MHADHIRI mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam, Professa Haroub Miraji Othman, 66, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hoteli ya Abuso Shangani mjini Zanzibar.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia hiyo, Ali Uki alisema kifo cha Professa Othuman kilitokea ghafla akiwa usingizini. Alisema wakati mkewe akimuasha, alistuka alipoona Dk Othman haamki na ndipo alipoita watu kumsaidia.
Alisema mkewe pia aliomba msaada wa kuitiwa daktari ili aende kumpima na kuthibitisha kwamba taarifa za kuthibitisha kifo chake zilitolewa majira ya saa 1:30 asubuhi.
Professa Othman alifika mjini hapa juzi asubuhi akitokea Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kilichotungwa na Professa Thomas Burgess, Ali Sultan Issa na Maalim Seif Sharif Hamad kiitwacho ‘Race Revolution and the Struggle for Human Rights in Zanzibar".
Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi mpya wa Al- Yamin Funguni mjini hapa na baadaye kuhudhuria uzinduzi wa Tamasha la Nchi za Jahazi (ZIFF) hadi majira ya saa 6:00 usiku baadaye kwenda hoteli ya Abuso iliyo Mji Mkongwe akiwa na mkewe Professa Saida Yahya Othman.
“Professa hakuwa anaumwa jana... si mlimuona alivyokuwa katika usinduzi wa kitabu asubuhi na usiku alikuwa katika uzinduzi wa tamasha la ZIFF. Amefariki alfajiri; kwa hakika kila mtu yatamfika mauti yeye ametangulia na sisi tupo nyuma yake ndio ameshatutoka, tunachofanya sasa ni kuwasiliana na jamaa kwa ajili ya matayarisho ya mazishi,” alisema msemaji huyo.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Professa Rwekaza Mukandala alisema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimestushwa na kifo cha mhadhiri huyo na kumuelezea kuwa ni mtu asiyechoka na mchapakazi mzuri.
Profesa Othman atazikwa leo jioni na mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake eneo la Baraste - Michenzani. Habari zinasema atazikwa pembeni kwa kaburi la mama yake mkoa wa Mjini Zanzibar.
Mhadhiri huyo atakumbukwa kwa msimamo wake na heshima aliyokuwa amejijengea kitaaluma katika sheria za kimataifa, masuala ya maendeleo na diplomasia.
Hakusita kuwakosoa viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wakati zilipokuwa zikienda kombo.
Mkuu wa Taasisi ya Mawasiliano ya Umma, Dk Bernadetta Killian alisema kuwa amestushwa na kifo cha mhadhiri mwenzake katika chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha hilo la ZIFF alikuwa Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha na tamasha hilo lilikuwa likirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha serikali, TVZ.
Hadi mauti yanamfika, Professa Othman alikuwa mwenyekiti na muanzilishi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ambacho kilianzishwa kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa watu wenye kipato cha chini.
Mara baada ya kumaliza masomo yake ya juu nchini Urusi, Prof Haroub alirejea Zanzibar lakini hakupata ajira na kufanyiwa mipango na serikali kwenda kufanya kazi Bara.
Professa Othman alikuwa akifanya kazi katika kitivo cha sheria cha UDSM kuanzia miaka ya sabini na amefariki akiwa mhadhiri mwandamizi.
Mbali na elimu yake, Professa Othman alikuwa mstari wa mbele katika kupigania haki na ameshawahi kuteuliwa katika tume mbalimbali, ikiwemo ya kufanya marekebisho ya katiba na tume ya Nyalali.
Tume ya Nyalali ilikuwa ikiangalia mfumo unaofaa kisiasa nchini wakati dunia ikiwa kwenye mageuzi ya kisiasa na kiuchumi baada ya kumalizika kwa vita baridi kati ya mataifa ya mashariki na magharibi. Aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya iliyokuwa Shirika la Habari la Tanzania (Shihata) katika mwaka 1995.
Katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi, Prof Othman alikuwa mwenyekiti wa taasisi ya wangaalizi wa ndani wa uchaguzi ambayo iliingia katika lawama kubwa baada ya kusema uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995 haukuwa huru na haki jambo ambalo lilimsababishia kuwekewa chuki na baadhi ya viongozi wa Zanzibar kutokana na msimamo huo.
Waangalizi waliokuwa chini ya Professa Othman walitoa taarifa ya kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 haukuwa huru na haki tofauti na taarifa ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Mwezi uliopita alihudhuria semina iliyowakutanisha waandishi wa habari waandamizi kuhusu jinsi ya kuhakikisha chaguzi zinazofuata zinakuwa huru na haki bila ya kutawaliwa na fujo pamoja na kutoa mafunzo ya sheria za kimataifa na haki za binaadamu kwa makamanda na wakuu vya vyuo vya mafunzo Zanzibar, ikiwa ni hatua moja ya kuwaelimisha juu ya masuala ya ukiukwaji wa haki za binaadamu.
"Nikiwa hai inshaallah nataka kushuhudia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 unafuata misingi yote ya demokrasia na haki za binadamu, zaidi kwa vyombo vya habari," alisema Prof Othman katika semina hiyo.
Akizungumzia kifo hicho, Mwanadiplomasia Dk. Salim Ahmed Salim na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad walieleza kupokea taarifa hizo kwa mshituko mkubwa na kwamba msomi huyo atakumbukwa kwa mengi, lakini wakasema kubwa zaidi ni utetezi wake kwa wanyonge na kupigania haki za binaadamu.
Naye Prof Abdallah Safari alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha msomi huyo na kuelezea kifo chake kuwa ni msiba mkubwa kwa wanataaluma na jamii kwa ujumla.
"Unajua pengo la Prof Haroub ni kubwa na si kirahisi kuzibika katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu kifo cha mwanataaluma siku zote pengo lake huwa kubwa sana," alisema Profesa Safari.
Alimfananisha Prof Haroub na wanafalsafa wa zamani kama Walter Rodney, aliyeandika kitabu kinachoelezea jinsi Ulaya ilivyorudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi ya Afrika, na kwamba dunia imempoteza mwanadiplomasia mkubwa.
"Kwa Tanzania ukitaka uchambuzi mzuri wa migogoro hususan ya Mashariki ya Kati, Afrika na nchi nyingine, basi bila ya kumpata Profesa Haroub ni vigumu kupata uchambuzi uliokamilika," alisema.
Alisema hii ni wiki ya misiba mikubwa kwa sababu Tanzania imempoteza Sheikh Suleiman Mohamed Gorogosi, aliyefariki kwa ajali ya gari na mwanamuziki nyota wa miondoko ya pop, Michael Jackson wa Marekani.
Alimkumbuka Prof Othman wakati alipofundisha katika miaka ya sabini akiwa UDSM na kuelezea kuwa walikuwa na uhusiano mzuri.
Prof Othman alikuwa mstari wa mbele kuikosoa SMZdhidi ya ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za raia.
Prof Othman ameacha mjane ambaye ni Professa Saida Othman na mtoto mmoja, Tahir Othman.