WAZIRI wa Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa vituo vya mafunzo ya amali nchini unalenga kuwasaidia na kuwajengea uwezo vijana.
Alisema vyuo hivyo ni msingi wa kuwawezesha vijana ili waweze kujiari na kuajiriwa jambo ambalo litawasaidia kuepukana na ugumu wa maisha.
Alisema hayo jana, wenye ufunguzi kituo cha Elimu ya Amali huko Chukwani, Wilaya ya Magharibi Unguja, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya Mapinduzi Zanzibar yanayotimiza miaka 47.
Alisema kujenga kwa kituo hicho ni chachu ya maendeleo na kupunguza umasikini kwa wananchi, ambapo inakwenda sambamba na sera za Serikali ya kuwawezesha vijana kupia vituo hivyo kwa ajili ya kujiajiri wenyewe na kuajiriwa.
Alieleza kituo chiho kitatoa mafunzo ya kompyuta, lugha ya kiingereza na ufundi wa magari kwa kuanzia, ambapo alitoa wito kutangazwa zaidi ili vijana waweze kujiunga na kufaidika na matunda hayo.
Waziri Samia alizishukuru taasisi zilizotoa msaada wa ujenzi wa kituo hicho ikiwemo Ujerumani ambayo ilishirikiana na ‘Pamoja Zanzibar’, ambapo jumla ya Euro milioni 4.7 zilitumika katika kituo hicho ikiwemo vifaa vya kisasa vilivyofungwa.
Hata hivyo, aliwakumbusha wananchi wanakila sababu ya kusherekea Mapinduzi Matukufu 1964, ambayo ndio yaliyowakomboa wananchi na matunda yake yanaonekana.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Shaaban aliwapongeza wahisani hao kupitia Jumuiya ya Pamoja Zanzibar na mashirikiano makubwa baina ya Chuo cha Ufundi na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia katika kufanikisha ujenzi huo, ambao unatokana na sera ya elimu ya kuwajengea uwezo vijana.
Nae Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dk. Guido Herz aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kukubali kujengwa kwa kituo hicho ambacho kitasukuma mbele maendeleo ya kiuchumi na kupambana na umasikini
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa taasisi ya Sayansi na Teknolojia, ambao ndio walezi wa kituo hicho, Haji Abdulhamid alieleza Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alianzisha Chuo cha Ufundi Mbweni kwa ajili ya kukuza maendeleo kupitia sayansi na teknolojia.
Alisema uwepo wa chuo hicho ni kuziendeleza fikra za kiongozi huyo aliyeasisi Mapinduzi ya Zanzibar miaka 47 iliyopita.
JUMLA ya wafanyakazi wanne walioajiriwa kwa mkataba usio rasmi katika skuli ya HIGH VIEW, wameachishwa kazi na kukoseshwa haki zao zote ikiwemo mishahara ya miezi miwili.
Wakizungumza na Zanzibar Leo wafanyakazi hao walisema uongozi wa skuli hiyo umechukua hatua ya kuwafukuza kazi kwa vile walikuwa wanadai haki zao kisheria.
Aidha walifahamisha kuwa mnamo Disemba 2 mwezi uliopita, waliandikia barua kwa uongozi wa skuli hiyo na kudai kupatiwa mishahara, posho la likizo na kupatiwa mikataba rasmi pamoja na kupatiwa vitambulisho vya ZSSF.
Walimu hao walisema wameajiriwa katika skuli hiyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili na tokea kipindi hicho wamekuwa wakikatwa fedha zao mfuko wa hifadhi ya jamii, lakini wanashangazawa kuona hadi kufikia hii leo hawajapatiwa vitambulisho vyao.
“Tumekwenda hadi ZSSF kudai mafao yetu tumeambiwa kuwa hakuna fedha zilizowasilishwa na skuli hiyo hivyo hawawezi kupata haki yoyote”, alisema mmoja wa walimu hao.
Hata hivyo waliongeza kwa kusema kuwa skuli hiyo imekuwa ikiwajiri walimu kwa mikataba isiyo rasmi kwani haipitii katika kamisheni ya kazi na inaishia kwa wakuu wenyewe.
Aidha walieleza kua uongozi wa skuli hiyo umekuwa ukiwanyanyasa wafanyakazi wake na kutowapa fursa ya kujitetea.
Hata hivyo juhudi za kumpata miliki wa Skuli hiyo ili kuweza kujibu madai hayo zimeshindikana kutoka na kuwepo kwa nje ya ofisi na walimu waliyokuwepo Skulini hapo walishindwa kujibu madai hayo