Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Zanzibar Yajinyakulia Tuzo ya Utalii Nchini Russia

-
Rehema Mwinyi.


ZANZIBAR imefanikiwa kuwa mshindi wa kwanza na kujinyakulia tuzo ya Utalii nchini Russia kwa mwaka 2011, ‘Star Travel.ru 2011’.
Tuzo hiyo hushindaniwa kila mwaka kwa maeneo yalio bora zaidi kwa shughuli za kiutalii barani Afrika, ambapo watalii na waongoza watalii wa nchi hiyo hutembelea.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ali Khalil Mirza, amesema amepokea taarifa hiyo kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Russia, ikielezea Zanzibar kuchaguliwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, kama eneo lililo bora kwa shughuli za kiutalii barani Afrika.

Alisema kuwa kinyang’anyiro hicho kilihusisha maeneo 23 yalio bora zaidi kwa shughuli za kiutalii, ispokuwa nchi ya Misri haikushirikishwa.
Alisema tayari tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo tangu juzi katika hafla maalum ilioambatana na kuanza kwa maonyesho ya Kimataifa ya Utalii nchini.
Mirza alisema ushindi wa tuzo huyo unatokana na msukumo mkubwa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Russia pamoja na hatua ya Kamisheni hiyo kufanya ziara maalum ya kuutangaza utalii wa Zanzibar mnamo 2009.
Alisema makubaliano yaliofikiwa kati ya Kamisheni ya Utalii na Makampuni ya kutembeza watalii yamelifanya soko la Utalii nchini Russsia kuimarika, ambapo wastani wa watalii 300 hufika nchini kila mwaka tangu wakati huo.
Alieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa soko la utalii nchini Russia kwa kuzingatia watalii wanaokuja ni wale wanaotumia zaidi, ambao hufikia katika Hoteli zenye hadhi za juu kama vile Plan Hotel,Lagema,Green of Zanzibar na The Residents.
Aidha alisema Kamisheni yake ina matumaini makubwa kuwa ifikapo 2013 idadi ya wataalii kutoka nchi hiyo itaongezeka, hususan pale Shirika la ndege la Uturuki litakapoanza kufanya safari zake moja kwa moja hadi Zanzibar, ikizingatiwa watalii hao hivi sasa hutumia usafiri wa Shirika la Emirates, na kutembelea kwanza katika Mbuga za wanyama na hatimae kuja Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alivitaja baadhi ya vigezo muhimu vinavyozingatiwa katika kumpata mshindi wa tuzo hiyo, kuwa ni pamoja na hali ya usalama, kufikiwa kwa matarajio ya wageni, vivutio vya utalii ikiwemo michezo mbali mbali (pwani na ufukweni), huduma katika mahoteli pamoja na tamaduni za wenyeji.

Leave a Reply