Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

CWT, HakiElimu wasaka chimbuko la kuvuja mitihani

-
Rehema Mwinyi.

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na asasi ya HakiElimu, wamezindua shindano la kufahamu chimbuko la kuvuja kwa mitihani ili kukusanya maoni yatakayosaidia kupata ufumbuzi wa tatizo hilo nchini. Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Idara ya Upatikanaji wa Habari wa HakiElimu, Robert Mihayo alisema lengo la shindano hilo ni kupata mawazo na maoni ya wananchi kujua sababu za kuvuja kwa mitihani nchini na kupata ufumbuzi na kuhimiza wananchi kuboresha elimu.

Alisema taifa linahitaji elimu iliyo bora ambayo siyo tu kufaulu mitihani, bali pamoja na kumjengea uwezo mwanafunzi wa kutumia elimu aliyoipata kutatua changamoto anazokumbana nazo katika maisha ya kila siku ambapo mfumo wa elimu nchini sasa umejikita zaidi katika kufaulu.

“Katika shindano hilo litakalowashirikisha Watanzania wote bila kujali umri wala uwezo wa kitaaluma yaani kuanzia wanafunzi hadi maprofesa, linawataka washiriki kutumia kurasa mbili au michoro kuelezea chanzo cha uvujaji wa mitihani, athari zake na nini kifanyike kutatua tatizo hilo,” alisema. Alisema mwisho wa shindano hilo ni Agosti 15, mwaka huu na washindi wawili wa kwanza watapata Sh 500,000 kila mmoja, washindi 10 wanaofuata watapata Sh 200,000 kila mmoja na washindi hao na wengine 50 watakaofuata watapatiwa redio moja kila mmoja zinazotumia umeme wa jua.

Alisema mawazo ya washiriki yatachambuliwa na kutengeneza kitabu kitakachosambazwa nchini ili maoni hayo yawafikie wananchi wengi na kupelekwa serikalini ili watendaji wayafanyie kazi kupata ufumbuzi wa tatizo hilo. Akizindua shindano hilo, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema ingawa serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwamo za kuwafukuza kazi wakuu wa shule zilizohusika, kuwafutia matokeo ya mitihani wanafunzi waliobainika kuiba, lakini uvujaji na wizi umeendelea kutokea mwaka hadi mwaka.


Leave a Reply