Ajali hiyo ya kutisha imesababisha vifo vya watu 7 waliokuwa ndani ya basi dogo, baada ya lori hilo kulilalia basi hilo lililokuwa likitokea Kibamba kwenda Ubungo. Akiongea na mwandishi wetu aliyefika eneo tukio, Kamanda Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani, Mohamed Mpinga , alisema kuwa basi hilo dogo aina ya Hiace lilikuwa na abiria saba ambao wote wamefariki dunia, na kati ya maiti hizo, ni maiti mbili tu ndizo zilizoweza kutolewa hadi muda huu tena zikiwa vipandevipande.
Katika maiti hizo zilizotolewa, moja ni ya mwanamke ambae hakuweza kutambuliwa kwa wakati ule na na mwanaume aliyetambuliwa kwa jina la Shukuru Hussein, maarufu kama Kibwetere, mkazi wa Kibamba. Aidha Kamanda Mpinga aliongeza kuwa bado utaratibu unaendelea kwa kuwa lori lilikuwa limejaza mafuta hivyo imeleta ugumu katika utoaji hadi mzigo wote utakapoisha na kuweza kufanya utaratibu wa utoaji.
Kamanda Mpinga aliweza kumtaja dereva wa lori ambaye amekimbia mara baada ya tukio hilo kutokea kuwa ni Kudura Adam na mmiliki wa Lori hilo ametambuliwa kwa jina la Mahamudu Mohamed.
Hata hivyo baada ya ndugu wa mmiliki wa Hiace kupatikana na kudai mwenyewe yuko Mkoani Kilimanjaro, walisema kuwa mmiliki huyo anaitwa Selemani Khalfan na Hiace yake huwa inalala Ubungo Kibo maeneo ya Rombo na kumtaja Dereva wa Hiace hiyo kwa jina moja kuwa ni Seif na Kondakta wake Faraji Ismail Kalama ambao mpaka sasa bado maiti zao hazijatolewa eneo la ajali.
SOURCE:GLOBAL PUBLISHERS.