Naamini yupo alivyo kwa sababu ya malezi aliyopata kwenye familia yake yaliyomsaidia msichana, Agnes Dominic (20), kufanya vizuri kwenye Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka huu na kuwa mwanafunzi wa tano kitaifa. Licha ya msingi alioupata kutoka katika malezi ya wazazi wake, pia naamini kuwa juhudi binafsi na dhamira aliyoiweka ya kutorudia makosa aliyoyafanya kidato cha nne, vimechangia sehemu kubwa ya mafanikio hayo ya kitaifa.
Niliwasiliana naye kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) Alhamisi iliyopita jioni na Ijumaa iliyopita asubuhi, alinipa majibu yake yaliyonipa mwanga wa awali kuhusu Agnes. Katika mawasiliano hayo ya awali kwa njia ya sms, nilitaka anieleze atakayekuja kunipokea kituoni wakati tulipokubaliana nifike kwao Mtoni kwa Dosa, wilayani Temeke, Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano naye ili wasomaji wa Jarida la Nyota la HabariLeo Jumapili wamfahamu na kujifunza kitu kutoka kwake. Alinieleza atakuja yeye na ningemtambua kwa kuwa yeye si mtu wa kujiremba awapo nyumbani.
Alipokuja kunipokea jirani na barabara ya Kilwa, nilikumbuka sms aliyonitumia, ‘hakupiga pamba’ za kupigia picha kama nilivyomtania kwenye ujumbe niliomtumia, alikuwa na nywele za rasta, alivaa sketi ndefu nyeupe, fulana nyeusi na kandambili. Saa mbili za kuzungumza na Agnes, zilinipa jibu ni kwa nini amekuwa mwanafunzi wa tano kati ya wasichana 10 bora waliofaulu mtihani huo na mwanafunzi namba moja kati ya 47 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibosho mkoani Kilimanjaro.
Amekuwa namba moja katika shule hiyo iliyoongoza kitaifa mwaka huu ya mkoani Kilimanjaro ikifuatiwa na Shule ya wasichana ya Marian iliyokuwa ya pili na kufuatiwa na Kibaha zilizopo mkoani Pwani, Mzumbe ya Morogoro ilishika nafasi ya nne na Ilboru ya Arusha katika nafasi ya tano. Anajiheshimu, ni mchangamfu, mstaarabu na katika dhamira yake hiyo ya kufaulu, aliweka mikakati, alisoma kwa malengo na kumtanguliza Mungu. “Sikuiba, sikuibia mtihani, nilimtegemea sana Mungu na nilisoma kwa bidii… sio kwamba kufaulu ni juhudi zangu mimi, kuna watu wengi waliojitolea na walikuwa na dhamira ya kufaulu na walimu waliwategemea,” anasema msichana huyo aliyehitimu katika shule hiyo inayoongozwa na watawa wa Kanisa Katoliki.
“Haikuwa rahisi na wala siwezi kumkufuru Mungu kwamba ilikuwa migumu sana, ilikuwa kama mitihani mingine,” anasema msichana huyo aliyezaliwa Dar es Salaam Machi 30, 1989. Alisoma mchepuo wa Historia, Kiswahili na Fasihi (HKL), alisoma pia dini na kwa mtazamo wake, mitihani ya Kiswahili na Dini (Divinity) ilikuwa migumu zaidi ya Historia na Fasihi. Alitumia vizuri muda aliopewa kujiandaa na Mtihani wa Taifa na tangu walivyokwenda shule Januari 3 mwaka huu, hakuna mwalimu aliyeingia darasani kuwafundisha, walikuwa wakijisomea baada ya kumaliza ‘topics’ za darasani. “Kuna watu wanakesha, it happens (huwa inatokea), analala saa saba usiku, anaamka saa 10 usiku,” anasema na kubainisha kwamba yeye hajawahi ‘kukesha’.
Anasema alikuwa anasoma kuanzia saa moja usiku hadi saa nne na baada ya hapo aliacha kusoma na kuandaa sare kwa ajili ya kesho yake. Baada ya maandalizi ya siku inayofuata, alijikumbusha masomo yake kwa mara nyingine hadi saa sita ambapo alilala hadi asubuhi. “Ni kuijua tu akili yako, kama wewe ukisoma mchana unaelewa vizuri zaidi kuliko usiku, inabidi usome sana mchana na usiku unalala, kama unaelewa sana usiku, pumzika mchana kisha soma usiku. “Usisome kwa sababu fulani anasoma, soma kwa sababu unataka kuelewa, cha msingi ni kuitambua akili yako,” anasema.
