MAMIA ya wakazi wa kijiji cha Sing'isi kilicho wilayani Arumeru mkoani Arusha, wamevamia kwa siku mbili mfululizo shamba la Madira Estate linalomilikiwa na Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro na kuteketeza kwa moto zaidi ya nyumba 15 zilizo kuwa kwenye shamba hilo na kukata mazao kadhaa yenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Tukio hili limetokea wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa mjini hapa kushiriki matembezi ya kuchangia mradi wa kutoa chakula mashuleni yaliyoandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Wananchi hao waliokuwa na mapanga, visu, nondo na silaha nyingine kadhaa, walianza uvamizi wa shamba hilo kuanzia majira ya saa 3:00 usiku juzi na kuendelea hadi jana asubuhi, vitendo vilivyosababisha kufungwa kwa muda barabara ya Arusha-Moshi.
Licha ya polisi kumwagwa katika eneo hilo na kupiga mabomu kadhaa ya machozi na risasi kadhaa za moto hewani, wananchi hao waliendelea na uharibifu huo na kubeba mbao, mabati na mali mbalimbali zilizokuwa katika eneo hilo.
Wakizungumza katika eneo hilo, baadhi ya wananchi walisema wanapinga serikali kuliuza shamba hilo lenye ekari 50 kwa mbunge huyo wakati wao wana shida kubwa ya ardhi na eneo la upanuzi wa shule yao.
'Hatukubali... hili ni eneo letu. Tutapigana hadi mwisho na hakuna kumilikiwa tena na mbunge. Tumefunga barabara na tumevunja nyumba zote... serikali ilipaswa kutupa eneo letu wananchi baada ya Wazungu kuacha mashamba, lakini ajabu imeliuza," alisema John Akyo mkazi wa kijiji hicho.
Mkuu wa wilaya hiyo, Marcy Silla aliyefika eneo hilo jana asubuhi, alionekana kupigwa na butwaa wakati akishuhudia ujasiri wa wananchi kuendelea kubeba mali mbalimbali kutoka katika nyumba zaidi ya 15 walizovunja, nyumba ambazo zipo ndani ya shamba na nyingine ambazo mbunge huyo amezirithi.
"Sijui lolote kuhusu tukio hili. Nimepewa taarifa leo, lakini nilichoelezwa ni kwamba wananchi wanadai eneo, lakini kweli kwa nini watumie nguvu kiasi hiki," alihoji Silla.
Kimaro, akizungumza na mwandishi wa habari jana, alisema ameshangazwa na uamuzi wa wananchi kuvamia eneo lake pekee wakati jirani kuna Wazungu wana zaidi ya ekari 1,000.
"Nilipata taarifa hizi tangu juzi, nikawapa taarifa polisi, lakini nashangaa hawajachukua hatua hadi usiku wananchi walipovamia shamba. Mimi mzalendo mwenzao kumiliki heka 50 kujenga hoteli imekuwa nongwa!" alisema Kimaro.
Alisema anaamini tukio hilo sio shamba tu, bali kuna siasa ndani yake kwa kuwa anataka kujenga hoteli na ndio maana alianza kulitunza eneo kwa kupanda miti ya asili ambayo imekatwa na wananchi hao.
"Kuna miti zaidi ya 4,000 imekatwa na wananchi. Wanasema eti wanataka kulima... lile eneo ni la hoteli ya kitalii na kabla ya ujenzi nilikuwa nalirejesha kwenye uasilia wake," alisema Kimaro.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Matei Basilio alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hadi jana zaidi ya watu 15 walikuwa wamekamatwa.
"Ni kweli kuna vurugu tangu usiku na vijana wangu wanashughulikia na hadi sasa watu wanakamatwa na vurugu zinaendelea," alisema Basilio jana mchana.
Diwani wa kata hiyo, Petro Kiungani na mwenyekiti wa kitongoji cha Maviruni yalipo mashamba hayo, Desaulo Akyoo, walisema kwa zaidi ya wiki wamekuwa wakitoa taarifa polisi juu ya mpango huo wa uvamizi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
"Nilimweleza mkuu wa polisi wa wilaya kuna vikao vinaitishwa kuchochea vurugu. Wananchi walikuwa wakidai sisi viongozi serikalini tumeuza eneo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa," alisema Kiungani.
Hadi jana mchana vurugu zilikuwa zikiendelea na hakuna taarifa kamili ya hasara ambayo imepatikana. Mkuu wa wilaya hiyo alikuwa akiwaomba viongozi wa serikali ya kijiji cha Singisi kuwasihi wananchi kuacha vurugu hizo.