Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Ahadi za Obama kwa Watanzania

-
Rehema Mwinyi.


Rais Barack Obama wa Marekani amemhakikishia Rais Jakaya Kikwete, kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali yake katika kupambana na umasikini na kuwaletea Watanzania maisha bora.

Ili kuhakikisha kuwa ahadi hiyo inatekelezwa ipasavyo, Rais Obama juzi alimwelekeza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na wasaidizi wake Ikulu ya White House jijini hapa kufuatilia kwa karibu na kwa makini ahadi hizo.

Rais Obama juzi alimkaribisha Rais Kikwete katika Ikulu hiyo kwa mazungumzo, akiwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana naye tangu apewe madaraka ya kuongoza Marekani Januari 20, mwaka huu. Clinton alikuwa mmoja wa maofisa sita waandamizi wa Serikali ya Obama waliohudhuria mazungumzo hayo katika Ofisi ya Rais, Oval Office.

Wengine waliokuwapo ni pamoja na Mshauri wa Obama wa Uchumi, Larry Summers ambaye alipata kuwa Waziri wa Fedha wa Marekani, Mshauri wa Masuala ya Usalama, Jenerali James Jones, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Afrika, Balozi A. Carson, ambaye alipata kuwa mwalimu wa kujitolea katika Shule ya Malangali ya Iringa wakati wa ujana wake.

Obama alimwambia Kikwete kuwa uamuzi wake wa kumkaribisha na kumfanya kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana naye, kunatokana na sera za mafanikio na uongozi uliotukuka wa Kikwete. “Napenda kukupongeza kwa uongozi wako mzuri wa Tanzania na pia kwa uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), hata kama umemaliza muda wa uongozi wako wa umoja huo,” Obama alimwambia Kikwete na kuongeza:

“ Nataka ufanikiwe katika uongozi wako. Niambie unataka tukuunge mkono vipi ili uendeleze mafanikio ambayo Serikali yako imeyapata. Unakuwa kiongozi wa kwanza kukutana nami tangu niingie madarakani. Hii ni ishara ya imani yangu na ya Serikali yangu katika uongozi wako. Ninafurahishwa na uongozi wako.” Bila kusita Obama alimwambia Kikwete: “Nataka kuja kutembelea Tanzania.

Mara ya mwisho niliiona Tanzania kutokea upande wa pili wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.” Aliongeza: “ Serikali yangu nzima inavutiwa na uongozi wako. Tunapenda kuunga mkono na kufanya kila linalowezekana kufanikisha hilo ili uendelee kuwatumikia wananchi wa Tanzania.”

Obama pia alimsifu Kikwete katika kuboresha elimu nchini na kumhakikishia kuwa misaada yote ya ujenzi wa miundombinu itakayotolewa chini ya akaunti ya Millennium Challenge Account (MCC) itaharakishwa, ili ujenzi wa miradi hiyo uanze.

“Msimamo wako wa kuweka mkazo katika elimu ni mfano usiokuwa na kifani wa uongozi. Hii miradi ya MCC… tutaangalia nini kifanyike ili ianze kutekelezwa haraka iwezekanavyo na kama lazima tuiongeze.”

Utawala wa Serikali ya Rais George W Bush uliondoka madarakani baada ya kuwa umeidhinisha msaada wa kiasi cha dola milioni 700 kwa ujenzi wa miundombinu katika Tanzania chini ya MCC. Obama hakusema ataongeza kiasi gani katika awamu ijayo ya misaada ya MCC kwa Tanzania, au kama anakusudia kukipiku kiasi kilichotolewa na Rais Bush.

Kikwete alimpongeza Obama kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania na Afrika, lakini akataka Marekani iunge mkono zaidi juhudi za Tanzania katika jitihada za kufuta umasikini, kuhakikisha kuwa kuna chakula cha kutosha katika Afrika kwa kuunga mkono jitihada za kuboresha kilimo, kuendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha elimu na hasa ya sayansi na kuendeleza mapambano dhidi ya malaria, Ukimwi na kifua kikuu.

Kikwete pia aliutaka uongozi wa Obama kuendeleza juhudi za kupunguza vifo vya akinamama wakati wa uzazi na kuisaidia Tanzania na Bara la Afrika kukabiliana na athari za kuvurugika kwa uchumi duniani.

Viongozi hao pia walijadili baadhi ya migogoro mikubwa katika Afrika, ukiwamo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Darfur katika Sudan, Somalia na hali ya kisiasa Kenya. Kikwete pia alimweleza Obama kuhusu jitihada zinazofanywa na serikali kuleta suluhu ya kisiasa Zanzibar.

Obama alimwomba Kikwete kuendelea kuwasiliana na Serikali ya Marekani kwa namna ya kushauri kuhusu jinsi gani serikali hiyo inavyoweza kuchangia katika kutafuta utatuzi wa migogoro inayolikabili Bara la Afrika hasa ile ya DRC na Darfur. Mapema kabla ya kukutana na Obama, Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Clinton ofisini kwake.

Clinton alitaka kujua jinsi Marekani inavyoweza kuisaidia Afrika kuondokana na matatizo yake na Kikwete alitoa maelezo ya kina kuhusu jinsi jambo hilo linavyoweza kufanikishwa. Viongozi hao pia waliijadili Kenya na hali ya kisiasa katika Zanzibar na kuhusu migogoro mingine inayoikabili Afrika.

Leave a Reply