NI ajabu lakini kweli, unaweza kusema vyovyote unavyoweza, lakini mimi nasema, mwacheni Mungu aitwe Mungu.
Nasema hivyo kwa sababu naamini kwamba, ndiye aliyewapa ujasiri marubani wa ndege ya United Airlines, Airbus 319 wakaweza kuiongoza ndege hadi ikatua kwa dharura baada ya mfumo WOTE wa utendaji wa ndege hiyo kufa wakati ikiwa angani dakika 20 baada ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Louis Armstrong huko New Orleans, Marekani jana asubuhi.
Baada ya mfumo huo kufa, moshi ulianza kujaa kwenye chumba cha marubani hivyo walitafuta uwezekano wa kurudi uwanjani lakini hawakuwa na uwezo wa kujua wapo wapi, umbali gani kutoka juu, mwendo kasi, hali ya hewa, hivyo walitegemea miujiza tu.
Walikuwa angani lakini hawakufahamu walikuwa wapi, na umbali gani kutoka uwanjani au umbali gani kutoka ardhini, kwa bahati, waliweza kupata mawasiliano ya simu na mwongozaji ndege uwanjani, akawa anawaeleza waende kushoto au kulia, chini, chini, chini chini na waangalie alama wanazoweza kuzitambua ili wajue wapo wapi.
Kwa kuwa mfumo wote wa ndege hiyo ulikuwa umekufa, ilimaanisha kuwa hata ingefika uwanjani isingeweza kusimama kwa kutumia mfumo wa kawaida wa breki hivyo marubani walilazimika kutumia mfumo wa dharura (backup system) ulio nyuma ya ndege hiyo, Mungu akawasaidia ikatua kwenye majani ikiwa na kiasi kikubwa cha mafuta kwa sababu ilikuwa na safari ndefu.