Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

MAALIM SEIF AIOMBA KOREA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA.

-
Rehema Mwinyi.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiomba serikali ya watu wa Korea Kusini, kuangalia uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika sekta za Elimu na Kilimo ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi vijana.

Maalim Seif, alitoa ombi hilo huko Ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini nchini, Kim Young Hoon, ambapo pamoja na mambo mengine walizungungumzia haja ya kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.

Makamu huyo alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoendelea, inakabiliwa na changamoto nyingi za kimaendeleo, ikiwemo kuwajengea uwezo wa kielimu vijana wake ili waweze kujiajiri pamoja na kuimarisha sekta ya kilimo.

Alisema Serikali ya Zanzibar imeunda Wizara maalum ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, kwa lengo la kuwajengea mazingira bora vijana ili waweze kujiajiri kwa kufanya kazi za amali.

Aidha alisema msukumo zaidi unahitajika ili kuinua kiwango cha elimu, kuanzia ngazi za msingi hususan katika fani za kiufundi, hivyo alimuomba Balozi huyo kutoa fursa zaidi za masomo katika nyanja hiyo.

Maalim Seif alifahamisha vijana wa Zanzibar, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ushindani wa ajira katika soko la pamoja na Afrika Mashariki, ambapo vijana wa ukanda huo watakuwa na fursa ya kufanyakazi kutoka nchi yoyote mwanachama.

Aidha Maalim seif alimweleza Balozi huyo kuwa visiwa vya Zanzibar vinahodhi eneo dogo la ardhi, ambapo upatikanaji wa mazao umekuwa sio wa uhakika kwa vie unazingatia zaidi mvua, huku kukiwa na mabadiliko ya hali ya hewa kila mara.

Alimwomba Balozi huyo kuangalia uwezekano wa nchi yake kusaidia uimarishaji wa miundo mbinu ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na pembejeo ikiwemo ‘Power tiller’, sambamba na kutoa fursa zaidi za mafunzo kwa wataalamu wazalendo ili hatimae waweze kueneza taaluma hiyo kwa wakulima.

Katika hatua nyingine Malim Seif alimuomba Balozi huyo kuangalia uwezekano wa Shirika la Ndege la nchi yake kufanya safari za moja kwa moja hadi Zanzibar, ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza utalii.

Alisema Serikali ya Zanzibar inaendelea na jitihada za kuimarisha miundo mbinu ya mawasiliano ikiwemo uimarishaji wa kiwanja chake cha Ndege kwa lengo la kukuza sekta hiyo muhimu inayochangia asilimia kubwa ya pato la taifa.

Nae Balozi Kim, alimuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais, kuwa Korea itaendeleza ushirikiano wake wa muda mrefu na Zanzibar kwa kuongeza fursa za masomo kwa Wazanzibari ili kuwajengea uwezo vijana pamoja na kutuma Wataalamu wa kujitolea kushirikiana na wazalendo katika miradi mbali mbali.

Alisema vijana wa Zanzibar wanaweza kufaidika zaidi kutokana na fursa za mafunzo kwa kutafuta taarifa sahihi kupitia mtandao wao wa  Koika.

Aidha aliiomba serikali kuangalia kwa karibu zaidi usalama wa wataalamu wake wa kujitolea pale wanapokuwa nchini katika shughuli za kazi katika maeneo ya vijijini.

Leave a Reply