Alikuwa akihutubia mkutano wa maafisa wa afya ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa mjini Cancun, nchini Mexico.
Dr Chan alisema hatua ya kufanyika kwa mkutano huo nchini Mexico ambako homa hiyo ilianzia, ni ishara kubwa ya kuwa na imani katika nchi hiyo.
“Mexico ni salama, inavutia na ni pahali penye ukarimu mkubwa.”
Alisema kwamba aina ya ugonjwa huo ya H1N1 si hatari mno kwa kuwa ni rahisi kwa mgonjwa kupata nafuu bila ya matatizo.
“Na hapo ndipo tunakumbana na changamoto; kuwapa watu nasaha ya kuelewa wakati wa kupata huduma za matibabu na wakati wa kutokuwa na hofu,” alisema Dr Chan.
Kenya imeripoti visa tisa vya watu ambao wana virusi hivyo. Wote ni wageni kutoka Uingereza ambako inakisiwa maambukizo yatakuwa mengi.
Uganda nayo pia imetangaza kisa kimoja cha ugonjwa huo.
Viongozi na wataalamu kutoka nchi 50 wanakutana mjini Cancun kwa siku mbili ili kujadili mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huo.
Tangu ugonjwa huo kuzuka karibu miezi miwili iliyopita, zaidi ya watu elfu 70 wameambukizwa na zaidi ya mia tatu kufariki dunia.