Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Tume ya Uchaguzi yakabidhi ripoti ya miaka mitano ya tume kwa Rais



 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar,(ZEC) Khatib Mwinyichande,akiongoza ujumbe wa Tume hiyo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar,Kumuaga Rais kwa kumaliza muda wa kazi wa Tume hiyo jana
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Shein,akipokea Ripoti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar,(ZEC) kutoka kwa Mwenyekiti wake Khatib Mwinyichande, alipoongoza ujumbe wa Tume hiyo walipofika Ikulu Mjini Zanzibar,Kumuaga Rais kwa kumaliza muda wa kazi wa Tume hiyo jana.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
WAJUMBE wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar wanaomaliza muda wao wa utumishi, leo wamemkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Ripoti ya miaka mitano ya Tume ya Uchaguzi katika kipindi cha utumishi wao.
Akikabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Khatib Mwinyichande alitoa pongezi kwa mashirikiano makubwa iliyoyapata Tume hiyo katika kipindi chote cha utumishi wao ndani ya miaka mitano.
Wajumbe hao ambao wamefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kukabidhi ripoti hiyo pamoja na kumuaga rasmi Rais baada ya kumaliza muda wao wa kazi, walieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi wao, Tume ilipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa uchaguzi kwa kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika kipindi cha uchaguzi.
Aidha, Tume hiyo ilieleza kuwa ilipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Taasisi/Mashirika ya uchaguzi ya Kimataifa na Kikanda pamoja na kuweza kuwajengea uwezo wa kielemu watendaji wake kadhaa kwa kujiunga na vyuo mbali mbali vya ndani na nje ya Zanzibar.
Katika maelezo yao wajumbe hao walieleza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume iliendesha kwa mafanikio makubwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na chaguzi ndogo nne, pamoja na kusimamia na kuendesha Kura ya Maoni ya mwanzo katika historia ya Zanzibar kufuatia maridhiano ya kisiasa ya terehe 5 Novemba mwaka 2009.
Mbali ya majukumu mbali mbali yaliotekelezwa na Tume hiyo katika kipindi cha utumishi wake ilikuwa ni pamoja na kuendeleza mashirikiano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushauriana juu ya utekelezaji bora wa majukumu ya Tume hizo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, alieleza kuwa ripoti hiyo waliyomkabidhi Rais inatoa muhtasari wa kazi zote zilizofanywa na Tume katika kipindi cha utumishi wake.
Sambamba na hayo, Tume hiyo inayomaliza muda wake ilieleza imani yake kuwa Ripoti hiyo mbali ya kutoa maelezo juu ya kazi zilizofanywa na Tume katika kipindi hicho, lakini pia, itakuwa ni mwongozo kwa Wajumbe wengine wa Tume watakaoteuliwa kushika nafasi zao.
“Ni matumaini ya Tume hii, kwamba Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yalioainishwa katika ripoti hii”,alisema Mwinyichande.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa Tume hiyo inayomaliza kazi zake kwa kazi nzuri iliyoifanya katika kipindi chake chote cha utumishi.
Dk. Shein alisema kuwa chaguzi zote zilizofanywa chini cha Tume hiyo zimefanywa kwa mafanikio makubwa licha ya kuwepo baadhi ya changamoto ndogo ndogo.
Alisema kuwa Tume hiyo imefanya kazi kubwa na nzuri ambapo yeye mwenyewe binafsi pamoja na wenziwe waliomo Serikalini wanathamini sana juhudi za Tume hiyo ilizozichukua katika utumishi wake wote wa miaka mitano.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Tume hiyo imehfanya kazi ya kupongezwa ambayo imewajengea sifa kubwa ndani na nje ya Zanzibar sanjari na kuijengea sifa kubwa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza Wajumbe wa Tume hiyo kuwa, kutokana na uzoefu wa kazi yao hiyo nzuri watarajie kutoa mchango wao wa uzoefu kwa wale wote watakaohitaji mchango huo.
“Hongereni kwa kazi nzuri mliyoifanya katika kipindi hichi cha miaka mitano cha utumishi wenu katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwani kazi yenyewe ni ngumu na hasa joto huzidi wakati wa uchaguzi unapofika”alisisitiza Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwathamini Wajumbe hao huku akiwapongeza kwa juhudi zao za kuwawezesha kielimu watendaji wa tume hiyo kwa elimu ya juu ikiwa ni pamoja na Shahada ya Kwanza,Uzamili na nyenginezo.
Kwa maelezo ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Khatib Mwinyichande kwa Dk. Shein, Tume hiyo inamaliza siku tatu kuanzia leo kwani Wajumbe hao waliteuliwa tarehe 02/01/2008 na kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano na utumishi wao unamaliza tarehe 01/01/2013
Wajumbe hao wanaomaliza muda wao, waliteuliwa na Rais Mstaafu wa awamu ya sita Mhe. Dk. Amani Abeid Karume.
[ Read More ]

MAKACHERO KUTOKA DAR WATUA ZANZIBAR KUCHUNGUZA SHAMBULIO LA PAROKO


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, imetuma timu ya Makachero kuja Zanzibar kuungana na wenzao wengine wa Polisi Zanzibar katika Upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Amrose Nkenda.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Zanzibar ACP Yusuf Ilembo, amesema kuwa timu hiyo ambayo inaongozwa na Afisa mmoja wa ngazi ya juu (hakumtaja jina) ina jumla ya Makachero watano waliobobea katika masuala ya upelelezi hapa nchini.

Amesema kuwa nia ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuituma timu hiyo kuja hapa Zanzibar, ni kutaka kuengeza nguvu katika tukio hili ambalo linatazamwa kwa aina tofauti hasa ikizingatiwa kuwa aliyeshambuliwa ni Kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika kipindi cha siku kuu ya Krismas.

Amesema Jeshi la Polisi limeamua tukio hili kupelelezwa kwa pamoja kati ya wenzao wa makao makuu ya Polisi Dar es salaam na wa hapa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika kumshambulia Paroko huyo wanakamatwa.

Hata hivyo kamanda Ilembo amesema kuwabado Polisi wanaendelea na Upelelezi wa kubaini sababu za kushambuliwa kwa Paroko huyo bila ya kuibwa kwa kitu chochote kutoka kwa mshambuliwa.

Amesema kuna uwezekana kuwa watuhumiwa wameshindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio lisingekuwa salama kwao kwa vile kulikuwa na walinzi na ni eneo ambalo ni karibu kabisa na makazi ya viongozi wengine wa dhehebu hilo.

Akizungumzia siku kuu ya mwisho wa mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2013, Kamanda Ilembo amewahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa wahalifu ili wachukuliwe hatua.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wadogo kuranda barabarani ama kwenda katika fukwe za bahari kuogelea pasipo uangalizi wa watu wazima.

Kamanda Aziz amesema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari ama kuzama na kufa maji katika siku hizi za siku kuu za mwisho wa mwaka kwa kukosa uwangalizi wa watu wazima.

Aidha amewataka wananchi kutoziacha nyumba zao wazi ama bila ya kuwa na uwangalizi wa kutosha ili kutowapa nafasi kwa wahalifu kupata fursa ya kuwaiba.
[ Read More ]