Mtanzania aliyeuawa India azikwa bila kichwa
Na Charles Ndagulla na
Na Charles Ndagulla na
Dixson Busagaga, Moshi
VILIO, simanzi na majonzi jana vilitawala mazishi ya Mtanzania Imran Mtui (31) aliyeuawa kikatili nchini India hivi karibuni, katika mazishi yaliyofanyika makaburi ya Njoro Manispaa ya Moshi.
VILIO, simanzi na majonzi jana vilitawala mazishi ya Mtanzania Imran Mtui (31) aliyeuawa kikatili nchini India hivi karibuni, katika mazishi yaliyofanyika makaburi ya Njoro Manispaa ya Moshi.
Mwili wa marehemu huo ulizikwa bila kichwa huku pia ukidaiwa kuwa na majeraha mengi mwilini kuanzia miguuni na kwenye paja lake karibu na kiuno huku kiwiko cha mkono wa kulia nacho kikidaiwa kunyofolewa.
Mwili huo uliwasili mjini moshi usiku wa kuamkia jana baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam, ukitokea nchini India huku gharama zote za kuusafirisha zikibebwa na serikali ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya mazishi, kaka wa marehemu, Maliki Mtui, alisema kuwa wameshtushwa na kifo cha ndugu yao hasa kutokana na marehemu kutokuwa na historia ya ugomvi.
Kwa mujibu wa kaka huyo, mwili huo pia umeonekana kuwa na alama za kamba kwenye mikono yake hali ambayo inaonyesha marehemu kabla ya kuuawa alifungwa kamba ili asiweze kujitetea.
Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea katika mji wa Bangalore nchini India ambako marehemu alikuwa tayari amehitimu masomo yake ya biashara na utawala (Business Administration) na tayari alikuwa akijiandaa kurejea nyumbani.
Kaka huyo wa marehemu aliwaambia waandishi wa habari kuwa mdogo wake huyo alipatwa na mkasa huo akiwa njiani kuelekea mjini ambako rafiki yake wa kike ambaye pia ni Mtanzania aishie visiwani Zanzibar alikuwa akisoma.
“Niliwasiliana naye siku ya tukio kabla hajapatwa na mauti haya nikamuuliza anatarajia kurudi lini nyumbani akanijibu angerudi mapema na rafiki yake alikuwa akimsubiri lakini hakuweza kutokea” alisema.
Pamoja na kuishukuru serikali ya Tanzania kugharamia kuusafirisha mwili wa marehemu mdogo wake, Mtui ameitaka pia serikali kuwathamini raia wake walioko nje ya nchi kwa kufuatilia taarifa zao pindi wanapokumbwa na matukio kama hayo ya kuuawa kwa mdogo wake.
Naye msemaji wa familia ya marehemu Mtui ambaye pia ni shekhe wa msikiti wa Majengo, Shekhe Said Khatibu, alisema kuwa serikali haiwathamini raia wake walioko nje na ndiyo maana serikali haijatoa tamko rasmi kulaani mauaji hayo.
Shekhe huyo pia alisema katika kile kinachoonyesha kuwa idara za serikali zimelala, serikali imeshindwa kutuma hata mwakilishi kwenye mazishi hayo ambayo tukio lake lina utata.
Aidha, alipinga taarifa zote zilizotolewa na madaktari nchini India kwamba marehemu alifariki dunia kwa ajali ya treni na kusisitiza kuwa taarifa hizo sio za kweli.
source:michuzi.