Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mahakama yaamuru hoteli ya Bwawani ipigwe mnada

-
Rehema Mwinyi.


Mahakama Kuu Zanzibar, imeamuru kupigwa mnada Hoteli ya Kimataifa ya Bwawani inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) baada ya kushindwa kulipa deni la mchele la Sh. trilioni 1.6 kwa muda mwafaka.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kampuni ya Leamthore Rice Ltd kutoka nchini Thailand kushinda kesi ya madai namba 4 ya mwaka 1997, dhidi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika kesi hiyo, kampuni hiyo ilifungua mashitaka dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar, baada ya Serikali kuchukua mchele kutoka kampuni hiyo na kushindwa kulipa kwa muda mwafaka.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifunga mkataba wa kibiashara kuchukua mchele kutoka katika kampuni hiyo na kuuza katika soko la ndani la Zanzibar.

Amri ya kupigwa mnada hoteli hiyo ya Serikali ilitolewa na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Yesaya Kayange kufuatia hukumu iliyotolewa Mei 16, mwaka 1997 na Jaji Walfong Dourado.

Kwa mujibu wa barua ya Novemba 12, mwaka huu, uongozi wa Ushirika wa Mnada wa Kumekucha, umetakiwa kupiga mnada hoteli ya Bwawani ambayo ipo mita chache kutoka katikati ya Mji mkongwe wa Zanzibar.

“Ili haki itendeke, uendelee na utekelezaji wa hukumu ya kuuza Hoteli ya Bwawani Zanzibar”, alisema Mrajis huyo katika barua yake hiyo.

Mrajis huyo alieleza kuwa awali Mahakama iliamuru kupigwa mnada Shamba la Serikali liliyopo katika kijiji cha Kijichi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, lakini ilishindikana kutokana kutoeleweka kwa mipaka yake ya ardhi.

Akizungumza na Nipashe, Kiongozi Mwanadamizi wa ushirika wa mnada wa Kumekucha, Salim Ahmed Salim, alithibitisha kupokea amri ya Mahakama inayowataka kuipiga mnada Hoteli ya Bwawani ili kulipa deni la mchele iliyokuwa ikidaiwa Serikali.

Kampuni hiyo ilifungua kesi ya madai Januari, mwaka 1997 baada ya Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar, kushindwa kulipa deni la dola za Marekani milioni 69.4 na kutaka walipwe riba ya asilimia 25 na gharama zote za kesi.

Kampuni hiyo ilikuwa ikitetewa na wakili wake, Masumbuko Lamwai na Mahakama Kuu iliamua kutoa hukumu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi wakati huo, Omar Sheha Mussa, kushindwa kuzingatia wito wa Mahakama na kuamriwa kutolewa uamuzi huo.

Hata hivyo, upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ulichukua juhudi za kutaka kukata rufaa lakini muda ulikuwa umepita na hivyo kuamuliwa kulipwa kiwango hicho cha fedha pamoja na asilimia 25 ya riba tangu kutolewa kwa hukumu hiyo.

Kutokana na deni hilo kutolipwa kwa muda mwafaka, riba ya deni hilo iliendelea kuongezeka kutoka deni ya dola za Marekani milioni 69.4 hadi dola za Marekani biloni 1.6 sawa na bajeti ya miaka mitatu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliingia mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo wakati wa Utawala wa Serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wake marehemu Idrissa Abdul Wakil na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Maalim Seif Sharif Hamad.

Iwapo amri hiyo ya Mahakama itatekelezwa, kampuni nyingi zitaathirika kwa vile hoteli hiyo hivi sasa imepangishwa baadhi ya makampuni yanayofanya biashara ya utalii na uwakala wa mizigo.

Tayari wafanyabiashara marufu Zanzibar na wengine kutoka nje ya nchi, wameanza kufanya matayarisho ya kuinunua hoteli hiyo ambayo ilijengwa kwa nguvu za wazalendo baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.


source;nipashe.

Leave a Reply