MAMIA ya wananchi wa Zanzibar na vitongoji vyake wakiwemo wasanii wakongwe na chipukizi, walijitokeza katika mazishi ya marehemu Bakari Abeid Ali aliyefariki dunia jana.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis, Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mwinyihaji Makame Mwadini, Rais mstaafu wa awamu ya sita Dk Amani Abeid Karume, makatibu wakuu na watendaji kadhaa wa wizara mbalimbali.
Akielezea namna alivyoguswa na kifo cha marehemu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi, alimsifia kwa kipaji cha lugha fasaha alichokuwa nacho, akisema daima alijua ni maneno gani ya kuzungumza kwa wakati na pahala maalumu.
Aidha alisema marehemu Abeid alifahamu namna ya kuzifurahisha nyoyo zilizojaa majonzi katika namna ambayo mlengwa alifarajika na kurudi matao ya chini hata kama alikuwa amefura kwa hasira.
Mkuu huyo wa Mkoa alikuwa mshirika wa karibu na marehemu wakifanya kwa pamoja vipindi vya 'Ndivyo tulivyo' na 'Usilolijua' vilivyokuwa vikirushwa na Sauti ya Tanzania Zanzibar na Televisheni Zanzibar miaka kadhaa iliyopita.
Naye msanii mkongwe wa fani za ushairi Haji Gora, alisema marehemu alikuwa kama maktaba kwake kwani aliweza kuchota mengi katika kazi zake za usanii, na kwamba kifo chake ni sawa na maktaba hiyo kufungwa kufuli na ufunguo wake kutupwa katika bahari ya kina kirefu.
Msanii wa maigizo Hassan Suleiman 'Chita', alimtaja marehemu kuwa ni mwalimu aliyebobea na ambaye hakuwa na hiyana katika kutoa ujuzi wake kwa wasanii waliokuwa wakijifunza sanaa.
"Unavyoniona nikiigiza, ni sehemu ya faida nilizopata kutoka kwake, kwani alikuwa akinihimiza kwa kuniambia niwahi kuchota mapema kwani hakuna ajuaye lini ataondoka duniani.