Banner 468

1234453_10201664080105694_1716282793_n
Facebook

Mtoto aunguzwa Dar kisa chakula!

-
Rehema Mwinyi.

Hali ya afya ya mtoto Comfort Kimaro, 7 wa Mbezi Saranga Jijini Dar bado haijatengemaa na anaendelea kuuguzwa katika Hospitali ya Tumbi wilayani Kibaha kutokana na majeraha mabaya ya moto yaliyotokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuunguzwa moto na mke wa baba yake mdogo.

Taarifa zinadai kuwa mtoto huyo, aliunguzwa mwilini kwa mkasi wa moto na mke wa baba yake mdogo anayetajwa kwa jina la Domina Kimaro, kutokana na kosa la kula chakula kilichokuwa kimehifadhiwa kwa ajili ya msichana wa kazi almaarufu kama hausigeli.

Inaelezwa kuwa Comfort ameunguzwa kwa kutumia mkasi uliokuwa ukiwekwa kwenye mafuta ya moto na mke huyo wa baba yake mdogo (Domina) na kisha kupitishiwa mwilini mwake mara kadhaa kwa ni ya kumuadhibu.

Taarifa zinadai kuwa tukio hilo limejiri hivi karibuni, mishale ya saa 4:00 usiku baada ya kubainika kuwa mtoto huyo alikula chakula cha msichana wa kazi.

Imeelezwa kuwa siku ya tukio, mama huyo (Domina) alipandwa na hasira aliposikia kuwa Comfort amekula chakula cha msichana wa kazi na kuamua kuchukua hatua hiyo ya kumuunguza mwilini kwa mkasi uliokuwa ukichemshwa kwenye mafuta ya moto na kumbabua mwilini tena na tena.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amesema polisi wanamshikilia mtuhumiwa Domina na kesho wanatarajia kumpandisha kizimbani.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa Shirika la Elimu Kibaha, ambaye pia ni Afisa uhusiano wa Hospitali ya Tumbi Bw. Gerald Chami, amesema hali ya Comfort bado haijawa nzuri na hivyo anaendelea kulazwa ili apate matibabu zaidi.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa majirani ndio waliomfikisha mtoto huyo hospitalini baada ya kumtwaa toka kwa Bi. Domina aliyekuwa ameshamuunguza mwilini bila huruma na kumuacha ndani pasi na kumpeleka jospitalini.

Mjumbe mmojawapo wa eneo hilo la Mbezi Saranga, Bw. Christopher Francis, amesema kuwa siku ya tukio, mtoto huyo alikuwa akipiga kelele nyingi za kuomba msaada.

Akasema majirani walipojaribu kwenda kumsaidia, wakashindwa kwa vile Domina alikuwa ameufunga mlango wa nyumba na kuendelea kumuadhibu akiwa ndani.

Hata hivyo, akasema yeye na majirani wengine wakaenda tena siku nyingine na kufanikiwa kumpata mama aliyefanya ukatili huo ambaye kazi yake ni kupika na kuuza chakula katika eneo la Saranga Temboni.

Akasema baada ya kumpata walimuhoji kuhusina na adhabu hiyo, lakini mama huyo akakana kuwa hakumuunguza.

Akasema baada ya kuona mama huyo anakwepa tuhuma, walimua kumuhoji msichana wa kazi wa mama huyo ambaye ndiye aliyetakiwa kula chakula kile kinachodawa kuliwa na mtoto Comfort.

Mjumbe huyo wa shina akasema msichana huyo wa kazi ndiye aliyefichua kuwa mtoto huyo alichomwa na mama yake mdogo kwa kutumia mkasi uliokuwa ukilowekwa kwenye mafuta ya moto.

Bw. Fransis akasema kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kutoa taarifa Polisi na mama huyo akapelekwa kituoni kwa ajili ya kutoa maelezo zaidi.

Akasema baadaye majirani waliamua kuchangishana fedha na kupata zaidi ya shilingi 60,000 walizozitumia kumpeleka mtoto Comfort katika hospitali ya Tumbi, ambako hadi sasa anaendelea kutibiwa.

Aidha, alipohojiwa, Comfort amesema mama yake mdogo alikuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara, hasa baba yake mdogo aitwaye Geofrey Kimaro anapokuwa safarini.

Akasema siku ya tukio baba yake mdogo alikua safarini na hakupewa chakula tangu asubuhi hadi jioni na ilipofika mishale ya saa 10:00 jioni, mama yake mdogo alimpa chakula ili akipeleke nyumbani kwa msichana wao wa kazi.

Akasema kwa vile yeye (mtoto) alikuwa na njaa kutokana na kuwa alikuwa hajala chochote, aliamua kukila na ndio maana akajikuta akiunguzwa moto kwa kosa hilo.

Akasema mama huyo alimuunguza kwa kutumia mkasi alioukuwa akiuloweka kwenye mafuta ya moto.

Hata hivyo, akasema baada ya kuunguzwa huko, mama yake mdogo (Domina) hakumpeleka hospitali na badala yake akawa anampaka yai, hali iliyomfanya awe akipata maumivu makali zaidi.

Kwa upande wa mama mzazi wa mtoto huyo Elinani Lalashowi, 36, mkazi wa Moshi ambaye alifika juzi kumuuguza mwanawe baada ya kupata taarifa kutoka kwa shemeji yake aitwae Vicent, amesema hana la kuongea kwa sasa kwani hakuwahi kuwa na ugomvi wowote na mke huyo wa shemeji yake.

Leave a Reply