Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II
TAARIFA KWA VYOMBO HABARI
.NATANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE MBEYA MJINI KUPITIA CHADEMA
· NATOA TAMKO RASMI KUHUSU KUHOJIWA KWANGU NA POLISI
Mimi, Joseph Mbilinyi ambaye najulikana zaidi katika anga ya muziki kama “Sugu” ama “Mr II” leo tarehe 29 Juni 2010 natangaza rasmi nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa muda mrefu katika maisha yangu ya kimuziki pamoja na kuimba nyimbo za kuburudisha nimekuwa zaidi mstari wa mbele kuimba nyimbo za kutetea haki za makundi mbalimbali katika jamii na taifa kwa ujumla.
Wakati umefika sasa wa kuhamisha jukwaa la mapambano ya kudai haki kutoka jukwaa la muziki mpaka jukwaa la siasa kwa dhamira ile ile ya kutumia kipaji changu alichonijalia Mwenyezi Mungu kuimba na kuhutubia kwa ajili kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa letu.
Nyimbo zangu zimekuwa zikibeba sauti ya watu wasio na sauti ili zisikike na watawala; lakini hata hivyo kwa kipindi chote ambazo nimekuwa nikifanya harakati hizi watunga sheria na wafanya maamuzi ya kisera chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kuongoza vizuri taifa kuweza kufanya mabadiliko ya kweli yenye kuhakikisha watanzania wananufaika na vipaji vyao ambavyo Mwenyezi Mungu amewajalia na taifa linanufaika na rasilimali na maliasili ambazo tumejaliwa kuwa nazo.
Hivyo natangaza nia ya kugombea ubunge ili kuchangia katika kuongeza nguvu ya chama mbadala katika Bunge letu; niwe sehemu ya sauti mbadala katika kutunga sheria, kuwawakilisha wananchi, kuandaa sera na kuiwajibisha serikali kuweza kutekeleza yale ambayo mimi na wanaharakati wenzangu katika sanaa tumekuwa tukiyapigia kelele muda mrefu kupitia muziki wetu na maisha yetu.
Uamuzi wangu wa kugombea ubunge Mbeya Mjini ni haki yangu ya kikatiba na natambua kuwa kwa kuwa mbunge nitafanya kazi ya kuwawakilisha wananchi wenzangu na kama ambavyo wakati wote nimekuwa nikipambana katika harakati mbalimbali ndivyo ambayo nataka niwe mstari wa mbele kupambana katika kuleta maendeleo.
Huu si wakati wa kampeni hivyo niwaahidi wananchi wa Mbeya kwamba nitaeleza mengi kuhusu sera zangu na ahadi zangu kwao mara baada ya kupitishwa na CHADEMA kugombea ubunge katika jimbo letu.
Hivyo, nachukua fursa hii kuwajulisha watanzania wenzangu kwamba siku chache sijazo nitachukua fomu ya chama ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini.
Lakini kwa ujumla uamuzi wangu wa kugombea umesukumwa na harakati zangu za miaka mingi na ufahamu wangu kuhusu hali halisi ya maisha yetu wananchi wa Mbeya Mjini.
Natangaza nia ya kugombea nikiwa ni mgombea mpya kutoka chama mbadala ili kushirikiana na wananchi wenzangu wa Mbeya Mjini kuondokana na siasa za makundi, ukabila, ubaguzi, na migogoro ambazo zimekuwa zikitawala katika Jimbo letu na Mkoa kwa ujumla na hatimaye kusababisha tuwe na uongozi mbovu unaokwamisha maendeleo.
Jiji la Mbeya linakabiliwa na ubovu wa barabara ukiondoa barabara kuu inayokwenda Tunduma; barabara za mitaani ni mbovu wakati ambapo kuna fursa ya kuwa mkoa wenye makaa ya mawe ambayo mabaki yake yangeweza kutumika kukarabati barabara za mitaani Uyole, Soweto na kwingineko.
Natambua kwamba wafanyabiashara wa Mbeya Mjini wanamalalamiko mengi kuhusu kubambikiziwa kodi huku wafanyabiashara wadogowadogo wakiwa wananyanyaswa katika maeneo wanayofanyia biashara kwa kuwa hata mimi mwenyewe nimewahi kuwa mfanyabishara katika soko letu la Mwanjelwa.
Natambua kwamba jiji letu la Mbeya ni kitovu cha elimu katika mkoa wetu hata hivyo lugha zinazotolewa na uongozi wa Mkoa zinawadhalilisha walimu wakati uongozi huo unashindwa kuweka mazingira bora ya elimu na kusababisha Mbeya mjini kuanza kudorora kielimu. Kwa upande mwingine, kadiri mji unavyopunuka ndivyo kero ya usafiri wa wanafunzi inakithiri na shule za pembezoni zinakosa walimu.
Natambua kwamba kwa muda mrefu Mbeya Mjini yetu ina kero ya umeme wakati ambapo tupo jirani na Mgodi wa Kiwira ambao ungeweza kuzalisha umeme wa kututosheleza lakini kutokana na ufisadi tunashindwa kuondokana na hali hii ambayo inasababisha ugumu na kupanda kwa gharama za maisha na kukosa taa za barabarani hali ambayo inaweka mazingira ya kuongezeka kwa uhalifu.
