Dk. Ali Mohamed Shein alizaliwa Machi 13, 1948 katika Kijiji cha Chokocho kilichoko Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba. Dk Shein ameoa, ana watoto na wajukuu.
ELIMU
Msingi na sekondari
Alipata elimu yake ya msingi na sekondari kisiwani Unguja. Elimu ya msingi alisoma katika Shule ya Wavulana Gulioni kati ya mwaka 1956 na 1964 na alijiunga na Shule ya Sekondari Lumumba mwaka 1965 na kuhitimu mwaka 1968.
Elimu ya Juu
Mwaka 1969 alikwenda nchini Urusi na kujiunga na Chuo Kikuu cha Vorenezh (State University) kwa kozi ya maandalizi ya mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu. Baada ya kuhitimu kozi hiyo (mwaka 1970) alijiunga na Chuo Kikuu cha Odessa kusomea masuala ya tiba ya magonjwa ya binadamu (medical biochemistry) hadi mwaka 1975 alipohitimu na kutunukiwa shahada ya uzamili. Alirudi nyumbani kufanya kazi hadi mwaka 1984 alipokwenda nchini Uingereza kuchukua masomo ya shahada ya juu ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Newcastle Upon Tyne. Alihitimu masomo hayo mwaka 1988 na kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika “Clinical Biochemistry and Matabolic Medicine” akiwa amejikita katika eneo kwa jina la kitabibu “Inborn errors of Metabolism”.
MAFUNZO MENGINE
Mbali na mafunzo hayo, Dk. Shein alipata mafunzo mengine mbalimbali katika fani ya tiba na uongozi ndani na nje ya nchi. Miongoni mwayo ni mafunzo juu ya utiaji na utoaji damu pamoja na namna ya uendeshaji wa Benki za Damu (Blood Transfusion Services and Operation of Blood Banks) yaliyofanyika mwaka 1981 Stockholm, Sweden. Mafunzo ya Menejimenti na Uongozi (A course in Management and Situation Leadership) yaliyofanyika Dar es Salaam, mwaka 1994 na Mipango kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi Katika Nchi Zinazoendelea (Planning for HIV/AIDS in Developing Countries) yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha East Anglia, Norwich nchini Uingereza mwaka 1995.
UZOEFU WA KITAALUMA
Mara baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, Dk. Shein aliajiriwa kama karani katika Wizara ya Elimu, Zanzibar Mei, 1969 na baada ya muda aliongezewa majukumu ya kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu ‘B’ katika wizara hiyo; majukumu aliyoyatekeleza kwa pamoja hadi Septemba, 1969 ambako aliondoka kwenda masomoni nchini Urusi.
Baada ya kurejea aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Huduma za Maabara katika Wizara ya Afya, Zanzibar mwaka 1979 na kudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1984 alipoondoka tena nchini kwenda nje kwa masomo ya Shahada ya Uzamivu. Alirejea nchini mwaka 1989 ambako aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Patholojia katika Wizara ya Afya, Zanzibar. Mwaka 1991 aliteuliwa kushika nafasi ya Meneja wa Mradi wa Kudhibiti Ukimwi, Zanzibar huku akiwa na majukumu mengine ya kutoa ushauri kwa Wizara hiyo katika masuala ya Huduma za uchunguzi wa magonjwa ya binaadamu na huduma za maabara (clinical biochemistry and Diagnostic Services).
UZOEFU WA UONGOZI NA SIASA
Dk Shein alianza kujishughulisha na masuala ya siasa tangu akiwa kijana mdogo wakati akiwa mwanafunzi. Alijiunga na Umoja wa Vijana wa chama cha Afro Shirazi tangu akiwa shuleni ambapo mwaka1968 aliteuliwa kuwa Katibu wa Habari wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro-Shirazi skuli ya sekondari ya Lumumba. Akiwa nchini Urusi alichaguliwa Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Tanzania,Odessa mwaka 1973-1975. Dk Shein ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa Chama cha Mapinduzi kilichozaliwa mwaka 1977 kufuatia kuunganishwa vyama vya TANU na ASP. Amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 1997 hadi sasa na amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu tangu mwaka 2001 hadi sasa.
Dk Shein aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar tarehe 29 Oktoba 1995 na tarehe 13 Novemba aliapishwa kuwa Naibu Waziri wa Afya Zanzibar. Alishinda uchaguzi wa nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mkanyageni, Kisiwani Pemba Novemba mwaka 2000 na kuteuliwa kushika nafasi mpya ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Katiba na Utawala Bora katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alidumu katika wadhifa huo hadi tarehe 13 Julai 2001 alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Makamu wa Rais aliyemtangulia Dk Omar Ali Juma kilichotokea 4 Julai 2001.
Alikuwa mgombea mwenza wa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi, alitangazwa tena na Tume ya Uchaguzi kuwa Makamu wa Rais tarehe 17 Disemba 2005 kufuatia ushindi wa Mgombea wa CCM Rais Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Aliapishwa kushika wadhifa huo tena tarehe 21 Disemba 2005 nafasi anayoendelea nayo hadi sasa.
MACHAPISHO NA UANACHAMA KATIKA VYAMA VYA KITAALUMA
Dk Shein ameandika na kuchapisha makala mbali mbali za kitaaluma ikiwemo zile za tafiti za shahada za uzamili na uzamivu.Ni mwanachama wa vyama vya kitaalumambalimbali na amekuwa akishiriki katika Mabaraza na Kamati mbalimbali kwa nafasi tofauti. Miongoni mwao ni kwa mfano alikuwa Mjumbe wa Association of Clinical Biochemists of the United Kingdom (1984-1989), Katibu wa Baraza la Utafiti la Wizara ya Afya Zanzibar (1989-1995). Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Ukimwi (1989-1995),Mjumbe wa Bodi ya Taaluma ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba Muhimbili (1990-1995),Mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Tekinolojia-COSTESH (1990-1995) na Mjumbe wa Chama cha Mapatholojia wa Nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika(1990-1995).
source:kwanza jamii.
source:kwanza jamii.