Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Wanafunzi 70 Mbagala kutibiwa Muhimbili kutokana na mabomu

-
Rehema Mwinyi.

KARIBU wanafunzi 70 kati ya 1,000 waliobainika kuwa na matatizo mbalimbali yaliyotokana na milipuko ya mabomu iliyotokea Aprili 29 kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Mbagala Kuu, watatibiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwananchi imeelezwa.

Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa watu walioathirika na milipuko hiyo, karibu wanafunzi 900 walibainika kuwa na matatizo na kutibiwa na timu ya madaktari iliyopelekwa eneo hilo baada ya kuripotiwa kuwa watoto wengi walipata matatizo ya kutoona, kutosikia vizuri na maumivu ya kichwa.

Milipuko hiyo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 26 na kujeruhi watu kadhaa huku ikiharibu nyumba za wakazi wengi wa maeneo yanayozunguka kambi hiyo.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zinasema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi waliopewa rufaa hiyo ni wale waliobainika kuwa na matatizo ya kutosikia na kutoona vizuri.

“Wanafunzi sita wamepelekwa Muhimbili kutokana na kugundulika kuwa hawasikii vizuri kutoka na kuathirika na milipuko ya mabomu hayo na madaktari wamesema watoto wengine 20 hawataweza kuona vizuri hadi wapate matibabu zaidi na kupewa miwani,” alisema mwalimu mmoja wa Mbagala Kuu ambaye alikataa kutajwa gazetini.

Katika Shule ya Msingi Maendeleo habari zinasema kuwa wanafunzi 30 wamebainika kuwa na matatizo ya macho huku 14 wakiwa na matatizo ya kutosikia vizuri.

Kwa mujibu wa walimu hao, baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la masikio kuvuma wakati wote, kuwa na nta nzito na macho kuwasha walitibiwa shuleni hapo na kuendelea vizuri.

Baadhi ya walimu wa shule hizo waliliambia gazeti hili jana kwa nyakati tofauti kuwa tangu kutokea milipuko hiyo Aprili 29 mwaka huu, baadhi ya wanafunzi bado hawajafika shule.

Wamesema kuwa miongoni mwa wanafunzi hao ni pamoja na Majaliwa Petro (10) Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Maendeleo ambaye tangu kutokea milipuko hiyo hajafika shule.

Hata hivyo, dada wa Petro, Siwema Petro (13) anayesoma Maendeleo alisema mdogo wake ameathirika kisaikolojia na kuwa wakati wote anataka kukimbia na mara kadhaa anaongea mwenyewe.

“Wakati milipuko inatokea Majaliwa alikuwa shuleni, lakini tunasikia katika harakati za kujiokoa aliona mtu aliyekatwa shingo na bomu, sisi tunadhani ndicho kilichomuathiri zaidi,” alisema Siwema.

Milipuko hiyo pia imefanya miguu ya mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Mbagala Kuu, Quntinea Livingston, 7, kupooza na hivyo kusaidiwa kwa kubebwa.

Margareth Gilbert, 28, mama mzazi wa Livingston alisema mwanaye aliangukiwa na ukuta akiwa katika harakati za kukimbia baada ya kusikia milipuko ya mabomu.

Katika hatua nyingine, meya wa manispaa ya Temeke, Jerome Bwanausi amesema Mbagala sasa iko shwari na anasikitishwa na baadhi ya watu kutoa kauli za uongo na kuwatisha wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya hiyo, Bwanausi alisema taarifa zinazosambaa Mbagala kwamba mabomu yatalipuka wakati wowote ni za uongo.

“Msemaji mkuu wa suala zima la mabomu ni mkuu wa mkoa na mpaka sasa hajatoa taarifa yoyote ya ulipuaji mwingine wa mabomu kwa hiyo eneo hilo ni shwari,” alisema.

Naye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi jana alilazimika kuiongezea muda kamati inayofanya tathimini ya mali na majengo yaliyoteketezwa kwa mabomu hadi Juni 3 mwaka huu.

Lukuvi aliliambia gazeti hili jana kuwa amelazimika kuiongezea kamati hiyo muda baada ya mwenyekiti wake kuomba muda zaidi kwa ajili ya kukamilisha kazi.

“Nilitegemea kupokea taarifa ya kamati hiyo kesho (leo), lakini mwenyekiti wa kamati Cleophace Rweye alifika ofisini kwangu na kuomba muda zaidi wa kufanya kazi hiyo,” alisema Lukuvi.

“Moja ya mambo aliyodai hajayakamilishwa ni uandaaji wa taarifa na kufikisha taarifa yao kwa mtathimini mkuu wa serikali.”

Alisema ili waathirika hao waondokane na shida ya kuishi kwenye mahema hayo, serikali inahitaji kuwalipa fidia zao mapema, hivyo taarifa ya kamati hiyo ndiyo itakayokuwa mwongozo wa malipo.

Baadhi ya wakazi wa Mbagala Kuu jana waliendelea kuilalamikia kamati hiyo kuwa haikufanya tathimini kwenye nyumba zote zilizokumbwa na maafa hayo.

Wakizungumza na Mwananchi katika ofisi za kata hiyo wakazi hao walisema nyumba zao hazijafanyiwa tathimini tangu zoezi hilo lilipoanza.

Swaum Husein, 32, mkazi wa kitongoji cha Mwanamtoti alisema: “Sijafanyiwa tathimini yoyote katika nyumba yangu mpaka leo hii tunatangaziwa kuwa kazi hiyo imefikia ukomo wake.”

Lusian Matius mkazi wa mwanamtoti alisema: “Unavyotuona hapa tumelazimika kumchukuwa mjumbe wetu aje atueleze kwa nini mpaka leo hii nyumba zetu hazijafanyiwa tathimini.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mjumbe wa shina namba moja, Mohamed Likata, 48, alikiri kuwa wakazi hao hawajafanyiwa tathimini na kwamba lina nyumba 34 zinazohitaji.

Leave a Reply