Natambua kwamba viwanda vyetu vya Mbeya Mjini vimeuzwa kwa bei chee na vingine vimeshindwa kuendeshwa na kubaki magovu na kusababisha vijana kukosa ajira na uchumi kuathirika kama ilivyokuwa kwa viwanda vya pamba, mafuta na nyama.
Natangaza nia ya kugombea ubunge wa Mbeya Mjini kwa kuwa naamini kwamba kero ya maji inayotukabili inaweza kuondolewa tukiwa na uongozi mbadala ambao utaweza kutumia vyanzo mbadala vya maji kama mto Mzovwe, Ivumwe na kutoka katika Mlima Igamba.
Natangaza nia ya kugombea Ubunge ili pamoja na kuingia bungeni niweze kuingia katika halmashauri ya Jiji la Mbeya nishirikiane na wananchi wenzangu kuibua ufisadi na udhaifu iliopo unaosababisha ubadhirifu wa fedha za wananchi na mali za umma kama ilivyotokea kwa milioni 68 zilizobaishwa kwenye ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2007/08; tuhuma za kutaka kuuza kiwanja cha wazi eneo la Sokoine na kushindwa kulipa fidia wananchi wa Kata ya Kalobe waliondolewa katika viwanja vyao.
Wakati huo huo; napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wananchi wenzangu wa Mbeya Mjini, wapenzi wa muziki wangu, wanachama wenzangu wa CHADEMA na watanzania kwa ujumla kwa jana tarehe 28 Juni 2010 nilikamatwa na polisi kwa kile walichonieleza kuwa kuna malalamiko dhidi yangu kuwa nimemtishia kwa maneno kumuua Ruge Mutahaba kupitia wimbo uitwao “Wanna Kill” uliopo kwenye album iitwayo “Anti Virus”.
Walinikamata saa 5 asubuhi nikiwa naingia ukumbi wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa ajili ya kutoa Mada kuhusu “Tathmini ya Muziki wa Kizazi Kipya na Hatma yake nchini” na kunihoji kwa takrabani masaa matano mpaka saa 10 jioni.
Wameniachia kwa kile walichonieleza kuwa ‘dhamana ya kujidhamini mwenyewe’ na kunitaka niripoti kwao siku ya jumatano tarehe 30 Juni saa 5 asubuhi siku ambayo nilipanga kwenye ratiba zangu kurejea nyumbani Mbeya Mjini kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge kabla ya tarehe ya mwisho ya utoaji na upokeaji fomu ndani ya CHADEMA.
Katika mahojiano nao yaliyofanyika Makao Makuu ya Upelelezi Wizara ya Mambo ya Ndani; maofisa usalama (CID) walionihoji walirejea mstari mmoja katika kiitikio cha wimbo husika wenye maneno “I Wanna Kill Right Now” na kusema kwamba mlalamikaji ameutafsiri mstari huo kuwa ni tishio la kutaka kumuua.
Napenda kuwajulisha mashabiki wangu na watanzania wenzangu kwamba nimelieza wazi jeshi la polisi kwamba hakuna wimbo wala maneno niliyowahi kutamka kwa lengo la kukusudia kumuua binadamu yoyote. Niliwaeleza jeshi la polisi kwamba sanaa ya muziki inalugha zake zake za kifasihi.
Maadhui ya wimbo mzima yamejikita katika harakati zangu za siku zote za kupambana na wanyonyaji dhidi ya maslahi ya wasanii Tanzania na wimbo huo una maudhui ya kutaka “Kuondoa ama kuiua dhamira ya mbovu na nia zao ovu”.
Ni vyema mashabaki wangu, wanachama wenzangu na watanzania kwa ujumla wakarejea katika Kamusi mbalimbali za kimataifa ambapoo neno KILL linamaana zaidi ya 10 zikibeba pia maana ya KUKOMESHA, KUONDOA nk.
Katika wimbo huo nimeghani kwa kutumia fasihi mambo ya ukweli yanayotokea katika sekta ya sanaa na wala hauna dhamira yoyote wala maudhui ya kufanya kosa lolote la jinai; hivyo kama kuna mtu ameguswa na ukweli uliomo katika wimbo huo na hakubaliani nao basi aupinge kwa hoja ama akafungue madai badala ya kukimbilia kutaka kuliingiza jeshi la polisi kwenye masuala ya sanaa.
Aidha nimeshangazwa na hatua ya jalada hilo la polisi kufunguliwa ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Wizara ya Mambo ya Ndani yaliyopo Wilaya ya Ilala wakati mimi na mlalamikaji wote ni wakazi wa Wilaya ya Kinondoni.
Baada ya maelezo niliyoyatoa ni matumaini yangu kuwa jeshi la Polisi ambalo lina kazi muhimu zaidi ya kukabiliana na ujambazi na vitendo vingine vya uhalifu ambavyo vinazidi kuongezeka katika Mkoa wa Dar es salaam ambapo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yapo litaelekeza nguvu zake katika kukabiliana na vitendo hivyo vya makosa ya Jinai badala ya kupoteza muda wake kushughulikia masuala ya kifasihi ambayo yana sura ya madai yasiyo na uzito wowote.
[ Read More ]