Binti mmoja wa nchini Pakistan ambaye alitoroka nyumbani kwao na kwenda kuolewa bila ya idhini ya wazazi wake ameuliwa yeye na mumewe kwa kupigwa risasi na ndugu zake ambao walidai wanasafisha aibu iliyowekwa na binti huyo. Ndugu wa binti huyo wakiwa wamevalia unifomu za polisi walivamia nyumba aliyokimbilia binti huyo baada ya kuolewa kisiri na kuwaua watu wote waliokuwemo ndani ya nyumba hiyo.
Polisi wa Pakistan walisema kwamba kundi kubwa la ndugu wa binti huyo walivamia nyumba ambayo binti huyo na mumewe walikuwa wakikaa kwenye kitongoji cha Charsadda, kilichopo kaskazini magharibi mwa Pakistani.
"Kundi hilo lilimchukua bwana harusi na kumtoa nje ya nyumba hiyo kabla ya kumuua kwa kumpiga risasi, wakati baadhi yao wakiingia ndani na kumuua bi harusi, mama na dada wa bwana harusi" alisema afisa wa polisi wa eneo hilo.
"Waliwapiga kwanza kisha wakawaua kwa kuwapiga risasi" alisema afisa huyo.
"Baba wa bwana harusi naye aliuliwa" alisema afisa mwingine wa polisi alipohojiwa na shirika la habari la AFP.
Bi harusi alikuwa na umri wa miaka 19 wakati bwana harusi alikuwa na umri wa miaka 29.
Polisi walisema kwamba binti huyo wa kitongoji cha jirani alikimbia nyumbani kwao na kwenda kuolewa kwenye kitongoji hicho bila ya ruhusa ya wazazi wake.
"Walikuwa wameoana wiki chache tu zilizopita" alisema mjomba wa bwana harusi Misal Khan wakati akihojiwa kwenye eneo la tukio.
Kundi la ndugu wa bi harusi inasemekana liliongozwa na wajomba na binamu zake ambao walifanya mauaji hayo kwa madai ya kusafisha heshima ya ukoo wao.
Polisi walisema kwamba wamewakamata ndugu wa binti huyo na watu walioambatana nao kuwasaidia kufanya mauaji hayo.
Shirika la kutetea haki za binadamu limekuwa likipinga mauji yanayofanywa nchini humo kwa madai ya kulinda heshima ya familia.
Wanawake wanaobakwa au wanaopata mimba kabla ya ndoa wamekuwa wakiuliwa nchini humo kwa madai kwamba wanaitia aibu familia.
Mwaka 2005 rais wa wakati huo wa Pakistan, Pervez Musharaf aliamuru adhabu ya kifo kwa watu watakaofanya mauaji kwa madai ya kurudisha heshima ya familia zao.
Categories: