WIMBI la ujambazi linazidi kutikisa nchi baada ya watu 14 kuuawa na wengine 17 kujeruhiwa kwa risasi katika shambulio lililofanywa na kundi la majambazi kwenye kisiwa kidogo cha Izinga kilicho wilayani Ukerewe na wengine 17 kujeruhiwa kwa risasi.
Katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Jakaya Kikwete alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanikiwa kupunguza wimbi la ujambazi, lakini siku chache baadaye kuliripotiwa matukio makubwa ya ujambazi, likiwemo la mkoani Ruvuma ambako askari polisi walinusurika kuuawa baada ya kushambuliwa na majambazi na kuporwa bunduki mbili.
Tukio jingine lilitokea mkoani Mwanza ambako jambazi mmoja aliuawa wakati polisi wakirushiana risasi na kundi la majambazi katika jaribio la uporaji kwenye mgahawa wa UTurn.
Hali imekuwa mbaya zaidi kwenye kisiwa cha Izinga kilicho Ziwa Victoria ambako majambazi hao walivamia majira ya saa 9:25 usiku.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliiambia Mwananchi kuwa umati wa watu ulijitokeza kujaribu kupambana na majambazi hao baada ya kusikia kelele za kuomba msaada.
Mashuhuda hao walisema baada ya wananchi kujitokeza, mmoja wa majambazi hao aliwafyutulia risasi na kasababisha majeruhi na vifo vya watu hao.
Waliongeza kuwa awali waliposikia mlio wa bunduki, walidhani ni baruti, lakini baada ya kelele hizo walijikusanya kwa ajili ya kuwakabili na wananchi wengine walienda kujaribu kuharibu mtumbwi wao ili wasiutumie kutoroka, ndipo majambazi hao wakamimina risasi na kuua watu zaidi.
Walidai kuwa kundi la majambazi hao lilivamia kisiwa hicho usiku likitumia mitumbwi miwili ya injini, lakini wananchi walibaini kuingia kwao na kuwazingira. Baada ya kubaini kuwa wamezingira, walianza kufyatua risasi na kusababisha vifo vya wananchi saba.
Katika mashambulizi hayo wavamizi hao waliweza kujeruhi watu wengine 17 na wao wananchi kufanikiwa kuwaua wavamizi hao wawili.
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Ukerewe, Queen Mwashinga Mlozi alisema kati ya watu hao waliokufa wawili wanasadikiwa kuwa ni majambazi.
Mlozi ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Ukerewe alisema tayari taarifa ya tukio hilo ameifikisha kwa uongozi wa mkoa na kuongeza kuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama walifika eneo la tukio ili kupata taarifa zaidi za tukio hilo.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Dk Faustine Nkinga alisema hali za majeruhi bado ni mbaya na kwamba wanaendelea na kazi ya kunusuru maisha yao kwa sababu kati yao wanne walipoteza damu nyingi na wengine walifanyiwa upasuaji ili kuwaondoa risasi kwenye miili yao na wengine wamehamishiwa Hospitali ya Bugando.
Mkuu wa mkoa, Abbas Kandoro, ofisa usalama wa mkoa, Jason Mutashongerwa na kamanda wa polisi mkoa, Jamal Rwambow waliondoka asubuhi jana kwenda eneo la tukio kujionea hali halisi ya uvamizi huo.
Kandoro alisema kuwa majeruhi wote 17 walihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na hospitali ya Ukerewe kutomudu kuwahudumia wagonjwa hao.
Naye Kamanda Rwambow alisema kuwa watu waliothibitika kuuawa eneo la tukio kisiwani humo ni saba na watu wengine watano ambao walipelekwa wakiwa majeruhi kutibiwa walifariki wakati wakitibiwa. Habari zilizofika baadaye zilieleza kuwa watu wengine watatu walipoteza maisha.
"Mpaka sasa niko na viongozi wengine wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa tukielekea eneo la tukio, lakini ninachoweza kukueleza ni kuwa tukio lipo na watu wamekufa na kati ya hao waliokufa wawili ni majambazi ambao waliuawa na wananchi.
Lakini taarifa kamili nitatoa baada ya uchunguzi kamili na kufika eneo la tukio," alieleza Kamanda Rwanbow kwa njia ya simu.
Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongella alisema kuwa Jeshi la Polisi linastahili lawama kutokana na tukio hilo kwa sababu wananchi wa visiwa vya wilayani Ukerewe walichanga Sh3 milioni ili wajengewe kituo, lakini hadi leo jeshi hilo limeshindwa kutoa maelekezo ya kufanikisha nia hiyo.
"Nimesikitishwa na tukio hili, lakini jeshi la polisi linastahili lawama kutokana na kuzembea kutoa maelekezo kwa wananchi ambao tayari wamechanga Sh3 milioni za kujengea vituo vya polisi katika visiwa vya uvuvi," alieleza Mongella.
Tukio hili linaufanya mkoa wa Mwanza kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa matukio ya ujambazi. Wananchi wamekuwa wakivamia kila mara na kujeruhiwa kwa mapanga, nondo na silaha za moto na kuporwa mali na fedha.
Julai mwaka jana watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walivamia na kuteka Kisiwa cha Ziragula na kujeruhi wananchi zaidi ya 13 na kupora mali na fedha.
Januari 14 mwaka huu majambazi pia walivamia eneo la uvuvi la Igombe na kupora Sh700,000 na kujeruhi wananchi watatu.
source..mwananchi.