Askari wawili ambao ni marubani wa Jeshi la Wananchi Tanzania wa Kambi ya Ngerengere ya Morogoro, wamekufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kutua barabarani kwa dharura na kugonga gari la watalii na kupinduka jana katika eneo lijulikanalo kama Zimbabwe katika kijiji cha Manga wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga.
Katika basi la watalii inasemekana kulikuwa na watu 24 ambao 19 kati yao ni raia kutoka Uholanzi, wanne kutoka Kenya na mmoja Mtanzania. Wote walinusurika kufa.
Inasemekana kuwa marubani hao walikuwa katika mazoezi ya kawaida katika anga ya eneo hilo, na kwamba wakati ikiwa angani ndege ilipata hitilafu ndipo rubani akaamua atue barabarani ili kuokoa maisha yao, kabla gari hiyo ikiwa kwenye mwendo mkali iliigonga.
Ndege hiyo ndogo ya JWTZ yenye namba F59119 ilikuwa inatumika katika mafunzo ya kijeshi. Kaimu kamanda wa polisi mkoani Tanga, Afande Jafari Mohammedi, aliwataja waliokufa kuwa ni rubani wa ndege hiyo Meja Kathbet Leguna (41) na mwanafunzi wake Luteni Andrew Yohana Kijangwa (31).
Taarifa zinasema Meja Leguna alikuwa ni mwalimu wa mafunzo ya ndege za kivita katika kikosi hicho cha Ngerengere na alikuwa anamfundisha urubani Luteni Kijanga.
source:issa michuzi blog.