WATOTO 4750 kutoka shehia 22 za wilaya ya Wete wanaishi katika mazingira magumu mno, utafiti uliofanywa na kitengo cha hifadhi ya mtoto Pemba, umebainisha.
Afisa kutoka kitengo cha hifadhi ya mtoto Pemba, Raya Said aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kwamba, watoto hao walibainika katika kaya zote zilizo ndani ya wilaya hiyo.
Alisema hao ni wale wanaoishi katika mazingira magumu mno, ambao hawana msaada wala usaidizi wowote, ambapo miongoni mwao wapo pia wanafunzi wa kike.
Shehia zilizoandikisha rekodi ya juu ni Kojani ambapo watoto 186 wakiwemo wanawake 83 wanaishi katika mazingira ya kusikitisha.
Shehia nyengine ni Kigongoni yenye watoto 386 wakiwemo wanawake 201, Mtambwe kaskazini watoto 281 wakiwemo wanaume 117, Pembeni watoto 121, Gando (126), Junguni (100) na Kisiwani watoto 115.
Raya alisema tatizo kubwa linalowakabili watoto hawa ni huduma muhimu za kijamii ikiwemo chakula cha uhakika, mavazi, malazi na matunzo kutoka kwa familia zao, hali iliyowafanya wengi kuishi katika maisha ya kukata tamaa.
Aidha alisema baadhi ya watoto hawana sare za skuli na wale walionazo zimechakaa mno.
Hali hiyo imewafanya watoto wengi kukatisha masomo na kujishughulisha na ajira mbadala ambazo ni hatari kwa afya zao.
Afisa huyo alisema baadhi ya familia zimekuwa zikiwatumia watoto hao kama mtaji; kwa kwenda kufanya kazi ili waendeshe familia zao ikiwemo kupara samaki.
Aliziomba asasi za kiraia za kitaifa na kimataifa kushirikiana na kitengo chake kusaidia kumkomboa mtoto na kumuweka katika mazingira bora kielimu na kiafya.