Sheria za kupata viza za wanafunzi nchini Uingereza zinatarajiwa kuwa ngumu zaidi- baada ya kuibuka wasiwasi kuwa mbinu za kuingia nchini humo kwa minajil hiyo hutumiwa kiudanganyifu
Waziri wa mambo ya ndani Theresa May alisema viza za wanafunzi hazitumiwi inavyotakiwa na "wengi wamekuja hapa kufanya kazi na si kusoma".
Alitangaza mpango wa kupunguza idadi ya viza za wanafunzi kufikia 80,000- takriban robo ya idadi iliyopo sasa.
Waziri kivuli wa wizara ya mambo ya ndani Yvette Cooper alionya sheria hazitakiwi kuharibu idara zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni tano kwa mwaka.
Bi May aliliambia bunge kuwa matumizi mabaya ya viza za wanafunzi yamekuwa "ishara ya mfumo wa uhamiaji uliotumiwa vibaya".
Sheria za lugha
Sheria ngumu zilizowekwa ni pamoja na mwanafunzi kutakiwa kuzungumza lugha ya Kiingereza.
Bi May alisema alitaka kumaliza tatizo ambapo wale wanaojifanya wanafunzi hufika kwenye uwanja wa ndege wa Uingereza na kushindwa hata kutaja masomo wanayotarajia kufanya.
Pia utaratibu utazidi kubanwa kwenye kuwaruhusu wanaolelewa na mwanafunzi huyo kujiunga naye Uingereza- na idadi ya miaka ya wanafunzi kutoka nje kukaa Uingereza baada ya kumaliza masomo yao itapunguzwa.
Katika kukabiliana na wasiwasi wa viza za wanafunzi kutumiwa vibaya na wahamiaji wa kiuchumi, kutakuwa na kiwango maalum cha saa za kufanya kazi kwa wanafunzi kutoka nje.
Awali vyuo vikuu vilionyesha wasiwasi wa kupoteza wanafunzi kutoka nchi za nje kutokana na sheria kali za kuomba viza.
Vikwazo vingi vinawalenga wanafunzi walio katika vyuo vya watu binafsi badala ya vyuo vikuu.
Hata hivyo Bi May aliwaambia wabunge kwamba "njia kama hiyo" ya kusoma kupitia vyuo vikuu vitalindwa, iwapo tu vyuo vikuu vitawadhamini wanafunzi.