Bodi ya Utalii Tanzania inapenda kuwaarifu wananchi na umma kwa ujumla kuwa Tanzania itakuwa ni
miongoni mwa nchi ambazo angalau moja ya vivutio vyake kitaingia katika orodha ya Maajabu Saba ya Asili
Barani Afrika baada ya kukamilika kwa upigaji wa kura katika shindano la kutafuta Maajabu Saba ya Asili
Barani Afrika Desemba31, 2012 na Tanzania kuwa miongoni mwa washindi
Kampeni ya kutafuta Maajabu Saba ya Asili ya Bara la Afrika ilikuwa iikiendeshwa na Taasisi ya Seven
Natural Wonders yenye makao yake makuu nchini Marekani tangu mwaka 2008 ambapo upigaji wa kura
ulihusisha Taasisi za Kimataifa ikiwemo taasisi ya uhifadhi asili wa Mazingira (IUNC) na wataalamu wengine
duniani ambao walipiga kura kwa kuzingatia zaidi umuhimu wa asili, upekee na uzuri wa kivutio husika.
Taasisi hiyo ya Seven Natural Wonders imewasiliana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania,
Dr. Aloyce Nzuki na kumfahamisha kuhusu matokeo ya awali na kumthibitishia kuwa Tanzania ni kati ya nchi
zilizoshinda na kwamba vivutio vyake zaidi ya kimoja vitakuwa miongoni mwa Maajabu hayo Saba ya Asili
Barani Afrika. Tanzania itakuwa mwenyeji wa sherehe za tukio la utangazaji wa vivutio vilivyoshinda katika
shindano hili na kwamba itakuwa ni fursa kwa Watanzania na Afrika kwa ujumla kufurahia tukio hilo na
Maajbu yatakayoshinda.
Sherehe za utangazaji wa washindi zitafanyika jijini Arusha katika Hotel ya Mt Meru Februari 11, 2013 ambapo
watu mashuhuri kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika, na wandishi kutoka vyombo vya habari vya Kimataifa
na ndani ya nchi wataalikwa kushiriki katika sherehe hizo na kushuhudia utangazaji wa vivutio vya Tanzania na
vingine vya Afrika kuwa Maajabu Saba ya Asili Barani Afrika.
Bodi ya Utalii Tanzania inapenda kuwashukuru watu wote ndani na nje ya Tanzania walioshiriki katika kupigia
kura vivutio vya Tanzania. Vivutio vya Tanzania vilivyokuwa katika shindano hili ni Mlima Kilimnajaro,
Bonde la Ngorongoro, na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mwendeshaji
Bodi ya Utalii Tanzania
Jengo la IPS ghorofa ya tatu
Mtaa wa Samora/Azikiwe
S.L.P 2485 D’slaam, Tanzania
Categories: