Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Buriani Bi Rahma Mshangama

-
Rehema Mwinyi.


Leo baada ya Salat ya  IJumaa, maiti ya Maremu Bi Rahma Mshangama ilisaliwa katika msikiti wa Ijumaa Mwembeshauri, mjini Unguja na baada ya hapo ilienda kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwereke nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Bi Rahma Mshangama alifariki jana katika hospitali ya MnaziMmoja mjini Zanzibar, Marehehemu Bi Ramha alizaliwa tarehe 21 Aprili 1961 Kikwajuni Mjini Zanzibar na kupata elimu yake ya msingi mwaka 1969 mpaka 1978 katika skuli ya msingi na Sekondari ya Kidutani na Lumumba Zanzibar.

Mnamo mwaka 1979 mpaka 1981 alipata elimu ya Juu katika Chuo Cha Lumumba ambapo katika mwaka huo wa 1981 aliajiriwa katika Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.

Mwaka 1985 mpaka 1987 alipata elimu ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Mkoani Morogoro ambapo mwaka 1991 alihudhuria mafunzo ya Utafiti wa Masuala ya Elimu na Ufugaji katika Chuo Cha Mifugo Afrika nchini Ethiopia.

Mwaka 1989-1990 alihudhuria mafunzo ya (MSC) Uzalishaji wa wanyama katika Chuo cha Reding University nchini Uingereza na mwaka 1991 alihudhuria mafunzo ya Ukuzaji Kilimo pamoja na Mafunzo ya Maendeleo ya Wanawake katika Kilimo nchini Uingereza na mwaka 1996 alihudhuria mafunzo ya Ubinafsishaji nchini Ireland.

Katika uhai wake Marehemu Bi Rahma Mshangama aliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Posta kuanzia mwaka 1996, na pia alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Uzalishaji wa wanyama nchini Tanzania kuanzia mwaka 1989 mpaka alipofariki.

Kwa upande wa nafasi alizowahi kushika Marehemu Bi Rahma Mshangama aliwahi kuwa Mkuu wa Idara ya Mifugo katika kitengo cha Mifugo mnamo mwaka 1987-1989, mwaka 1991 hadi 1992 alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Kamisheni ya Mashamba ya Serikali katika Wizara ya Kilimo na Mifugo.

Mwaka 1992 hadi mwaka 1995 alikwua msaididi wa Meneja wa Mradi wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar na mwaka 1995 hadi mwaka 2000 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Wanawake na Watoto na mwaka 2000 hadi 2008 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Maliasili na Ushirika na mwaka 2008 hadi 2010 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto.

Hadi anafariki Bi Rahma Mshangama alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto. Bi Rahma Mshangama ameacha mume na Mama Mzazi.

Mapema katika hotuba ya Sala ya Ijumaa, akieleza sifa za Marehemu Bi Rahma Mshangama, Sheikh Fadhil Soraga alisema kuwa Bi Ramha Mshangama atakumbukwa daima kutokana na alikuwa mchapa kazi hodari na aliishi na jamii kwa wema mkubwa na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu amuweke mahala pema peponi, Amin

Leave a Reply