Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohammed Shein ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzi ya Amali kuhakikisha michezo yote inayoruhusiwa kisheria Zanzibar kuchezwa mashuleni isipokuwa mchezo wa Ngumi (Boxing).
Amesema michezo yote inafaa kuchezwa wala haipunguzi kasi ya mwanafunzi kusoma na kwamba Wizara inapaswa kulisimamia agizo hilo ili Zanzibar iweze kupata vipaji vitakavoiletea nchi Medali za mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Rais Shein ameyasema hayo alipokuwa akizindua Mradi wa “Mpira Mmoja” “One World Football ball Project for Africa” Wenye lengo la kupambana na Ukatili dhidi ya Watoto kupitia mchezo wa Mpira katika Uwanja wa Aman mjini Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar.
Amesema Mradi huo ambao umewalenga zaidi Wanafunzi wa Shule umefufua matumaini mapya ya kuibua vipaji vya michezo mbalimbali Zanzibar na kwamba kinachohitajika kwa sasa ni mipangilio mizuri kutoka kwa Walimu na wasimamizi wa michezo mashuleni.
Aidha amesisitiza kuwa michezo haimzuii mwanafunzi kufanya vizuri darasani hivyo Wazazi na walezi waendelee kutoa mashirikiano kwa watoto wao kuhusu michezo stahiki wanayoipenda.
“Jukumu lenu Wizara ya Elimu ni kuhakikisha kuwa Michezo yote ile iliyoruhusiwa kisheria chini ya Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo kuwa inachezwa Mashuleni..Wala michezo haimzuii mwanafunzi kufanya vyema Darasani ” Alisema Rais Shein.
Rais Shein alifahamisha kuwa mradi huo pia utasaidia sana kujenga kikosi imara cha Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa vile vipaji vya Soka vitaibuka vingi mashuleni vitakavyosaidia Timu hiyo kuwa tishio Afrika Mashariki na Kati.
Akigusia suala la Zanzibar Heroes na ushindi wa nafasi ya tatu uliyoipata katika Mashindano ya SECAFA Rais Shein amesema timu hiyo ilicheza vizuri kiasi cha kumvutia sana na kuongeza kuwa Zawadi yao ipo kinachohitajika ni kumalizwa tofauti baina ya Wachezaji na Viongozi wa Timu hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Habari na Utamaduni Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema Mradi huo umelenga kuleta vuguvugu la michezo na kuondoa tatizo la vifaa vya michezo Zanzibar ili kuibua vipaji vitakavyoifanya Zanzibar iwe tishio katika michezo mbalimbali.
Aidha ameongeza kuwa Mipira hiyo itagaiwa katika maeneo yote ya Unguja na Pemba bila ya upendeleo na kwamba Timu zote zilizosajiliwa na Makundi maalum watanufaika na mipira hiyo.
Mradi huo ambao umefadhiliwa na One World Futbal,Shirika la Kusaidia Watoto Duniani kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar unajumuisha Mipira-Elfu 20, itakayogaiwa kwa Wanafunzi wa shule na Timu za Soka za Unguja na Pemba.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR