Sakata la watoto wachanga 10 waliofukuliwa na jeshi la polisi katika shimo moja maeneo ya Mwananyamala, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wiki iliyopita limeingia katika sura mpya baada ya mama zao kujulikana.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Mwananyamala kunakotajwa kwamba ndiko maiti za watoto hao wachanga zilikotoka, umebaini kwamba wazazi wanaohusika na tukio hilo wanafahamika na wako katika makundi matatu.
MAKUNDI MATATU
Chanzo chetu cha habari ndani ya hospitali hiyo kimedai kuwa kundi la kwanza lililotajwa kuhusika ni machangudoa wanaopata mimba lakini hawako tayari kulea watoto, hivyo kufika hospitalini hapo kwa nia ya kutoa.
Imedaiwa kuwa machangudoa hao wanapofika hospitalini hapo huongea na baadhi ya wauguzi ambao baada ya kukubaliana kiasi cha fedha, huwawekea maji ya uchungu kisha kujifungua watoto wafu ambao hubaki hospitalini hapo kwa makubaliano kuwa watazikwa na watumishi kwa malipo maalumu.
Aidha, chanzo hicho kiliendelea kudai kwamba, zoezi la kutoa mimba hufanyika kwa siri. Imeelezwa kuwa machangudoa hao wameshajenga uhusiano mzuri na baadhi ya wauguzi ambapo wamekua wakiwapa fedha kuanzia shilingi 30,000 na kuendelea ili kuharibu mimba bila uongozi wa juu wa hospitali kujua.
Imeelezwa kuwa gharama za kuchimba kaburi na kuzika watoto hao wachanga ni kati ya shilingi 20,000 hadi 25,000 ambazo mwenye mtoto hutozwa.
“Siku hizi hata mitaani huwezi kukuta maiti za watoto wachanga zikiwa zimetupwa kwenye mifuko ya plastiki kama ilivyokuwa zamani. Hii ina maana kwamba wameshagundua kuwa hospitali ni kituo chao cha kutolea mimba,” kilisema chanzo hicho.
Aidha, kundi lingine lililotajwa kuhusika na vitendo hivyo ni wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu ambao wamekua wakijihusisha na ngono zembe, hivyo kupata ujauzito.
“Kimbilio lao ni hospitalini ambapo wamekua wakitolewa mimba kwa siri na ndiyo maana hata rekodi za watoto saba waliofukuliwa na polisi hazipo kwenye kumbukumbu za Hospitali ya Mwananyamala,” kilidai chanzo hicho.
Kundi la tatu linalohusishwa na maiti hizo za vichanga ni wazazi wasio na uwezo, wanaojifungulia njiani au hospitalini hapo na kwa bahati mbaya watoto wao kufariki.
Wazazi hao hushawishiwa na baadhi ya wauguzi kutoa fedha kati ya shilingi 20,000 na 25,000 kwa ajili ya kuchimba kaburi na kuzikia kichanga kilichofariki.
JESHI LA POLISI
Tayari jeshi la polisi nchini katika uchunguzi wake hospitali hapo limebaini majina ya wazazi watatu ambao maiti za watoto wao ni kati ya zile zilizofukuliwa wiki iliyopita.
Wazazi hao wametajwa kuwa ni Ruth Mtanga aliyejifungulia njiani Januari 27, mwaka huu na Furaha Rajabu, mkazi wa Manzese aliyejifungua Januari 24 mwaka huu ambaye kumbukumbu zinaonesha kuwa maiti ya mtoto wake ilichukuliwa siku hiyo hiyo na mtu aliyetajwa kuwa ni Zuberi Idrisa, baba mzazi wa marehemu.
Mzazi mwingine ni Regina Samwel, mkazi wa Kimara aliyejifungua hospitalini hapo mtoto mfu. Hata hivyo kumbukumbu katika chumba cha maiti hazioneshi mwili huo kuingia wala kutolewa.