Tangu ameanza kusoma darasa la kwanza, hajawahi kuwa namba moja darasani na hakutarajia kufaulu kwa kiwango alichofikia kitaifa. Anasema hakudhamiria kuwa miongoni mwa wanafunzi bora kitaifa kwani lengo lake lilikuwa ni kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kwa pointi zozote. Amepata daraja la kwanza pointi tatu. Ana alama ya ufaulu ya A katika Kiswahili, A katika Fasihi, A katika somo la Dini, na B katika Historia. Ni miongoni mwa wanafunzi 35 waliopata daraja la kwanza Shule ya Kibosho, saba wamepata daraja la pili, na watano wamepata daraja la tatu.
Ana malengo katika maisha yake na anatambua kuwa mchango wa wazazi wake ikiwamo nia na dhamira ya kumwezesha asome kidato cha tano na sita, vimemsaidia kupata sifa si tu kwa ndugu, jamaa, na marafiki bali Tanzania nzima. “Kingine ambacho kimenisaidia sana ni kupitia ‘past papers’ (mitihani iliyopita) na kusoma maswali kwa uangalifu… mimi nilikuwa nimezoea kufanya mitihani, nimefanya ‘a lot of papers’ (mitihani mingi),” anasema. Aliweka dhamira ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita kwa kuwa alikuwa na mtazamo kwamba kufeli mtihani huo ni kupoteza mwelekeo wa maisha na fursa ya kuishi maisha mazuri.
“Kuna percentage (asilimia) kubwa sana ya kufaulu kama wewe mwenyewe utaijua akili yako ipo vipi,” anasema msichana huyo aliyewahi kusoma masomo ya ziada mara moja tu kwa wiki mbili. Ni mtoto wa kwanza kwa Dominic Benard na Joyce Dominic. Ana wadogo zake wawili, Happy ambaye anasoma Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph Ngarenaro iliyopo Arusha na Justine anayesoma katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Anthony, Mbagala, Dar es Salaam.
“Sijui kama watakaonifuata wataiga mfano wangu, unajua kila mtu na future (maisha yake ya baadaye) yake,” anasema msichana huyo aliyependa kusoma masomo ya biashara kidato cha kwanza hadi cha nne na hakupenda masomo ya sayansi. Anawashukuru wazazi wake kwa kumpa nafasi ya kusoma kidato cha tano na sita na kumpa moyo. Anasema kwa namna alivyofeli kidato cha nne ingekuwa ni wazazi wengine isingekuwa rahisi kumpa nafasi ya kuendelea kusoma.
Baba mzazi wa Agnes ni mjasiriamali, anauza magazeti, vitabu na majarida katika barabara ya Samora jijini Dar es Salaam, mama Agnes pia anafanya biashara. Kwa kuwa Agnes alidhamiria kufaulu, ilimbidi pia asome vitu vingi kadri alivyoweza ili kujiongezea ufahamu zaidi wa yale waliyokuwa wakifundishwa darasani na anatoa changamoto kwa walimu kuwazoesha wanafunzi kufanya mitihani ili wajiamini. “Ujiamini wewe mwenyewe kwanza, ujiamini kwamba mimi nimesoma na ninaenda kufanya mtihani, uwe na hicho kitu kinasaidia,” anasema msichana huyo.
“Usitegemee vitu vya darasani tu, tafuta ‘other resources’ (vyanzo vingine zaidi ya vya darasani),” anasema msichana huyo aliyedhamiria kusoma sheria kuanzia mwaka huu wa masomo ya elimu ya juu. Kuhusu mtazamo wake kwenye masomo wakati akiwa kidato cha tano na sita, Agnes anasema umemwezesha kujiwekea historia ya maisha yake na kuipa sifa familia iliyosikitishwa na matokeo yake ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne. Alihitimu kidato cha nne mwaka 2006 katika Shule ya Mtakatifu Anthony, Dar es Salaam, akapata daraja la 3 pointi 24.
Anasema baba yake alikasirika lakini mama yake na bibi yake mzaa mama aliyemtaja kwa jina moja la Matilda, walimfariji na kumpa moyo. Kwa mujibu wa msichana huyo, mama yake alimweleza kwamba hata angepata daraja la pili katika matokeo ya kidato cha sita, lingekuwa jambo zuri kwa kuwa matokeo hayo yangemsaidia apate chuo ambacho kingemsaidia awe na maisha mazuri baadaye. Anasema kwa namna alivyosoma kidato cha tano na sita na alivyofanya Mtihani wa Taifa, alifahamu kwamba hata kama angefeli asingekosa daraja la tatu.
