WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad, amesema haoni sababu ya kujiuzulu nafasi yake, kufuatia janga la kuzama kwa meli ya MV.Skagit iliyopoteza maisha ya zaidi ya watu 60.
Waziri huyo alieleza hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari alipokuwa akielezea kadhia ya ajali hiyo, ambapo katika mkutano huo waziri wa Uchukuzi wa Tanzania bara Harrison Mwakyembe na Naibu wake Lazaro Nyalandu nao walihudhuria.
Waziri Masoud alisema meli hiyo ilizama kutokana na janga la kimaumbile, kufuatia upepo mkali uliosababisha mawimbi na hatimaye kuzama kwa boti hiyo.
Alisema haoni sababu ya msingi ya kujiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli hiyo licha ya kutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzama kwa meli ya MV. Spice Islander.
Alikiri kuwepo kwa maoni ya watu kumtaka ajiuzulu na kuwaeleza watu wa aina hiyo kuwa hakuna mtu anayeweza kuzuia majanga ya kimaumbile kama upepo yasitokezee.
"Kumekuwa na watu wanaotoa maoni juu ya suala la kujiuzulu, lakini bado hakuna mtu anayeweza kuzuiya upepo usitokee kwani hauko katika mamlaka yake",alisema waziri huyo.
"Kuna wengine wanasema tumemkosa kule sasa watanipatia kwa hili, nimeshapata taarifa kuwa kuna ‘private member’ watapeleka hoja katika Baraza la Wawakilishi ya kujiuzulu, nimeshasikia na wimbo huu unaimbwa tena na natumiwa meseji kuulizwa nitajiuzulu wakifa wangapi kwani mimi napenda kuua", alisema.
Waziri Masoud alisema kutokana na ajali hiyo haitakuwa busara kuona kwa wakati huu kuanza kuzungumzia suala hilo na badala yake waendelee kushirikiana na serikali yao kuona wanaiunga mkono katika kusaaidia maafa hayo.
Akizungumzia juu ya watalii waliopatwa katika ajali hiyo alisema ni 15, ambao wanatoka nchini Ubelgiji, Israel, Uingereza na Marekani ambapo hali zao zipo vizuri baada ya serikali kuwapatia misaada mbali mbali na inatarajia kufanya utaratibu wa kuwarejesha nyumbani kwao.
KAULI YA BALOZI SEIF
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesikitishwa na tukio la pili la kuzama kwa meli ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Balozi Seif alisema tukio la kuzama Mv.Skagit limeiweka serikali ya Mapinduzi ya Zanzibra yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa kwenye wakati mgumu kwani baada ya kuzama MV. Spice Islander I, ilijipanga kuhakikisha tukio lile halijirejei.
Alisema ni jambo la kushangaza sana, kujitokeza tukio la kuzama kwa meli likifanana na kama lile la mwaka jana, ambapo mikakati ya kuhakikisha halijitokezi iliwekwa.
Balozi Seif alisema kujitokeza tena kwa tukio hilo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kunaifanya serikali kuonekana haiko makini katika kusimamia mambo yake.
Balozi alisema hivi sasa serikali inafanya juhudi za kuhakikisha inafanikiwa kukamilisha uokozi ambapo kwa mujibu ya idadi ya waliokuwemo katika meli hiyo walikuwemo watu 290 ambapo watu 146 waliokolewa wakiwa hai pamoja na maiti 67, huku 77 ikiwa bado hawajapatikana.
WABUNGE
Wabunge wa Bunge la Tanzania walifanya ziara maalum kuwatembelea majeruhi wa ajali ya Mv.Skagit katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la Maisara ambapo miili inayoopolewa hufikishwa katika eneo hilo kwa kutambuliwa na jamaa zake.
Katika hospitali ya mnazi mmoja Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa jimbo la Chambani, Salum Hemed, waliwafariji wajeruhiwa waliokua wamelazwa katika wodi maalum iliyotengwa kwa ajili yao huku wakipatiwa matibabu.
WAZAMIAJI WAANZA KAZI
Mamlaka ya Usafiri wa Bahari (ZMA), imesema kuwa wataalamu sita wa uzamiaji kutoka mataifa ya Afrika Kusini na Israel wameanza kuisaka meli ya Mv. Skagit iliyozama Jumatano iliyopita karibu na kisiwa cha Chumbe.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Abdullah Kombo, alilithibitishia Zanzibar Leo kuwa wataalamu hao jaa wameanza kazi ya kuzamia chini ya kina cha baharini kuisaka meli.
Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali zilizotolewa na wataalamu hao zinaeleza kuwa Mv. Skagit ipo chini ya bahari umbali wa mita 28.
"Wazamiaji wamefika katika eneo meli ilipo zama na wamebaini meli hiyo ipo chini umbali wa mita 28, muelekeao wa digirii 06`26.23 kusini na digirii 039` 10.40. mashariki",alisema Kaimu huyo.
Alifahamisha kuwa watalaamu hao wa uzamiaji baharini ambao wamepiga kambi Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, wameamua kufanyakazi ya ujasiri kama njia ya msaada na kwamba wamekuwa wakishirikina na vikosi vya Tanzania katika kazi hiyo.
Miongoni mwa vikosi wanavyoshirikiana nanyo ni pamoja na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kikosi cha Majini cha Jeshi (NAVY) na wazamiaji wengine wa kienyeji.
CHANZO CHA AJALI
Kaimu huyo alisema chanzo cha kuzama kwa MV. Skagit kimetokana na hali mbaya ya hewa wakati kikianza safari yake kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea bandari ya Malindi iliyopo Zanzibar.
Alisema wakati chombo hicho kikikaribia kisiwa cha Chumbe, kulikumbana na mawimbi makali yaliyotokana na dhoruba iliyotoka upande wa kusini.
Kombo aliwataka wananchi kutofautisha mazingira yaliyosababisha kuzama kwa MV. Spice Islander na tukio la kuzama kwa MV. Skagit ambapo tukio la juzi lilisababishwa na hali mbaya ya hewa iliyotokana na kuchafuka kwa bahari.
Kaimu huyo alisema kwa mara ya mwisho MV.Skagit ilifanyiwa ukaguzi (survey), mwishoni mwaka uliopita na kwamba kiliridhisha na kupewa idhini ya kusafirisha abiria na mizigo.
Akizungumzia juu ya tuhuma za marekebisho ya uundwaji wa meli hiyo, alisema hawezi kueleza jambo lolote kwani harakati zote za usajili wa meli hiyo zilikuwazimeshafanyika awali kabla ya kukaimu nafasi hiyo.
"Mimi naingia taratibu hizo zimeshafanyika hivyo siwezi kuthibitisha hilo", alisema Kombo.
MISAADA YAANZA KUTOLEWA
Kufuatia kuzama kwa mei hiyo misaada ya pole imeanza kutolewa ambapo jana Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kila mfuko uliwasilisha shilingi milioni 10 kama ubani kwa wafiwa na majeruhi.
Misaada hiyo alikabidhiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika ofisi yake ndogo iliyopo katika jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Balozi aliishukuru mifuko hiyo kwa misaada yao hiyo waliyoitoa na kuwaonea huruma wale waliofikwa na janga hilo.