baadhi ya wananchi wa manispaa ya mji wa Zanzibar wamelalamikia kupanda kwa bei ya mazao ya kilimo siku moja baada ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya wateja katika soko la Mwanakwerekwa wamesema bidhaa nyingi zinazotumika kwa ajili futari zimepanda bei ikilinganishwa na siku za kawaida.
Wamesema mazao yaliopanda bei ni pamoja na ndizi ya mkono mmoja inayouzwa kati ya shilingi elfu tatu na 1,500, kwa dole moja, viazi vikuu na majimbi yanauzwa kati ya shilingi elfu mbili na 5,000 kwa fungu.
Maboga yanayouzwa shilingi 1,500 hadi 4,000 kwa boga moja, na ndizi mbichi aina ya mtike inauzwa kati ya shilingi 2,000 hadi elfu nne kwa chana moja, huku nazi ikiuzwa kati ya shilingi 800 hadi elfu moja.
Miongoni mwa wateja hao Ali Kassim kutoka Fuoni, wilaya ya Magharibi ameiomba serikali kuwapunguzia ushuru wafanyabiashara wanaoingiza mazao nchini ili kupunguza bei ya mazao hayo masokoni.
Nao wafanyabishara wa mazao hayo wakizungumza na Zenji fm redio juu ya kupanda bei kwa mazao hayo wamesema mazao hayo wananua kwa bei ya juu kutokana na uzalishaji wake mashambani kuwa mdogo.
Mbali na serikali kuwataka wafanyabiashara kupunguza bei za bidhaa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa ramadhani, lakini bado kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ya mazao hayo.
Wakati huo huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshauriwa kuweka udhibiti wa bei za mazao yanayoonekana kupanda kiholela hasa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhani.
Mfanyabishara wa soko la Chakeche Hamis Juma Hamis amesema serikali haijaweka kitengo kinachosimamia bei na kusababisha wafanyabiashara kuuza mazao hayo kwa bei ya juu.
Amesema mazao yanayonekana kupanda bei ni pamoja na ndizi za mkono mmoja, mtwike, viazi vikuu na majimbi yanauzwa kwa bei ya juu.
Nae mnunuzi wa soko hilo Fatma Ali amesema wafanyabishara wanaufanya mwezi mtukufu wa ramadhani kujinufaisha kibiashara na kuwataka kupunguza bei ili watu wenye uwezo mdogo kumudu kununua futari
Nae katibu wa afisi ya mufti Zanzibar Sheikh Fadhili Sorofa amewausia wafanyabiashara kumuogopa mwenyezi mungu kwa kutopandisha bei za bidhaa. Amesema wafanyabiashara wanadhima kubwa iwapo watanunua bidhaa kwa bei nafuu na kuziuza kwa bei ya juu