Licha ya kuwa na uhakika huo, aliogopa kwenda kuangalia matokeo kwa kuwa alikumbuka namna alivyoumia wakati alipokwenda kuangalia matokeo ya kidato cha nne. “Form four’ (kidato cha nne) nilikwenda kuangalia mwenyewe na nilifeli vibaya sana,” anasema msichana huyo na kubainisha kwamba, miongoni mwa mambo yaliyosababisha afeli ni kutumia muda mrefu kuangalia sinema nyumbani. Anapenda uigizaji wa Michael Scolfild na kwa sasa anafuatilia mfululizo wa sinema za Prison Break.
Anaamini kwamba amefaulu sana masomo aliyoyaona ni magumu kwa kuwa anaamini mtihani ukiwa mgumu, mtahiniwa hulazimika kutumia uwezo wa ziada wa kufikiri ili kujibu maswali, na anahisi huenda ugumu wa mtihani huo ndio ulimsaidia. Anasema mwanafunzi anapaswa kufahamu ni mazingira gani akisoma atafaulu vizuri, mtazamo huo umemsaidia kwa kuwa alitambua kuwa hakufanya vizuri kidato cha nne kwa kuwa hakusoma shule ya bweni. Alisoma St Anthony kuanzia mwaka 2003 baada ya kuhitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chang’ombe iliyopo Temeke, Dar es Salaam.
Anaamini kwamba asingesoma katika shule ya bweni asingefaulu vizuri kwa sababu kusoma huko kulimsaidia kujitambua vizuri kwa kuwa suala la kwenda shule, kula, kulala, na kupata kila unachotaka havikuwapo. Anasema, alivyokwenda shule ya bweni maisha yalikuwa magumu kwake, hakuwaona wazazi kama alivyokuwa amezoea kuwa nao, na hakuweza pia kuwasiliana nao hata kwa simu. “Hayo maisha ya ‘mshike mshike’ ndiyo yamenisaidia kusoma vizuri zaidi,” anasema na kueleza kuwa yeye alipokuwa shule ya bweni alikumbuka nyumbani lakini alijua kukumbuka nyumbani hakumpi msaada.
“You don’t go anywhere (huendi popote), yaani ukiingia ndiyo mpaka Juni, unajua watu wengine hawaamini… yaani yale ndiyo maisha yako ya miezi sita,” anasema msichana huyo anayependa kutazama kandanda. Agnes ambaye ni shabiki wa timu ya Manchester United ya Uingereza, alianza kuwapenda ‘Mashetani Wekundu’ kwa kuwa baba yake alikuwa akimnunulia zawadi timu hiyo ikishinda, mjasiriamali huyo sasa anaishabikia timu ya soka ya Liverpool ya huko huko Uingereza.
“Nampenda sana Christian Ronaldo, yaani akihama tena dah,” anasema msichana huyo. Kwa upande wa muziki anawazimia TID na Makamua, na nje ya Tanzania anampenda Akon. Anapenda kujifunza taaluma ya sheria, amewasilisha maombi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). “Napenda kuona kila mtu anapata haki yake, hata mimi mwenyewe sipendi kunyanyaswa,” anasema na kuongeza kwamba, watu wengi wanasema masomo ya sheria ni magumu, anataka kusoma masomo hayo ili aone huo ugumu ni upi.
Anasema, miongoni mwa kazi ambazo hapendi kuzifanya ni kuwa mwalimu kwa kuwa, huwa anajisikia vibaya kuona mtu analia. “Nina moyo wa huruma, kuchapa kiboko mtu na kuona analia sipendi,” anasema. Anafuatilia maisha ya Dk. Asha-Rose Migiro, anapenda kuwa kama yeye na kufikia kiwango cha mafanikio alichofikia Mtanzania huyo ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN). Dk. Migiro pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kabla ya kuingia UN.
Anasema, akipata nafasi ya kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, atamshauri aimarishe mapambano dhidi ya rushwa ndogo kwa kuwa ni msingi wa kuimaliza rushwa kubwa. “Unajua huwezi ukafanya kitu cha ‘level’ kubwa wakati cha ‘level’ ndogo bado kinaendelea…mimi naamini kama ikiisha ya huku chini ya huko juu itaisha,” anasema. Msichana huyo anatumia muda mrefu kukaa nyumbani kutazama sinema na kusaidia kazi. Anafahamu kupika ugali, maharage, chapati, lakini anapenda kupika nyama. “Yaani nipike nyama nisionje hata vipande viwili jamani,” anasema. Anasema, ataolewa atakapokuwa tayari kuwa na familia na atapenda kupata watoto wawili.