TAARIFA mpya za uchunguzi wa kifo cha msanii Michael Jackson zimeonyesha matokeo ambayo yanashangaza kwa kiasi kikubwa.
Vyombo mbalimbali vya habari ulimwenguni vimefichua kuwa msanii huyo alikuwa amedhoofika kiasi cha kutisha na kubakia mifupa kutokana na kutokula na kisha kutumia kiasi kikubwa cha vidonge.
Uchunguzi huo umeonyesha kuwa baada ya kifo chake mabaki ya baadhi ya vidonge hivyo yamekutwa tumboni mwake.
Mwili wake, uchunguzi huo umebaini kuwa ulikuwa umedhoofu kiasi kwamba kiuno, mapaja na mabega yake yalikuwa na matundo ya vidonda vingi vya sindano, vinavyodhaniwa kuwa ni vya sindano za kutuliza na kuondoa maumivu ambazo alichomwa mara tatu kutwa, tena kwa miaka mngi.
Pia, amekutwa na makovu mengi yaliyotokana na upasuaji wa mara 13 ailiofanyiwa kwa ajili ya kubadili sura yake.
Wataalam hao wamegundua uchunguzi wa kusikitisha wenye kuonyesha kuwa msanii huyo, Wacko Jacko hali yake ilikuwa imedhoofu wakati mauti yakimkuta wiki iliyopita mjini Los Angeles.
Uchunguzi huo umeonyesha kuwa licha ya kuwa na urefu wa futi tano na inchi 10, lakini msanii huyo alikuwa amepungua uzito na kubakia na kilo chache ambazo hazilingani na urefu wake.
Wataalam hao wanaeleza kuwa alikuwa akila mlo mmoja kutwa, kiasi kwamba wakati akifariki tumbo lake lilikuwa tupu, mabaki ya vidonge vilivyoanza kusagika ambavyo alitumia na sindano ambazo hatimaye zilisababisha moyo wake kusimama. Sampuli zaidi zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kichwani, Wacko Jacko alikuwa amepoteza nywele karibu zote. Mfalme huyo wa pop, uchunguzi umeonyesha kuwa alikuwa akivaa nywele bandia, ambazo wachunguzi hawakuwa na kazi ya kuziondoa kwa ajili ya uchunguzi wao.
Kichwani mwake, upande wa sikio la kushoto, alikuwa na jeraha kubwa ambalo liliacha upara kutokana na ajali ya mwaka 1984 wakati alipoungua moto akipiga picha ya filamu ya tangazo la Kampuni ya Pepso.
Mwili mwake, wachunguzi hao wamebaini kuwa alikuwa amevunjika mbavu kadhaa, ikiaminika kuwa zilitokana na juhudi za kujaribu kuokoa maisha yake baada ya kuzimia. Matundu manne ya sindano yamegundulika karibu na moyo wa msanii huyo.
Uchunguzi huo umeonyesha kuwa harakati za kumwokoa ndizo zilizomsababishia madhara hayo yakiwamo ya sindano tatu zilizochomwa na kupenya ukuta wa moyo wake, kumsababisha madhara.
Katika uchunguzi huo, imeonekana kuwa magoti ya Jackson na sehemu ya mbele ya ugoko wake zilikuwa na majeraha kama ilivyokuwa mgongoni mwake.
Daktari wake binafsi, Conrad Murray, ambaye alikuwa karibu na msanii huyo amekamatwa na kuhojiwa huku familia ya msanii huyo ikieleza kuwa inataka uchunguzi zaidi unatakiwa kufanyika.
Dk Murray, ndiye anayeaminika kumpiga sindano msanii huyo kabla ya umauti kumkuta, akiaminika kumpa dawa iitwayo Demerol, jambo ambalo limemwingiza katika mzozo wa kitibabu.
Rafiki wa karibu wa familia, Mchungaji Jesse Jackson alieleza wasiwasi kuhusu chanzo cha kifo cha msanii huyo na kutaka uchunguzi zaidi na mtaalam, Dk Murray ambaye alikodiwa na Kampuni ya AEG Live , ambayo ilikuwa na jukumu la kuandaa matamasha 50 ya msanii huyo, katika ukumbi wa O2 Arena, London mwezi ujao, achunguzwe zaidi.