Aidha, kati ya maiti 10 za watoto zilizofukuliwa, saba hazina kumbukumbu kama walizaliwa au kufia hospitalini hapo na kuzua utata kutokana na zote kukutwa zimeviringishwa kwenye shuka moja la Hospitali ya Mwanyamala, moja ikiwa imekaa zaidi ya siku tano kabla ya kuzikwa.
Polisi wanamshikilia mmoja kati ya viongozi wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitaini hapo kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
MTANDAO HARAMU
Taarifa hizo zilieleza kwamba mtandao haramu uliopo hospitalini hapo ni mkubwa kwani unawajumuisha baadhi ya wauguzi, wafanyakazi wa chumba cha kuhifadhia maiti na madaktari.
“Hiki kilichotokea ni kama kutimia kwa usemi wa wahenga kuwa ‘za mwizi ni arobaini’ kwa sababu biashara hii haramu haikuanza leo. Ninaliomba jeshi la polisi liendelee na uchunguzi, watabaini mengi mazito,” kilisema chanzo hicho.
Kiliendelea kusema kwamba, kulingana na makundi hayo matatu, wazazi wanaoweza kujitokeza ni wale waliojifungua wakiwa njiani au hospitalini na kwa bahati mbaya watoto wao wakafariki dunia.
“Machangudoa na wanafunzi hawawezi kujitokeza na inaonekana kuwa maiti saba ambazo wazazi wao hawajulikani wala hakuna kumbukumbu katika vitabu vya Hospitali ya Mwananyamala ni zao,” kilisema chanzo hicho.
USHAWISHI WA WAUGUZI
Habari zaidi zinadai kuwa wauguzi ndiyo wenye ushawishi mkubwa kwa wafiwa ili waache maiti zao kwa makubaliano ya kuacha fedha kwa ajili ya kununulia sanda, kuchimba kaburi na kuzika.
Hata hivyo, imedaiwa kuwa hakuna maiti ya mtoto anayezikwa kaburi lake peke yake na badala yake wote hufukiwa kwenye shimo moja ambalo halina kina kirefu.
Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Mwananyamala umelaumiwa kwa kutokagua kwa umakini chumba cha kuhifadhia maiti kwani inadaiwa kuwa kuna sehemu maalum iliyotengwa kwa ajili ya kuweka miili ya watoto wachanga wakisubiri wawe wengi ndipo wapelekwa kufukiwa katika shimo moja.
HATUA YA SERIKALI
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema ripoti ya tume iliyoundwa bado haijakabidhiwa kwake lakini akaahidi kwamba atakapoipata ataitolea ufafanuzi.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema jana kuwa uchunguzi unaendelea na kuhusu maiti za watoto, hawajazikwa na zoezi hilo litafanyika mara baada ya upelelezi kukamilika.
Wiki iliyopita, watoto wachanga 10 waliofukiwa kwenye shimo moja walifukuliwa na polisi ambapo serikali iliunda tume kuchunguza tukio hilo na wakati wowote kuanzia leo taarifa ya uchunguzi huo itatolewa.
Hata hivyo, tume hiyo imepondwa vikali na baadhi ya wananchi hata kabla ya kutoa taarifa yake kwa madai kwamba asilimia kubwa ya wajumbe wake ni watumishi wa idara ya afya inayolalamikiwa. Watu wana wasiwasi kuwa wanaweza kuficha mambo mengi.
“Tangu lini kesi ya nyani akapewa ngedere na haki ikapatikana? Hii tume ni kiini macho, nia yao ni kupunguza hasira za watu,” alisema Juma Omari, mkazi wa Mwananyamala.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Lucy Nkya, wiki iliyopita alilaani kitendo hicho cha kufukiwa viumbe hao na kusema kuwa kwa kawaida watoto wanaozaliwa na kufa wakiwa na miezi mitano na kuendelea huwa wanahesabiwa kuwa ni viumbe, hivyo wanastahili kuzikwa kwa heshima zote.
source:global puplisher
Categories: