Kutoka Uuledi hadi Unahodha
Katika viongozi waliobahatika kuteuliwa katika nyadhifa kubwa na huku wakiwa na umri mdogo ni Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha. Katika mwaka 2000 akiwa na umri wa miaka 38 tu, alikabidhiwa moja ya vyeo vya juu kabisa katika nchi ya Zanzibar kwa kuteuliwa na Rais wa wakati huo Aman Abeid Karume kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Waziri Kiongozi kikatiba ndiye mwenye dhamana ya kusimamia na kuiendesha serikali kwani yeye huwajibika kwa Rais pekee katika utendaji. Mawaziri wote huripoti kwake kwa kupokea maelekezo na maagizo ya utendaji.
Alipochaguliwa, wengi walishangazwa na uteuzi wa Rais na ninaweza kudiriki kutamka hata mwenyewe alijishangaa lakini aliyapokea maamuzi ya Rais kwa mikono miwili na kuingia kazini akiripoti katika Ofisi ya Waziri Kiongozi hapo Vuga.
Waliobahatika kukikalia cheo hiki kabla yake walikuwa ni wanasiasa waliobobea au wakongwe waliokuwa na uzoefu katika siasa kama Mheshimiwa Ramadhan Haji Faki (Februari 1983 – Februari 1984), Maalim Seif Sharif Hamad (Februari 1984 – januari 1988), Dk Omar Ali Juma (Januari 1988 - Oktoba 1995) Dk Mohammed Gharib Bilaal (Oktoba 2005 – Novemba 2000). Hivyo wengi walikuwa na hamu ya kuona utendaji wa Waziri Kiongozi mpya, kijana mgeni kwenye ulingo wa siasa na hasa wakati alipoingia katika Serikali kulikuwa na vugu vugu la msuguano wa vyama viwili vyenye nguvu CCM na CUF.
Mheshimiwa Nahodha alizaliwa 20/11/1962 na kupata elimu yake katika Skuli ya Msingi Kiongoni huko Makunduchi na kuendelea Sekondari katika Skuli ya Benbella na kisha kufanikiwa kujiunga katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. Ana Shahada ya kwanza aliyoipata Chuo Kikuu cha Daressalaam katika fani ya elimu na pia stashahada aliyoipata katika Chuo cha Diplomasia hapo Dar. Huko mitaani hujulikana kama mtoto wa mkulima na mkwezi alizaliwa shamba Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mheshimiwa Nahodha ni Kijana msomi wa Chuo Kikuu mwenye shahada, mtaalamu wa lugha, mwanadiplomasia, mwandishi, mwenye kipaji na mwerevu. Historia yake haioneshi kuwa na dhamana yoyote kubwa kabla ya kujitosa katika siasa na kugombania uwakilishi katika jimbo lake na kuibuka mshindi. Kilichobakia baada ya hapo ni historia kwani nyota yake ghafla ilipaa kutoka Ofisa Habari katika Wizara ya Habari mpaka Waziri kiongozi.
Ameweza pia kuweka historia kwamba yeye ndiye Waziri Kiongozi aliyeikwaa nafasi hii akiwa na umri mdogo aliyedumu muda mrefu kupita Mawaziri viongozi wote waliopita na pia kuwa Waziri Kiongozi wa mwisho katika Historia ya Zanzibar inayoendelea kwa kuwa cheo hiki tayari kimefutwa katika katiba ya Zanzibar.
Ameweza pia kuweka historia kwamba yeye ndiye Waziri Kiongozi aliyeikwaa nafasi hii akiwa na umri mdogo aliyedumu muda mrefu kupita Mawaziri viongozi wote waliopita na pia kuwa Waziri Kiongozi wa mwisho katika Historia ya Zanzibar inayoendelea kwa kuwa cheo hiki tayari kimefutwa katika katiba ya Zanzibar.
Mheshimiwa Nahodha wakati wa uongozi wake kama Waziri Kiongozi, vijana walitarajia mengi kutoka kwake kama ambapo wazee walitarajia mageuzi ya kiutendaji. Sijui ni wepi waliofaidika na ndoto zao ila tu udiplomasia ulishika hatamu katika matendo yake na hata katika kuchukua maamuzi. Wakati wa maamuzi mazito hakuonekana msimamo wake na wala katika muda aliokuwapo madarakani hakuna jambo ambalo tunaweza kulitaja na kulinasibisha na jitihada zake binafsi kulitetea au kulisimamia jambo lililopelekea kunasibishwa na upole na yeye kudai si upole bali ni urasimu wa kimadaraka na aliwahi kunukuliwa akikataa masuala ya papo kwa papo katika Baraza la Wawakilishi akidai hawezi kuyazungumzia mpaka awasiliane na mkuu wake wa kazi Mheshimiwa Rais. Kauli hii ilitafsiriwa na wachambuzi wa Siasa kwamba anaonekana kama ni kondakta tu na si dereva, uledi tu ni si nahodha aliyepewa usukani kulipeleka jahazi.
Waliosomea udiplomasia huwa ni vigumu kuwajua misimamo yao kwani si rahisi kuweza kuwatambua wamesimamia wapi hasa kutokana na kauli zao kutokuwa na utashi wa kupendelea upande mmoja. Na ndivyo alivyokuwa Mheshimiwa Nahodha kwa muda wote wa utendaji wake.
Na hili pia halikumzuia kufikiria kuin’garisha zaidi nyota yake kwa kuingia katika kinyan’ganyiro cha urais 2010 ambapo jina lake lilivuka kisiwandui na kuweza kufika Dodoma lakini kwa bahati mbaya halikurudi huku akinasihiwa kwamba bado kijana ana muda zaidi wa kujijenga kisiasa kama ‘walivyoombwa’ kina Jakaya 1995 na Bilal 2005.
Aligombea tena uwakilishi katika jimbo lake na kushinda kwa kishindo huku wengi wakijiuliza mantiki na sababu ya mtu kama yeye aliyefikia cheo cha Uwaziri kiongozi kugombea kiti cha uwakilishi kwani ni kama kujishushia hadhi (demotion).
Kulipotangazwa viongozi wakuu wa serikali ya umoja wa kitaifa jina la Mheshimiwa Nahodha halikuwemo ila siku chache baadae tukasikia kuchaguliwa mbunge wa kuteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Serikali ya Muungano.Na lilipotajwa baraza la mawaziri wa Muungano jina la Mhe Nahodha lilikuwamo kwa kuteuliwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi.
Wizara aliyokabidhiwa Nahodha ni moja katika wizara zinazodaia kuwa ni za Muungano na mojawapo katika wizara nyeti na yenye majukumu mazito ya kusimamia Polisi, Uhamiaji, Magereza, Zimamoto na kadhalika. Ni wizara ambayo tukiangalia Mawaziri kutoka Zanzibar waliobahatika kuisimamia huko nyuma walikabiliwa na changamoto nyingi kufikia wengine kujiuzulu kama alivyofanya Ali Hassan Mwinyi miaka ya sabini. Ali Ameir Mohammed anaikumbuka vizuri wizara hii ambayo ingawa inaitwa ya Muungano ila ndani yake kuna idara ambazo si za Muungano kama Magereza na Zimamoto.
Na hapa ndipo tunapotarajia kumuona the Real Captain –Nahodha wa kweli kama lilivyo jina lake na wengi watarajie vitendo pia kwani hana tena uuledi sasa tayari uNahodha umepata mwenyewe. Tena si Nahodha wa ngarawa, dau, mashua au jahazi sasa ni nahodha wa meli haswa iitwayo M.V mambo ya ndani.
Kama kujijenga zaidi kisiasa na kukomaa hii ni changamoto atakayokabiliana nayo katika kuisimamia Wizara yenye kashkash na mikeke ya kila aina na kila siku. Wizara isiyokupa muda wa kupumua wala kutafakari kwa kina na tayari ameshaanza kuyaona kwani migomo ya wanafunzi hiyo hapo, ikifuatiwa na migomo ya wafungwa na mahabusu inayonukia huku Jeshi la Polisi likiangazwa angazwa kwa ‘ukimya’ wake kwa mambo mengi na karibuni vitendo vya Polisi wenye vyeo vikubwa kuhamishwa vituo vya kazi kwa kupotea vidhibiti – madawa ya kulevya, migomo ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo inadaiwa kuwa wanafunzi waliouawa baada ya Polisi kutumia nguvu myingi, maandamano ya CUF kudai katiba mpya. Haya yametokea katika kipindi cha miezi miwili tu tokea kuteuliwa kwake.
Mazingira ya kazi pia yanatofautiana na alipokuwa Waziri Kiongozi kwani kule visiwani hakukuwa na changamoto za waandishi, wasomi, viongozi wa makanisa,viongozi wa misikiti, jumuiya za kiislamu, wadadisi na magazeti lukuki yakiangalia kila kinachojiri hata kama kasindano kameanguka basi hufuatiliwa kulikoni. Visiwani mambo yalikuwa mswano kule hewalla bwana tu na likitokea basi pongezi ndizo zitakazotawala kuliko lawama.
Majuzi aliripotiwa kugomea chakula kilichoandaliwa katika mkutano na Wazimamoto wanaojitegemea ambao pia alikutana na matatizo kibao kutoka kwa wazima moto na lawama za wananchi kiwango kikubwa wanachotozwa kupata huduma hii ambao kimsingi hawana uwezo nayo.
Tokea kuteuliwa kwake tumesikia maagizo mengi yakitoka na mpaka sasa bado hatujapata kusikia au kuona udhaifu wake kiutendaji ila maagizo tu yatatosheleza kuwafanya watendaji wengine wachacharike? Tumesikia maagizo kwa wakimbizi, kwa wahamiaji, kwa vitambulisho vya taifa na mara nyingi huwa tunajiuliza vipi Mawaziri kutoka Zanzibar wanaweza kuyasimamia maslahi ya kizanzibari ndani ya Muungano kwa kuyapa kipaumbele na kuelekeza maendeleo nchini mwao.
Hivyo kwa wale wanaotaka kumuona na kumjua the real Captain, karibuni kwenye Mv Mambo ya Ndani tumuone Nahodha - si wa jina tu bali na vitendo pia.
Kama kweli Meli imepata mwenyewe au vyenginevyo time will tell.
Mdau