Ahmed Ghailani amepelekwa kukabiliana na mashtaka katika mahakama ya New York akihusishwa na uripuaji wa mabomu wa balozi za Marekani katika Afrika Mashariki.
Bwana Ghailani, Mtanzania, alikamatwa nchini Pakistan mwaka 2004. Anatazamiwa kufikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya Manhattan baadae siku ya Jumanne.
Alipelekwa Guantanamo akiwa pamoja na mahabusu wengine wanaoitwa "muhimu sana" mwishoni mwa mwaka 2006.
Kuhamishwa kwake kumekuja huku Rais Obama akiwa katika hekaheka za kutafuta utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa uchaguzi ya kufunga gereza la Guantanamo Bay katika kipindi cha mwaka mmoja akiwa madarakani.
Waandishi wa habari wanasema kesi ya Bwana Ghailani litakuwa jaribio muhimu katika mipango ya utawala wa Obama kufunga gereza hilo na hatimaye kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa.
Serikali ya Marekani ina matumaini ya kuwasafirisha baadhi ya watuhumiwa wengine katika baadhi ya nchi, lakini hadi sasa mashauriano juu ya hilo yamekwama hasa iwapo Marekani nayo ipo tayari kupokea mahabusu.
Baraza la Congress lilikataa maombi ya serikali ya kugharamia kufungwa gereza la Gauantanamo, kukiwa na upinzani mkali wa kuwapeleka watuhumiwa Marekani.