Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lolesia Bukwimba, ametangazwa kuwa Mbunge Mteule wa Jimbo la Busanda, baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vingine vilivyokuwa vikishiriki uchaguzi huo mdogo wilayani Geita.
Mgombea huyo alitangazwa jana kwa kupata kura 29,242 wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho hata hivyo kiliyakataa matokeo, kilishika nafasi ya pili kwa kupata kura 22,799. Chama cha Wananchi (CUF) kilichopata kura 977 na cha United Democratic (UDP) chenye kura 271, ‘viliingia mitini’ baada ya wagombea na mawakala wake kutoshiriki mchakato wote wa kuhesabu na kuhakiki kura katika hatua za mwisho.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi, Dani Mollel, alisema idadi ya waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 135,163, na waliopiga kura ni 55,660, kura halali zikiwa 53,309 na zilizoharibika 2,069. Kabla ya kutangaza matokeo hayo, msimamizi huyo wa uchaguzi aliwaita wagombea wawili waliokuwapo ambao ni Bukwimba na Finias Magesa, kujaza fomu maalumu ya matokeo baada ya kupata takwimu sahihi na kuyathibitisha kabla ya kuyatangaza.
Hata hivyo, wakala wa Chadema, Basil Lema, alisimama na kueleza kwamba mgombea hatasaini fomu hizo, hadi hapo watakapopewa nafasi wagombea na mawakala wao kutoa maoni juu ya mchakato mzima wa uchaguzi na wa kuhesabu kura. Msimamizi wa uchaguzi alifafanua, kwamba hatua hiyo ilifanyika tangu asubuhi baada ya wajumbe wa kikao hicho cha kuhesabu kura kukaa kwa muda mrefu wakiwasubiri wagombea na mawakala wa vyama vingine tofauti na CCM, ikiwamo Chadema, bila kuonekana.
Kutokana na kwamba awali msimamizi huyo alishatoa ufafanuzi juu ya kilichofanyika mbele ya wakala mwingine wa Chadema, Benson Kigaila kabla ya Lema kuingia ukumbini hapo saa 7 mchana huku amechelewa, baadhi ya watu waliokuwa ukumbini walilazimika kuingilia kati kwa kusisitiza kwamba uamuzi wa msimamizi ulifuata sheria. Baada ya majibizano yaliyochukua dakika kadhaa yakihusisha baadhi ya wawakilishi wa CCM na mawakala hao wa Chadema, msimamizi aliamua kumtangaza Bukwimba kuwa mbunge mteule na akataka yeyote mwenye malalamiko, afuate utaratibu wa kujaza fomu maalumu, jambo ambalo mgombea huyo wa Chadema alilifanya.
Kulingana na maelezo yaliyokuwa yametolewa awali kabla ya Lema kuwasili ukumbini, Msimamizi alitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa kikao hicho ambacho waandishi waliruhusiwa kuingia na kusikiliza, kwamba mgombea na wakala wa Chadema walifika wamechelewa, hali ambayo iliathiri mchakato wa kutangaza matokeo. Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi, Mollel, alimfafanulia Kigaila kwamba vyama vyote vilitaarifiwa tangu Mei 15 mwaka huu, kwamba Mei 23 na 24 wakutane katika ofisi hizo za halmashauri ya wilaya kwa ajili ya kuhesabu kura, lakini wahusika (kasoro wa CCM), hawakuonekana na mtandao wa mawasiliano yao haukupatikana.
“Nikapiga kwa wajumbe wa UDP, hawakupatikana. Wiki iliyopita, wajumbe wa Chadema niliwasiliana nao sana kwa mtandao, lakini kipindi hiki (baada ya uchaguzi) wameadimika,” alisema Mollel. Akisisitiza namna alivyovihimiza vyama kushiriki mchakato huo wa kuhesabu kura, msimamizi huyo alisema pia Mei 23 mwaka huu, aliandika barua kwa makatibu wote wa vyama kuwakumbusha waje. Alisema juzi usiku, baadhi walifika akiwamo Mohamed Habib Mnyaa wa CUF ambaye hata hivyo aliondoka saa 7 usiku na kuwaacha wajumbe wengine wakiendelea na mchakato huo hadi saa 12 alfajiri.
