Kwa mujibu wa maafisa waandamizi nchini humo, shambulio hilo lilitokea katika mji wa Peshawar kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari nchini humo, zimeeleza watu waliokuwa wamejihami waliwashambulia walinzi karibu na hoteli ya kifahari ya Pearl Continental kabla ya kulipua gari liliokuwa limebeba shehena ya mabomu eneo la kuegeshea magari.
Walioshuhudia tukio hilo waliiambia BBC, mlipuko huo ulionekana hadi umbali wa kilomita tano. Sehemu moja ya hoteli hiyo imeporomoka kabisa.
Mwandishi wa BBC nchini Pakistan amesema hoteli hiyo ndiyo maarufu zaidi katika mji wa Peshawar na ni mojawapo ya majengo yanayotambuliwa zaidi ya mji huo.
Miji kadhaa nchini Pakistan ukiwemo ule wa Peshawar imekumbwa na mashambulio ya mabomu tangu jeshi la nchi hiyo lilipoanza harakati za kupambana na wanamgambo wa Taliban.
Hata hivyo hakuna aliyekiri kuhusika na mashambulio hayo.