Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mawakili Wataka Kesi ya Mv Spice Kupelekwa Mahakama Kuu Malumbano ya sheria yatawala mahakamani

-
Rehema Mwinyi.

UPANDE wa utetezi unaoisimamia kesi ya washitakiwa wa kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders, imemshauri Kaimu Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Essaya Kayange, kuihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu ili maamuzi ya kisheria yaweze kupatikana.

Upande huo wa utetezi ulidai kuwa, katika kesi hiyo kuna baadhi ya mambo ya msingi ambayo mahakama hiyo haina uwezo wa kuyatoa kwa mujibu wa sheria, badala yake lazima yatolewe na Mahakama Kuu.

Hayo yameelezwa na wakili wa kujitegemea Masumbuko Lamwai, mbele ya Kaimu Mrajis huyo wakati kesi hiyo inayowakabili watuhumiwa 11 akiwemo Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, kufikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.


Watuhumiwa hao ni Said Abdallah Kinyanyite, Abdallah Mohammed Ali, Yussuf Suleiman Issa (Kassu), Simai Nyange Simai, Haji Vuai Ussi, Abdallah Mohammed Abdallah, Juma Seif Juma, Hassan Mussa Mwinyi, Salim Said Mohammed Battashy, Mohammed Hasnuu Makame pamoja na Jaku Hashim Ayoub.

Lamwai alisema kuwa, kuna mambo mengi yanahitajika kuzungumzwa katika kesi hiyo, lakini inashindikana kutokana na uwezo ulionao mahakama hiyo ambayo haitaweza kuyatolea maamuzi.

Alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria kesi hiyo ilikuwa ifikishwe Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na sio Mrajis wa mahakama, na kama suala ni mahakama tu basi ilikuwa isikilizwe na mahakama ya mkoa.

Kwa upande mwengine akiungana na hoja za wakili Hamid Mbwezelani juu ya suala zima la kutokamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo wakili Lamwai alisema kuwa hoja hizo hazina msingi mahakamani hapo.

Alidai kuwa Tume ya Uchunguzi iliyofanya uchunguzi wake ilikuwa na Jaji wa Mahakama Kuu pamoja na Mwendesha Mashitaka wa serikali, ambao wao ndio wanaowashuku watuhumiwa wa kesi hiyo, lakini Mwendesha Mashitaka huyo huyo anadai kuwa upelelezi wake bado haujamilika.

“Mheshimiwa kesi hii haikuletwa mahakamani kwa misingi ya kisiasa ya kuwapoza wananchi waliofikwa na maafa, bali imekuja kwa misingi ya kisheria, na kama ipo kwa misingi ya kisiasa basi haipaswi kuwepo hapa”, alisema Lamwai.

Alisema kuwa, kimsingi upelelezi wake tayari umeshafanywa na Tume hiyo, na pendekezo lake linaheshimika kwa ushahidi wao na hakuna wa chini yake akatoa hoja zake za kupingana na hizo.

Alisema kuwa, suala hilo la kutokamilika kwa upelelezi ni sawa na kuwatia hatiani watuhumiwa hao kabla ya kutiwa hatiani na mahakama.

Mapema wakili Hamid Mbwezeleni aliiambia mahakama hiyo kwa kudai kuwa wanashindwa kuelewa ni uchunguzi gani unaofanywa juu ya kesi hiyo wakati ripoti yake tayari imeshatolewa.

“Sizushi kama uchunguzi umefanywa na ripoti yake kutolewa na miongoni mwa wachunguzi ni Jaji Mkuu na kuamua watuhumiwa wafikishwe mahakamani, kwani hawakuwa na shaka kwa tuhuma walizokuwa nazo ndiyo maana wakaamua kuwaleta mahakamani”, alisema wakili Mbwezeleni.

Hivyo alisema kuwa suala la kutokamilika kwa upelelezi halina mashiko, na kuiomba mahakama hiyo ilikatae ombi lao hilo na kama kuna ulazima wa kukubaliwa, basi watuhumiwa hao waondolewe udhia wa kwenda na kurudi mahakamani, hadi watakapokamilisha upelelezi wao.

Akijibu hoja hizo, Mwendesha Mashitaka wa kesi hiyo Mohammed Khamis, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, alisema kuwa suala la uchunguzi uliofanywa na Tume hauhusiani kabisa na upelelezi wa upande wa mashitaka.

Alifahamisha kuwa, Tume iliyoundwa kutafuta chanzo cha ajali imetoa mapendekezo mengi ya kisheria na ya kiutendaji na si lazima yafuatwe, na kwa msingi huo mapendekezo yote hayo jukumu la kuamua nani ashitakiwe na nani asishitakiwe lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.

Aidha alisema kuwa, ijapokuwa Mwendesha Mashitaka wa serikali alikuwemo katika Tume hiyo, lakini uwepo wake huo hauhusiani kabisa na utendaji wake huo bali alikuwa ni Katibu wa Tume hiyo.

“Tume imetoa maoni yake na Ofisi imetimiza wajibu wake, sisi tunajenga upelelezi ambao utaishawishi mahakama na si kufuata maoni ya Tume ni vitu viwili tofauti visivyoingiliana kiutendaji, na mahakama inafahamu hilo”, alisema Mwanasheria huyo wa serikali.

Baada ya hoja za pande mbili hizo, hakimu Essaya Kayange ambaye pia ni hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 7 mwaka huu kwa maamuzi.
Mbali ya mawakili hao upande wa utetezi pia ulikuwa ukisimamiwa na wakili Abdallah Juma pamoja na Kepteni Bendera.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa wote hao wanakabiliwa na mashitaka ya uzembe na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hali iliyosababisha kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders na kuua watu 203, Septemba 10 mwaka jana.

Leave a Reply