BODI ya Ushauri wa hospitali Binafsi imeifungia hospitali moja na kutoa onyo kwa hospitali nne kutokana matatizo ya mbali mbali ikiwemo ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha pamoja na mazingira yasiyo salama ya utoji huduma za afya.
Msaidizi Mrajis wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi, Dk. Shaaban Seif Mohammed aliitaja hospitali iliyofungiwa ni Kidongoochekundu Dispensary na zilizopewa onyo kali ni Hassan Clinic, SDA Dispensary, Jang’ombe Dispensary pamoja na Kwamchina Dispensary.
Alitaja miongoni mwa makosa yaliyobainika ni pamoja na kutowasilisha vielelezo vya wafanyakazi wao pamoja na uchafu wa takataka za mabomba ya sindano ambayo yametumika kwa muda mrefu bila kutupwa sehemu husika.
Akizungumzia kwa hospitali iliyofungwa na pamoja na kukuta mfanyakzi mmoja anaefanya kazi zote za kiuguzi pamoja na kidaktari jambo ambalo linaweza kuhatarisha zaidi utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.
Alifahamisha pia kuwa hospitali ya kwa Mchina na DSA Dispensary Jang’ombe ndio zilizobainika kuwa na kasoro nyingi ikiwemo uchakavu wa majengo hasa kuta za ndani pamoja na sehemu ya kufungia vidonda kuwa sakafu yake imechimbika jambo ambalo linaweza kupelekea maambukizi ya maradhi zaidi kwa wagonjwa.
Alisema Bodi hiyo imetoa muda wa mwezi mmoja kwa wamiliki wa hospitali hizo kurekebisha kasoro hizo kwa lengo la kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Alisema vitendo vinavyofanywa na baadhi ya hospitali Binafsi si vizuri na vinaenda kinyume na maadili ya utoji wa huduma za Afya hali inayoweza kurudisha nyuma maendeleo ya serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii.
Ametoa tahadhari kwa wananchi kuwa waangalifu wanapokwenda hospitali hizo kuwa na kuacha mara moja kutumia hospitali ambazo zina kasoro za utoaji huduma za afya.
Alifahamisha bodi inazifanyia ukaguzi wa mara kwa mara hospitali hizo ili kuhakikisha zinafanya marekebisho ya kasoro walizonazo na iwapo watakaidi bodi haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuzifungia moja kwa moja.
Alisema serikali imekuwa ikichukua juhudi kadhaa katika kuhakikisha hospitali binafsi zinatoa huduma zenye ubora kwa wananchi kwani zinasaidia sana katika kupunguza misongamano kwenye hospitali za serikali.
Categories: