Wananchi wakishirika katika mazishi ya Mnikulu wa Ikulu ya Zanzibar Shaban Ahmada Hilika, katika kijiji cha Vuga Mkadinim Unguja.
Shekh.Talib Suleiman, akisoma dua baada ya kumaliza kuzika katika makaburi ya Vuga Mkadini Unguja.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Hassan Khatib, akisoma risala ya Marehemu Shaban Ahmada Hilika wasifu wake wa kazi wakati wa uhai wake alivyokuwa akishirikiana na Wafanyakazi wa ngazi zote na kutowa msaada pale kunapokuwa na matatizo kwa wafanyakazi wake.
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, leo ameongoza mazishi ya marehemu Shaaban Ahmada Hilika, aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Rais (MNIKULU), katika Afisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Mazishi ya marehemu Hilika yalifanyika huko kijijini kwao Mfenesini Vuga Mkadini, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo viongozi mbali mbali, wananchi na wanafamilia walihudhuria akiwemo Bwana Shaaban Gurumo MNIKULU kutoka Afisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliehudhuria akiiwakilisha afisi yake.
Baada ya kusaliwa katika msikiti wa Amaani, Mjini Unguja ambapo pia, Rais mstaafu wa Zanzibar Alhaj Dk. Amani Abeid Karume alihudhuria, mwili wa marehemu ulipelekwa huko kijijini kwao Mfenesini Vuga Mkadini kwa ajili ya mazishi mnamo majira ya saa saba za mchana.
Marehemu Shaaban Ahmada Hilika alifariki dunia jana tarehe 30/3/2012 huko katika hospitali Kuu ya MnaziMmoja.
Marehemu Hilika alizaliwa mwaka 1965 katika kijiji cha Mfenesini Vuga Mkadini na kupata elimu yake ya msingi katika skuli ya Kidutani Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi na kumaliza mwaka 1979.
Alimaliza elimu ya Sekondari katika Skuli ya Sekondari ya Vikokotoni mnamo mwaka 1983 ambapo pia, alijiendeleza kielimu na kufanya mitihani ya masomo ya Sekondatri ya Juu katika Skuli ya Lumumba mwaka 1999.
Mwa upande wa Elimu ya Kazi, marehemu Hilika alisoma masomo ya huduma za chakula na vinywaji katika vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi kwa mafunzo ya muda mfupi.
Marehemu alipata nafasi ya kujiunga na masomo ya Stashahada ya Juu katika fani ya Uongozi na Usimamizi wa Biashara katika Chuo cha Hoteli na Biashara kilichopo Dar es Salaam.
Utumishi wa umma wa marehemu ulianza rasmi mwezi Aprili, 1985, alipoajiriwa katika Chuo cha Hoteli na Utalii kama mwalimu wa Chuo hicho kabla ya kuhamishiwa kwenye hoteli ya Bwawani mwaka 1990.
Wakati akiwa katika hoteli ya Bwawani, marehemu aliwahi kushika nafasi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Hoteli hiyo kuanzia mwaka 1998-2001.
Mwaka 2001 marehemu alihamishiwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapainduzi kushika nafasi ya Mnikulu, nafasi ambayo marehemu alidumu nayo hadi kufa kwake.
Akisoma Risala fupi katika mazishi ya marehemu Hilika, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Hassan Khatibu, alisema kuwa marehemu katika utumishi wake wa umma alikuwa mchapa kazi hodari mwenye mashirikiano makubwa na wenzake ambapo pia alikuwa na uwezo wa kutatua matatizo kwa haraka na njia za hekima na busara.
Alieleza kuwa marehemu hakuwa na ubaguzi juu ya usimamizi wa kazi na utoaji wa haki kwa wafanyakazi na alikuwa msikivu na alikubali ushauri kutoka kwa wafanyakazi wenzake wa ngazi zote.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa marehemu Hilika ameondoka wakati ambapo Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inamhitajia kuliko wakati mwengine wowote, na ameacha pengo kubwa katika afisi hiyo.
Marehemu ameacha kizuka mmoja na watoto watatu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi-Amin.