Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Kashfa ya Kuvuja Mitihani - Mtihani Mwengine

-
Rehema Mwinyi.


MAMIA ya vijana wa Zanzibar waliofanya mtihani wa kidato cha nne wanakabiliwa na mtihani mwingine, tena ni mkubwa zaidi kuliko ule walioufanya mwaka jana na hawajui waukabili vipi huu mtihani mpya.

Matokeo yao ya mtihani wa kidato cha nne yamefutwa na kuambiwa juhudi zao zote za kujitayarisha kwa miezi kadha zimekwenda na maji, yaani “Ajwar” (pata potea).

Hivi sasa watoto hawa, wengi wao wakiwa wanatokana na familia za kimasikini, wamebaki wakilalama huku wakiwa na huzuni na hivi sasa wanahangaika huku na kule kama kuku anayetaka kutaga na hakuna dalili za kupata mafanikio.


Watoto hawa wa kimasikini wanaona dunia imewapa mgongo na huko wanakokwenda ni kiza kitupu na hakuna mtu wa kuwaashia taa ya kuona kilipo usoni. Ni unyonge mkubwa.

Ama kweli Waswahili hawakukosea waliposema mnyonge hana haki, lakini tukumbuke walipotutahadharisha kwa kusema; ‘Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni”.

Kwa kweli inasikitisha sana, inahuzunisha na inatisha kuona viongozi wetu wengi wanaliona suala la kufutwa matokeo ya mtihani kama vile ni jambo la kawaida na hawataki kukubali madhara yake kwa vijana wetu waliofutiwa matokeo ya mitihani.

Sishangai hata kidogo na mtazamo wao huu kwa sababu watoto wa hawa wakubwa ambao tumekuwa tukidhani na wengi kuamini watatuonea imani na kuwahurumia watoto wa kimasikini wanasoma nje ya nchi. Matatizo ya elimu tuliyonayo nchini, hayawahusu.

Ukifanya utafiti wa haraka utaona kuwa watoto wa karibu viongozi wote wa serikali na matajiri hawawapeleki watoto wao katika shule za serikali kwa sababu wanaelewa vizuri kwamba huko hakuna elimu ila kupoteza wakati.

Kwanza kuna msongamanao ndani ya madarasa, walimu ni wa kuokoteza na wanafunzi wanatumia muda mwingi kupokea wageni au kutakiwa kwenda kwenye sherehe za kitaifa zisizokwisha.

Baaadhi ya viongozi wa serikali na matajiri, bila ya aibu, wamewapeleka watoto wao katika shule zilizodhaminiwa na washirika wa maendeleo wa nchi za nje kusaidia watoto yatima.

Hii leo ukienda shule ya yatima ya OSS ya Zanzibar utashangaa na kushitushwa kuona zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi si yatima bali ni watoto wa viongozi na wafanyabiashara wakubwa wa nchi hii.

Hii ni aibu na ni dhambi, lakini wenye fedha na vyeo mara nyingi huwa hawajali kwa vile wanaongozwa na jeuri na kibri na si utu na ubinaadamu, imani wema au hisani. Watu hawa hawaoni kuwa wanavyofanya ni vibaya.

Wakati sasa umefika kwa serikali kulitupia macho suala hili kwa kuonyesha imani na huruma kwa watoto wa kimasikini.

Huu mchezo wa kuchezea mitihani na hatimaaye kuathiri zaidi watoto wa kimaskini ni wa hatari na hauna mwisho mwema.

Hivi sasa katika kila pembe ya Unguja na Pemba wazazi na watoto wao wanasikitika na wengine kulia kutokana na kufutwa kwa matokeo ya mithani wa kidato cha nne kwa mamia ya watoto wa kimaskini.

Ukweli ni kwamba Baraza la Mitihani Tanzania limeshindwa kazi yake na wizara zetu za elimu, Bara na visiwani zimeshindwa kuwajibika katika kuhakikisha mitihani haivuji.

Matokeo yake ni kwamba watoto wa kimasikini na wazee wao walioweka matumaini kwamba elimu ingewasaidia kutokana na umaskini (ukweli ni ufukara) na unyonge wa maisha ndio wanaoumia na kuteseka.

