ASKARI mstaafu wa Jeshi la la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Matiko Ng'eng'e (55) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kisu.
Ng'eng'e ambaye alikuwa sanjenti wa jeshi hilo anadaiwa kufanya hivyo saa 11:00 alfajiri ya jana nyumbani kwake Ukonga Mazizini, jijini Dar es Salaam.
Habari ambazo Mwananchi imezipata na kuthibitishwa na Polisi zilisema mauaji hayo yalifuatia mgogoro wa shamba ambalo mtuhumiwa alikuwa ashinikiza liuzwe huku mkewe akipinga vikali mpango huo.
Akisimulia mkasa huo nyumbani kwao, mtoto wa mtuhumiwa huyo, Joyce Matiko (22) alidai kuwa baba yake ana wake wawili wa ndoa na kwamba marehemu alikuwa ni mke mdogo.
Kwa mujibu wa Joyce, mke mkubwa wa baba yake anaishi Banana.
Alisema hata hivyo familia hizo zimekuwa katika mgogoro wa muda mrefu kuhusu eneo ambalo mke mdogo na watoto wake wamekuwa wakiishi na kwamba mgogoro huo ulitokana na baba yao kutaka eneo liuzwe ili apate fedha za kusafirisha familia kwenda kijijini.
"Muda mfupi kabla ya mauaji ya mama yetu, baba alituita watoto wote watano pamoja na mama na kutukanya tusithubutu kuuza eneo tunaloishi hata kama itatokea yeye amekufa.
Tulishangazwa sana baba kutuita na kutukanya eti tusithubutu kuuza eneo hilo, wakati yeye ndiye kinara wa kutafuta madalali kwa siri ili afanikishe zoezi hilo,"alisisitiza mtoto huyo.
Alisema mara baada ya kikao hicho, baba yao aliwataka warudi ndani wakalale na kwamba walifanya hivyo.
Mtoto huyo alisema ilipofika saa 9:30 usiku alisikia kelele za mama yao akiomba msaada kwamba anakufa na kuomba asaidiwe jambo lilowashtua mno.
Alisema baada ya kusikia kelele hizo waliamua kutoka na kumkuta mama yao akiwa amelala chini huku damu zikiwa zinamtoka kwa wingi mwilini.
"Tulimkuta mama akiwa amelala chini katika dimbwi la damu, lakini baba hakuwepo alikuwa amejifungia chumbani, tulipiga kelele za kuomba msaada na muda mfupi tu majirani walifika na kutusaidia kumtoa kabla polisi kufika," alisema.
Alisema baada ya polisi kufika walimchukua mtuhumiwa (baba yao) na mama yao ambaye kwa wakati huo alikuwa ameshapoteza maisha.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo katika Kituo cha Polisi cha Staki Shari, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Kamanda Shilogile alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Amana, kwa uchunguzi na kwamba upelelezi ukikamilka mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara moja.