Alisema alipompigia Mnyaa, alimwambia endeleeni hali ambayo alisema ilidhihirisha kwamba aliridhishwa na kilichokuwa kikiendelea. Kwa mujibu wa Mollel, baada ya kuona hali hiyo ya wagombea na mawakala kutofika, ilimlazimu kupiga simu kwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajabu Kiravu, ili kupata mwongozo wa nini kiendelee; akajibiwa kuwa hakuna sababu ya kuahirisha kama matokeo yote yamekamilika. “Mkurugenzi akashauri niwakumbushe wajumbe kwa barua na dispatch na akasema ikishapokewa, endeleeni na kikao.
Tukaendelea bila wawakilishi,” alisema msimamizi huyo wa uchaguzi. Akifafanua sababu za kikao hicho kuendelea bila mawakala, Mollel alisema walizingatia kwamba matokeo hayo yalitoka katika vituo ambavyo vyama husika vilikuwa na mawakala na akasema kwa kuchukua uamuzi huo, hawakuvunja sheria. Alisisitiza katika kikao hicho kwamba, “huu si uamuzi wa kuzuia wenzetu kushiriki. Uamuzi ulikuwa halali. Uamuzi sikuufanya kugandamiza chama, bali tumefuata taratibu na ndio wenzetu wakatokea (akimaanisha wa Chadema).”
Kwa upande wa Chadema, Lema na Kigaile walikiri kupokea taarifa ya kuwataka washiriki mchakato huo wa kuhakiki kura, lakini wakasema hawakuelezwa muda wa kufika katika ofisi hizo za Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kazi hiyo. Wakati msimamizi wa uchaguzi, Mollel katika taarifa yake ya awali alisema mchakato huo ulianza usiku wa kuamkia juzi hadi jana alfajiri, kwa upande wa mawakala hao wa Chadema, walidai kwamba walifika katika eneo hilo saa 5 asubuhi kwa kuwa hawakuambiwa muda halisi.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi wa kukataa matokeo hayo, mgombea wa Chadema alisema uchaguzi haukuwa huru kutokana na mazingira yaliyojitokeza wakati wa kampeni. “Zoezi hili liligubikwa na matatizo yanayokiuka misingi ya utawala bora,” alisema Magesa na kuyataja matokeo hayo kuwa ni ya NEC na CCM na kwamba si ya wananchi wa Busanda. Akikariri idadi ya watu 79,703 ambao hawakupiga kura, Magesa alisema Chadema walilalamika tangu wakati wa kampeni juu ya vitendo vya ununuzi wa shahada, lakini NEC ilipuuza kilio chao.
Magesa ambaye aliomba fomu maalumu ya malalamiko kwa ajili ya kuijaza, alidai kulikuwa na vitendo vya ugawaji chumvi, vitisho kwa wapiga kura na pia akalalamikia hatua ya Serikali kuanza mchakato wa kuweka nguzo za umeme katika barabara iendayo kata ya Kamena wakati wa mchakato wa uchaguzi. Wakati huo huo, nderemo na vifijo zilitawala kabla na baada ya mgombea wa CCM kutangazwa kushinda. Kwa upande wa mgombea wa Chadema, Magesa, alionekana mnyonge ndani ya ukumbi wa kuhesabia kura huku akiwa amesindikizwa na watu watatu, tofauti na ilivyotarajiwa.
Mmoja wa viongozi wake, Tundu Lisu, siku ya kuhitimisha kampeni (Jumamosi iliyopita) aliwahimiza wafuasi wake wasikose katika ofisi hizo za halmashauri kushuhudia mchakato wa matokeo, lakini hali ilikuwa tofauti jana kutokana na mgombea wao kujitokeza akiwa na wafuasi wachache bila viongozi wa juu wa chama hicho waliokuwa wakimnadi wakati wa kampeni. CUF ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 ilikuwa ya pili kwa mgombea wake kupata kura 26,000, safari hii imedorora na kuiachia Chadema kutamba ambayo mwaka 2005 ilipata kura 3,000 katika jimbo hilo.