Hapa tujiulize ni nani wa kulaumiwa kwa kuvuja mitihani? Ni hawa wanafunzi au kutokuwepo uadilifu na ulinzi wa kutosha hata mitihani ikavuja?

Kilichojitokeza hapa ni kwamba wanaostahiki kulaumiwa na kubeba dhamana ni Baraza la Mitihani kwani ni dhahiri kuwa kazi imewashinda na kwa vile imedhihirika wazi kuwa hawawezi kusimamia mitihani kinachotakiwa ni kujiuzulu.

Lakini lililo muhimu zaidi ni kwa wahusika kuwajibishwa kikazi na kisheria na si kuwaadhibu watoto wa kimaskini.

Hapa nataka nikumbushe kwamba zama za ukoloni nilipokuwa ninafanya mitihani ya darasa la nane na baadaye kidato cha nne hizi habari za kuvuja mitihani na udanganyifu zilikuwa hazisikiki.

Kama wakoloni waliweza kudhibiti mitihani isivuje miaka ile nini kinachopelekea leo kuvuja kwa mitihani iwe jambo la kawaida kama si kutokuwapo uadilifu na kushamiri kwa uhuni?

Tujiulize kulikoni hii leo? Jawabu unayoipata na ambayo ni sahihi kwa mapana na marefu ni kutokuwepo uongozi mzuri katika kusimamia mitihani na uhuni kutawala mwenendo mzima wa kuendesha shughuli za serikali.

Hii ni aibu na fedheha, tena kubwa na wahusika hawastahili kuvumiliwa wala kuonewa huruma. Kama wao hawahurumii watoto wa kimasikini hapana sababu kwa jamii kuwaonea huruma.

Lakini ukichunguza utaona waliohusika na uvujaji wa mitihani wamepoa na hawana wasiwasi kwa vile wana uhakika wa kulindwa kwa sababu za kisiasa.

Si ajabu hivi sasa waliohusika na kuvujisha mitihani wakawa wanapanga namna bora ya kuvujisha mitihani ya mwaka huu ili kujipatia fedha za bure kwa kuwa wanaelewa na kujiamini kuwa hawatawajibishwa kikazi wala kisheria. Kwa watu hawa kuvujisha mitihani ni sehemu ya kazi yao.

Hali hii ni ya hatari na inatisha. Serikali inapaswa kuelewa kwamba uhuni wa kuvujisha mitihani na baadaye kufuta matokeo ya shule kadhaa unawaumiza na kuwadhulumu watoto wa kimasikini ambao walitegemea elimu hapo baadaye ingewakomboa na maisha duni wanayokabiliana nayo hivi sasa.

Katika nchi nyingi zinazoheshimu utawala bora na demokrasia (tofauti na ilivyo Tanzania) panapotokea aibu kama hii ya kuvuja mitihani hatua ya kwanza inayofuata ni kwa viongozi wa juu wa Wizara ya Elimu (Bara na Visiwani) na wale wa Baraza la Mitihani kuachia ngazi kwa vile kazi waliopewa imewashinda.

Lakini huu utamaduni mchafu na unaonuka tulionao wa kulindana kwa maovu tunayoyatenda au kuruhusu wasaidizi wetu kufanya uhuni na wasiwajibishwe utaendelea kutuponza na gharama zake ni kubwa.

Mpaka pale tutapoanza kutoa umuhimu kwa uwajibikaji hizi hadithi za kuvuja mitihani kila mwaka zitaendelea na matokeo yake ni kuendelea kuwaumiza watoto wa kimasikini zitaendea tena kwa kasi zaidi.

Wahusika na uvujaji wa mitihani watasema Tumethubutu na tunaweza na tutaendelea”.

Ni vizuri kama hatuwezi kuwasaidia watoto wa kimaskini tuache kufanya maovu yanayosababisha kuwakandamiza.

Leo mambo haya yananyamaziwa na hapa na pale ndiyo hupigiwa kelele, lakini tukumbuke kama leo suala hili halitazusha balaa historia hapo baadaye itatuhukumu kwa kuwadhulumu watoto wa kimaskini.

Suala la mitihani ni mtihani, lakini maisha ni kupambana na mitihani. Ni vema tukapambana na mtihani huu bila ya woga au kulindana bila ya sababu za msingi

Chanzo: Tanzania Daima

Leave a Reply