DHAMIRA ya kuwa na walimu waliofuzu katika kiwango cha Shahada imeanza kufikiwa na katika kipindi kifupo kijacho walimu wote wa skuli za sekondari hapa Zanzibar watakuwa na Shahada ya Chuo Kikuu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), aliyasema hayo katika Mahafali ya saba ya Chuo Kikuu hicho yaliofanyika katika viwanja vya chuo hicho katika Kampasi ya Vuga.
Katika mahafali hayo ambapo pia, aliwatunukia Shahada za Heshima za Uzamivu za Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Salmin Amour Juma na Dk. Amani Abeid Karume kutokana na juhudi zao katika uanzishwaji wa chuo hicho pamoja na juhudi zao katika kuiletea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa Zanzibar.
Dk.Shein katika hotuba yake alieleza kuwa katika kuizingatia tathmini ya miaka kumi ya chuo hicho kuna kila sababu ya kuzingatia kukua kwa idadi ya taaluma zinazotolewa chuoni hapo ambapo leo hii wahitimu 139 walipata Shahada zao za Sanaa na Elimu na 63 walipata Shahada ya Sayansi na Elimu.
Dk. Shein aliwahakikishia wanachuo kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuhakikisha chuo hicho kinatoa fani nyenginezo kama vile Utalii, Kilimo na Udaktari na kueleza furaha yake kwa chuo kuanza kutoa wataalamu wa Fani ya Teknohoma (IT).
Katika maelezo yake Dk. Shein pia, alishauri kwamba Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo kikuu hicho ikuzwe ili iwez mashuhuri kwa lugha hiyo duniani kama ilivyo kwa chuo kikuu cha Oxford, Uingereza kilivyo mashukuri kwa lugha ya Kiingereza.
Alisema kuwa hilo linawezekana huku akieleza kutofurahishwa na tabia ya semina nyingi hapa nchini kuendelshwa kwa lugha ya kiengereza hali ambayo inaonesha kikiviza kiswahili.
Dk. Shein pia, alitilia mkazo suala zima la utafiti kwani kufanikiwa kupitia utafiti kutaongeza kiwango cha mandeleo katika chuo hicho pamoja na kupata sifa nzuri, wataalamu sanjari na kupata jawabu juu ya matatizo mbali mbali.
Akinukuu maelezo ya Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kwa Afrika Bwana Obiageli Ezekwesi, alisema kuwa ni muhimu kwa vyuo vikuu kutilia mkazo ubora wa elimu unaokidhi mahitaji ya kisasa ya uchumi uliojaa ushindani.
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein alieleza kuwa ni wajibu kujipanga vyema na kuhakikisha kwamba matunda ya vyuo vikuu ni kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha, Dk. Shein akieleza maandiko ya Profesa Manuel Castells kuwa Mfumo wa Elimu ya juu uwe ni injini ya maendeleo katika uchumi wa ulimwengu mpya, alisisitiza kuwa mtazamo huo ukitekelezwa ipasavyo vyuo vikuu vitaweza kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya nchi na wananachi wake.
Alieleza kuwa matarajio ya baadae katika chuo hicho ni kuwa na Vitivo vya Uhandisi, Biashara, Taasisi ya Utafiti na Taasisi ya Sayansi za Bahari na kusisitiza kuwa Vitivo hivyo na viliopo vitasaidia kupeleka mbele maendeleo.
Dk. Shein alieleza kuwa ataendelea kufanya kila jitihada katika kushajiisha na kutilia nguvu ushirikiano utakaoleta tija kwa chuo hicho kwa njia ya mahusiano na vyuo vikuu vya nchi za nje.
Pia, Dk. Shein alieleza kuwa jitihada zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha wanafunzi wanasaidiwa ili wawe na mazingira bora ya kujifunzia ikiwemo suala la kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu na kuahidi kuyaangalia maslahi ya Wahadhiri.
“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar itatengewa fedha zaidi katika bajeti zijazo za Serikali kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa wazazi wanaojimudu pamoja na sekta binafsi kwa jumla waunge mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha watoto kupata elimu kwa lengo la kuleta kasi ya maendeleo nchini.
Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Idrisa Ahmada Rai alieleza kuwa dhamira kuu ya chuo wakati kinaanzishwa ilikuwa ni kutayarisha walimu wenye sifa ili kukuza elimu ya msingi na sekondari Zanzibar, na baadae kukitanua na kusomesha masomo negine tofauti chuoni hapo.
Alisema kuwa ndani ya miaka 10 ya SUZA hilo limefanikiwa asilimia 100 ambapo kati ya wahitimi 327 wa leo 284 wamesomea ualimu sawa na asilimia 87 ya wahitimu wote na kueleza kuwa hiyo ni ishara ya SUZA kusonga mbele.
Nae Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume akitoa shukurani baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kutoka chuo hicho, alieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa chuo hicho tangu kuanzishwa kutoa wahitimu 1427 ambapo ingekuwa vigumu kuwapata wahitimu hao wote iwapo chuo hicho kisingelikuwepo na kueleza kuwa hayo yote ni matunda ya Mapinduzi matukufu ya Januari 1964.
Dk. Shein pia katika Mahafali hayo alitoa zawadi mbali mbali kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao, waanzilishi wa chuo kikuu hicho, Makamu wakuu wastaafu wa chuo hicho, Washirika wa Maendeleo waliokisaidia chuo, wafanyakazi bora na wengineo.
Viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar, wawakilishi wa Jumuiya na Mashirika ya Kimataifa na wengineo.