Mtoto aliyenusurika kimiujiza kwenye ajali ya ndege ya Yemen Airways iliyodondoka kwenye bahari ya Hindi karibu na visiwa vya Komoro na kuua watu 152 ameelezea jinsi alivyonusurika kimiujiza kwenye ajali hiyo. Bahia Bakari mwenye umri wa miaka 14 ndiye abiria pekee aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Yemenia, Airbus A310 iliyotokea alfajiri ya jumanne wiki hii.
Bahia aling'ang'ania mabaki ya ndege na kuelea juu yake kwa masaa 12 katika hali ya hewa mbaya na bahari ambayo imejaa papa wengi kabla ya waokoaji kufika na kumuopoa.
Mtoto huyo ambaye hali yake inaendelea vizuri baada ya kupewa matibabu nchini Komoro amerudi kwao Ufaransa kuungana na baba yake.
Kassim Bakari, baba wa msichana huyo, akiongea na vyombo vya habari vya Ufaransa alisema kuwa nilipoongea naye kwa simu aliniambia "Tuliona ndege ikiangukia kwenye maji, nilijikuta kwenye maji, niliwasikia watu wakiongea lakini sikuweza kumuona hata mtu mmoja. Nilikuwa kwenye kiza sikuona chochote".
"Baba sikuweza kuogelea vizuri, niling'ang'ania juu ya kitu, sijui ni kitu gani" alisema Bahia akimwambia baba yake.
Bakari ambaye ana watoto wengine watatu alisema kuwa aliposikia habari za ajali ya ndege hiyo, moja kwa moja alifikiria kuwa hatamwona tena mkewe na mtoto wake wa kwanza.
"Ni msichana mwenye aibu sana, sikufikiria kama angenusurika namna hii, Siwezi kusema hii ni miujiza bali ni matakwa ya mwenyezimungu" alisema Bakari.
Bakari alisema kuwa Bahia hadi sasa hajaambiwa kuwa mama yake amefariki.
"Walimwambia kuwa mama yako yupo chumba cha jirani ili kutomshtua lakini ukweli ni kwamba mama yake amefariki na sijui nani ataweza kumwambia" alisema baba wa mtoto huyo.
Waokoaji walimuokoa Bahia kwenye bahari ya Hindi kilomita 16 toka kwenye pwani ya Visiwa vya Komoro.
Waokoaji hao walisema kuwa Bahia alikuwa dhaifu sana wakati anaokolewa, hakuweza hata kulishika boya alilorushiwa na hivyo kumfanya mzamiaji kupiga mbizi na kumpandisha kwenye boti ambako alifunikwa na blanket na kupewa maji ya moto yenye sukari anywe wakati anawahishwa hospitali.
Watu wengi wamestaajabu jinsi mtoto huyo alivyonusurika ajali hiyo na kuelea kwa jumla ya masaa 12 kwenye bahari ambayo imejaa papa wengi tena akiwa hana hata life jacket.
source:nifahamishe.com