, alisema jana kuwa utekelezaji wa waraka huo wa BoT unaanza mara moja. Alisema kuna baadhi ya wabunge wenye maslahi katika taasisi za kifedha; hivyo si vizuri viongozi hao kuwa sehemu ya bodi za wakurugenzi.

Tayari BoT imetoa orodha ya wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye taasisi za fedha na imepeleka waraka huo kwa Msajili wa Hazina ili aondoe majina ya wabunge hao kwenye bodi hizo. “Lengo hapa ni kutenganisha usimamizi na utekelezaji…tumepata waraka huo wa BoT na kinachofuata ni utekelezaji,” alisema Sella wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), aliyehoji sababu ya wabunge wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa mashirika ya umma wakati kuna baadhi yao wana uwezo.

Mbunge huyo alisema kama kuna chama cha siasa kimeshinikiza suala hilo ni vyema kikapuuzwa; kwa kile alichodai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wabunge, kwani nao ni sehemu ya jamii. “Kuna wabunge wana uwezo mkubwa wa kuisaidia Serikali kupitia mashirika haya, iweje waondolewe kwenye nafasi zao za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma?” alihoji mbunge huyo. Baada ya swali hilo, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, alifafanua kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kimekuwa kinashinikiza suala hilo; ila ni ushauri uliotolewa na ofisi ya CAG.

Ndipo Kaimu Msajili wa Hazina akafafanua, kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na akaeleza kuwa zina nia nzuri ya kuwafanya wabunge wawe wasimamizi wazuri wa mashirika hayo. Wakati huo huo, Msajili huyo wa Hazina alikiri kuwa kampuni za Meremeta na Buhemba hazijawasilisha hesabu zozote katika ofisi yake kwa kile alichodai kuwa wizara ndiyo yenye jukumu la kuomba hesabu hizo. Alisema Meremeta ambayo iko chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, haina hesabu zozote lakini pia BoT ambayo inahusika na kampuni hiyo nayo haina hesabu zake.

“Hii inahesabika kama ni kitegauchumi cha serikali, lakini kwa mtazamo wangu, si shirika la kitega uchumi kwani hata CAG ameshindwa kuifanyia ukaguzi, kwa vile haina mali inayoonekana kwa macho,” alisema Sella. Kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Msajili huyo alilalamika kuwa ofisi yake imejikuta wakati mwingine ikifanya kazi za ndani za mashirika ya umma kutokana na mfumo wa kiutendaji uliopo. Alisema kwa sasa wanajitahidi kuandaa waraka utakaosaidia kufanya mabadiliko ili ofisi ya Msajili wa Hazina ibaki kuwa msimamizi wa mashirika ya umma bila kuingilia utendaji wa mashirika hayo.

“Tunataka sisi tubaki kusimamia na kuona kama uamuzi unaofanywa na mashirika haya unazingatia maslahi ya taifa,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa wizara nyingi ambazo zinatakiwa zipeleke mapendekezo ya wajumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali kabla ya kutangazwa, hazifanyi hivyo. Alisema licha ya sheria kuzitaka kufanya hivyo kwa makusudi, mawaziri wanakaidi. “Ukihoji utaulizwa Msajili ni nani na ukisema ufuate sheria lazima utagongana na wakubwa zako, ndiyo maana tunaamua kukaa kimya.”



[ Read More ]

UN yalaani hatua ya Korea Kaskazini


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kukutana kwa dharura, hatimaye limeshutumu vikali hatua ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kinyuklia.

Baraza hilo lilikutana kwa dharura saa chache tu baada ya jaribio hilo kufanywa na limeonya hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Korea Kaskazini.

Kauli ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imetolewa muda mfupi tu baada ya serikali ya Korea Kaskazini kutangaza imefanya jaribio lililofanikiwa la Kombora la nyuklia lililo kubwa zaidi ya lile iliyolipua mnamo mwaka wa 2006.

Mataifa wanachama sasa wanataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Korea Kaskazini ambayo tayari iko chini ya vikwazo vya baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa. Lakini serikali ya Korea Kaskazini imepuuza kauli hiyo na kusema iko tayari kukabiliana vilivyo na wapinzani wake wote.

