Tanzania iko tayari kuwachukua watu watakaopatikana na hatia ya makosa ya jinai kutumikia vifungo vyao nchini. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana alipokutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jaji Sang-Hyun Song. “Tunaweza kuchukua watakaopatikana na makosa kutumikia vifungo hapa Tanzania, tuko tayari kwa hilo,” Rais alimweleza Jaji Sang-Hyun Song. Mahakama ya Kimataifa ingependa watuhumiwa wa mahakama hiyo kutumikia vifungo vyao katika nchi zilizo karibu na wanakotoka ili waishi katika mazingira yaliyo sawa ama kufanana na nchi wanazotoka. Jaji Sang-Hyun Song alifika nchini kujitambulisha na kuishukuru Tanzania kwa kuiunga mkono mahakama hiyo na shughuli zake katika juhudi za kutafuta haki na kulinda haki za binadamu duniani. Jaji Song ameshika wadhifa huo kwa muda wa miezi miwili na nusu sasa. “Nimekuja Tanzania kujitambulisha kwako na uongozi wako na pia kukushukuru kwa kuiunga mkono Mahakama ya Kimataifa,” Jaji Song alimweleza Rais Kikwete. Katika kikao hicho, Rais Kikwete pia alimwambia Jaji Song kuwa ICC inaweza kutumia majengo ya Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda (ICTR) iliyoko Arusha. Rais Kikwete alisema ICTR ina uwezo wa kukidhi mahitaji yote ya ICC kwa kuwa ina vyumba vya mahakama vinne, ofisi na vyumba vyote muhimu kwa mahitaji ya mahakama ikiwamo jela ya kimataifa ambayo inawashikilia watuhumiwa wa mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. ICTR inatarajiwa kukamilisha kazi zake mwakani. “ICTR ina majengo na vifaa vya kimataifa, Afrika inataka pia kuwa na utambulisho wake katika hili, mnaweza kuendesha baadhi ya kesi mjini Arusha na pia itakapofika kipindi kuwa mnataka kuwa na ofisi za kanda katika Afrika, mnaweza kutumia majengo haya mara Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda itakapokamilisha kazi zake,” alieleza Rais. Jaji Song alimshukuru Rais Kikwete kwa wazo hilo alilosema ameshukuru kulipata na atalitilia maanani kwani ICC ina nia na lengo la kushirikiana vilivyo na Afrika na kwamba pamoja na kuwa na watuhumiwa wengi kutoka Afrika, pia wafanyakazi wengi wa mahakama hiyo wanatoka Afrika na wametoa mchango mkubwa katika kazi hiyo |