KESI za mahabusu wa gereza la Keko, jijini Dar es Salaam, waliogoma kula kushinikiza kesi zao kusikilizwa, zitaanza kuunguruma Mahakama Kuu ya Tanzania, mwezi huu.
Habari za kuaminika ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa maofisa wa Gereza hilo mwishoni mwa wiki, zilieleza kuwa tayari kesi hizo zimewekwa kwenye kalenda ya mahakama.
Ufafanuzi huo ulitolewa na mmoja wa maofisa wa gereza hilo, aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, kufuatia kuwepo taarifa za mahabusu kuanza mgomo.
"Hapa hakuna mgomo wa mahabusu kwa sababu wote wameishaelezwa kuwa kesi zao zinasikilizwa mwezi huu," kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya gereza hilo.
Alisema ndani ya gereza hilo wapo mahabusu wanaotaka kuishinikiza Serikali iwe inafanya kila kitu wanachotaka,jambo ambalo halikubaliki.
Chanzo hicho kilifafanua kuwa ndani ya gereza hilo wapo wafungwa wanaoshinikiza migomo. "Mahabusu hao ni miongoni mwa wanaoanzisha migomo wakati wanajua wazi kuwa kesi zao zipo mbioni kuanza kusikilizwa," alisema.
Wiki iliyopita baadhi wa mahabusu katika gereza hilo walipenyeza ujumbe kwa njia ya simu kwenye vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa mgomo wa kugomea chakula ili kushinikiza kesi zao zianze kusikilizwa.
Baadhi ya mahabusu hao, walidaiwa hali zao ni mbaya, madai ambayo yalikanushwa na mmoja wa maofisa wa gereza hilo.
Ofisa huyo alidai kuwa awali mgomo wa mahabusu hao ulikuwa ni wakutaka kesi zao zisikilizwe. "Kama tayari mahakama imewapangia tarehe ya kusikilizwa kwa kesi zao ni kitu gani wanataka?"alihoji ofisa huyo.
Mwaka jana mahabusu wa gereza hilo waligoma kula wakipinga kesi zao kutopangiwa tarehe za kusikilizwa.
Mahabusu hao walikuwa wakihoji sababu za kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.Abdallah Zombe, na wenzake ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kusikilizwa haraka wakati wao wamekaa muda mrefu gerezani bila kesi zao kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.
Mgomo huo ulimlazimu maofisa waandamizi wa Idara ya Mahakama na Wizara ya Sheria na Katiba kuwatembelea gerezani na kuzungumza nao.
Mwisho
Categories: