Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Michael Jackson 'hakufanyiwa hila'

-
Rehema Mwinyi.


Madaktari waliochunguza kifo cha mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Pop, Michael Jackson, aliyefariki dunia Alhamisi, wamesema matokeo ya awali hayajaonyesha hila yoyote.

Lakini vipimo vingine vikiwemo vya sumu vimechukuliwa ambapo uchunguzi wake unaweza kuchukua majuma kadhaa, ofisi ya mchunguzi wa vifo vya Los Angeles ilieleza.

Maafisa wamesharuhusu ndugu kuuchukua mwili wa Jackson, lakini bado hakujawa na taarifa zozote kuhusu mazishi yake.

Waombolezaji wakiwemo wasanii wenzake, viongozi wa mataifa mbali mbali na mashabiki wamekuwa wakitoa rambi rambi zao kwa mwanamuziki huyo.

Jackson aliyekufa akiwa na umri wa miaka 50, siku ya kifo chake alikimbizwa hospitalini huko Los Angeles, Marekani, baada ya kupata matatizo yanayodhaniwa kuwa ya moyo.

Taarifa za awali zilieleza kuwa mwanamuziki huyo alikuwa hapumui wakati madaktari wa huduma ya kwanza walipofika kumsaidia nyumbani kwake maeneo ya Bel Air yapata saa sita na nusu majira ya huko. Lakini mwishowe maafisa wakathibitisha kifo chake.

Utata mkubwa uligubika hali ya afya ya mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na albamu mbali mbali kama Thriller.

Wavuti ya TMZ ambayo huandika taarifa za watu mashuhuri katika maswala ya burudani ilikuwa ya kwanza kuandika kuwa Michael Jackson mwenye umri wa miaka 50 alikuwa ameaga dunia.

Vile vile, gazeti maarufu la Los Angeles Times liliandika katika wavuti yake kuwa Michael Jackson amefariki. Lakini vyombo vingine vya habari vilikuwa vikisema alikuwa bado yu hai, ingawa alikuwa mahututi.

Madaktari wa huduma ya kwanza walijaribu kuuzindua moyo wa Jackson wakati gari ya wagonjwa ilipokuwa ikimkimbiza katika hospitali ya UCLA, maafisa wameeleza.

Jackson alikuwa akitarajiwa kuanza matamasha mbali mbali ya kufufua kipaji chake kwenye ukumbi wa O2 jijini London ifikapo tarehe 13 Julai.

Imeelezwa alikuwa na historia ya matatizo ya kiafya na hajawahi kukamilisha ziara ya matamasha kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita.




Leave a Reply