Wataalamu wa makombora wa Urusi wanasema kombora lililolipuliwa lina uwezo sawa na yale yaliyoangushwa na Marekani katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan wakati wa vita vya pili vya dunia.

Hata China ambayo imekuwa ikiunga mkono Korea Kaskazini chinichini sasa imesema itakubaliana na azimio lolote la Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa.

Ili kuelewa wasiwasi huu ambao umekumba jamii ya kimataifa ni muhimu kuelewa uwezo wa zana za Kinyuklia.

Kulingana na shirika moja la utaalamu wa kivita la Marekani, Center for Defense Information, makombora matano au sita ya aina iliyofanyiwa majaribio siku ya Jumatatu, yakilipuliwa mara moja yana uwezo wa kuharibifu duniani kote na kuwaacha manusura wachache sana.

Ikiwa na silaha kama hizi, si ajabu Korea kaskazini sasa imeionya Marekani itakabiliana nayo kivita iwapo serikali ya Rais Obama itajaribu kuishambulia

[ Read More ]

Uchumi wa Afrika kusini umekumbwa na mdororo


Uchumi wa Afrika kusini umekumbwa na mdororo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1992, kufuatia kupungua kwa kasi ya uzalishaji viwandani halikadhalika sekta ya madini.

Uchumi wa nchi yenye Uchumi bora barani Africa imerekodi upungufu wa kiwango cha hadi asili mia 6.4% kati ya mwezi Januari na March, ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana.

Hiki ndio kiwango kikubwa cha upungufu tangu mwaka 1984 kikifuatiwa na mdororo wa asili mia 1.8% kila mwaka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Sekta ya ujenzi hata hivyo imeimarika kutokana na mashindano ya mpira ya Kombe la Dunia yanayopangwa kufanyika huko.

Afrika kusini imenufaika chini ya mpango kabambe wa serikali wa uwekezaji katika mipango ya mashindano ya mpira ya mwaka 2010.

Takwimu zilizofanywa na kampuni huru 'Statistics South Africa, imebaini kupungua kwa uzalishaji viwandani pamoja na uwindaji wanyama pori vimechangia mno mdororo huo.

Makampuni ya kuchimba migodi yameathiriwa na mdororo wa uchumi duniani.

[ Read More ]

Wahasibu watakiwa kuwania CPA

Wahitimu wa Uhasibu na Fedha wa Chuo Kikuu Mzumbe (MU), wameshauriwa kujiendeleza kwa kufanya mitihani ya juu ya Uhasibu (CPA) na baadaye kusajiliwa katika Bodi ya Uhasibu (NBAA) ili watambulike wanataaluma.

Changamoto hiyo ilitolewa na Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Kanda ya Mashariki na Kati, Meshack Bandawe, wakati wa hafla maalumu ya wanafunzi wanaotarajia kumaliza masomo yao ya Stashahada na Shahada.

Alisema taaluma ya uhasibu ni moja ya taaluma zinazohitaji kuwa na uaminifu na uadilifu wa kiwango cha juu kutokana na mazingira ya kazi yaliyojaa vishawishi vingi zaidi ukilinganisha na kazi nyinginezo.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa PPF Kanda ya Mashariki na Kati, wapo watu wenye taaluma ya uhasibu ambao wamekuwa wakiharibu sifa ya taaluma hiyo na kusababisha wananchi kupoteza imani.

Hivyo alisema ni wajibu wa wanafunzi wa chuo kikuu hicho kuheshimu sheria za kazi kwa kuwa waadilifu ili kuepukana na sifa mbaya katika utendaji wao kwa siku za usoni pindi watakapopata ajira.

Alisema watakapoingia kwenye ajira iwe ya sekta binafsi ama ya umma, wana wajibu wa kusimamia na kuhakikisha michango ya wanachama wa mifuko ya jamii ukiwamo wa PPF inawasilishwa kwa wakati ili kuepukana usumbufu baada ya watumishi kustaafu kazi ama kuondoka kwa sababu yoyote.
[ Read More ]