Mtoto wa miaka 14 ndiyo mtu pekee aliyenusurika kwenye ajali ya ndege ya Yemen Airways (Yemenia) ambayo ilidondoka jana kwenye bahari ya hindi ikiwa na jumla ya watu 153. | ||
Waokoaji walisema kwamba msichana mwenye umri wa miaka 14 alikutwa akielea kwenye bahari ya Hindi kilomita 16 kutoka kwenye pwani ya visiwa vya Komoro. Taarifa zilisema kwamba binti huyo aliyejulikana kwa jina lake la kwanza Bahia alikuwa akisafiri pamoja na mama yake. Hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri kwenye hospitali aliyolazwa kwenye visiwa hivyo. "Anaendelea vizuri na aliweza kuongea na mamlaka husika na kuwaelezea kilichotokea" alisema msemaji wa timu ya waokoaji. Taarifa za awali zilisema kwamba msichana huyo alikuwa na umri wa miaka mitano lakini msemaji huyo alikanusha taarifa hizo. Ndege ya Yemen Airways (Yemenia) ilidondoka na kuzama kwenye bahari ya Hindi jana karibu na visiwa vya Komoro wakati ikitokea Ufaransa kuelekea Moroni, mji mkuu wa Komoro kwa kupitia Yemen ikiwa na abiria 153. Watu wengi waliofariki ni raia wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya ulisema ulikuwa na mpango wa kuzipiga marufuku kwenye anga ya ulaya ndege za Yemenia ambazo zimekosolewa sana kwa kuvunja taratibu za usalama. Hii ni ajali ya pili ya ndege ambayo imepoteza maisha ya raia wengi wa Ufaransa ikiwa ni wiki chache baada ya ndege ya Ufaransa, Air France iliyokuwa ikitokea Brazili kuelekea Ufaransa ikiwa na abiria 228 kudondoka kwenye bahari ya Atlantic na kuua watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo. Yemenia kutokana na baadhi ya ndege zake kupigwa marufuku nchini Ufaransa ilikuwa ikitumia ndege zake mpya kwaajili ya nchi za ulaya na ndege zake za zamani kwaajili ya safari zake katika nchi za Afrika na kwingineko ambako hawakupewa masharti ya usalama wa ndege zao. Ndege iliyotoka Ufaransa ilikuwa ni mojawapo ya ndege mpya za Yemenia na ndege hiyo ilipofika Yemen, abiria walibadilisha ndege na kupandishwa ndege hiyo ya zamani iliyokuwa inakuja Afrika ambayo ilipigwa marufuku nchini Ufaransa kutokana na matatizo yake mbali mbali. | ||
| ||
|
Categories: