Rais Omar Al- Bashir alishtakiwa kwa madai ya ukatili dhidi ya raia katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan mwezi wa tatu.
Lakini wajumbe katika mkutano wa AU uliofanyika nchini Libya walikubaliana kuhusu azimio linalosema hawatatoa ushirikiano katika kukamatwa kwa Rais Bashir.
Wadadisi wanasema hatua hiyo ina maana kwamba rais Bashir anaweza kusafiri popote barani Afrika ya hofu ya kukamatwa.
Serikali ya Sudan imekuwa ikipigana na waasi katika jimbo la Darfur tangu mwaka 2003.
Mahakama ya ICC inamshtaki Rais Bashir kwa makosa mawili ya uhalifu wa kivita ; kuagiza kushambuliwa kwa raia na uporaji , pamoja na mashtaka mengine matano ya uhalifu dhidi ya binadamu , mkiwemo mauaji , ubakaji na utesaji , yote hayo yakihusishwa na mzozo huo.
Ameyakanusha mashtaka hayo yote , akisema serikali inao wajibu wa kupambana na makundi ya waasi.
Kwenye taarifa , AU imeeleza kwamba ombi lake la kuitaka mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague isimamishe kwa muda hoja hiyo ya kukamatwa kwa Rais Bashir limepuuzwa.
Taarifa jiyo inasema : '' Umoja wa Afrika hautatoa ushirikiano kuhusiana na hoja ya kukamatwa au kujisalimisha kwa Rais wa Sudan Omar Al- Bashir kwa mahakama ya ICC.''
Mwandishi wa BBC anasema ingawa taarifa hiyo imeungwa mkono na viongozi wengi wa Afrika , bado kuna nchi kadhaa , zikiwemo Chad na Benin ambazo zinaonekana kutoridhishwa na kauli hiyo.
Pia kumekuwa na maswali kuhusu taarifa hiyo, kwa sababu haijazitaka nchi 30 zilizotia sahihi ya kuundwa kwa mahakama ya ICC kusitisha uhusiano na mahakama hiyo.
Uamuzi huo ulifanyika katika siku ambapo Kenya imekubali kuendelea kushirikiana na mahakama hiyo ya ICC , kuwashtaki wale wanaotuhumiwa kwa kuchochea ghasia zilizofuatia uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka 2007.